Habari za Punde

Balozi Seif afungua Kongamano la Umoja wa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu wa Wilaya ya Dimani

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiingia kwenye ukumbi wa Mikutano wa CCM Wilaya ya Dimani  uliopo Kiembe Samaki kulifungua Kongamano la Umoja wa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu wa Wilaya hiyo.

Kushoto ya Balozi Seif anayemshindikiza ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi ambae pia ni Waziri wa Fedha Zanzibar Mh. Omar Yussuf  Mzee.
 Baadhi ya  Wanachama wa Umoja wa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu wa Wilaya ya Dimani wakiafuatilia matukio tofauti kwenye ufunguzi wa Kongamano lao ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Balozi Seif Ali Iddi.
 Balozi Seif Ali Iddi akilifungua Kongamano la Umoja wa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu na Elimu ya juu wa Wil;aya ya Dimani hapo kwenye ukumbi wa CCM wa Wilaya hiyo uliopo Kiembe Samaki.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu na Elimu ya juu wa Wilaya ya Dimani Nd. Abdulazizi  Saleh Khamis akitoa taarifa ya Umoja huo na malengo waliyokusudia kuyatekeleza hapo baadae.

Picha na – OMPR – ZNZ.


Othman Khamis Ame, OMPR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  Iddi ameeleza kwamba Vijana wa karne ya sasa wanaweza kuwa wanasiasa wazuri wenye kuelewa matukio tofauti yanayotokea nchini iwapo watakubali kujifunza Historia halisi ya Visiwa vya Zanzibar kabla na baada ya Mapinduzi ya mwaka 1964.

Alisema harakati za Kisiasa hapa Nchini ziliibua mambo mengi yanayopaswa kusomeshwa Vijana ili kuepuka kubabaishwa na matukio mbali mbali yanayotokea katika kiindi hichi cha mpito ambacho Taifa liko katika matayarisho ya kuingia kwenye uchaguzi wa marejeo ifikapo Tarehe 20  Mwezi huu.

Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo kwenye Kongamano la Umoja wa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu na Taasisi ya Elimu ya juu wa Wilaya ya Dimani lililofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya CCM  Wilaya ya Dimani uliyopo Kiembe samaki.


Alisema  mwananchi hasa Kijana kamwe hataweza kuwa mzalendo kama hatakubali kujifunza  Historia ya Taifa lake hasa ikizingatiwa zaidi kwamba uzalendo na historia ni watoto pacha mambo ambayo yanaokwenda sambamba wakati wote.

Balozi Seif alifahamisha kwamba ni muda mrefu wasomi wengi hapa Nchini wakiionea haya kuisomesha Historia ya Zanzibar kwa sababu wanazozielewa wao wenyewe.

Alisema dalili zinaonyesha wazi kwamba waliowengi wa wasomi hao wanaogopa kusema ukweli wa jinsi mambo yalivyokuwa  wakati wa kudai uhuru hapa Zanzibar kwa kuhofia kutokubalika kwa Watu wa aina fulani.

Alitahadharisha na kusema kusema  hizo ni kasumba mbaya zinazostahiki kupigwa vita na wasomi wa Chama cha Mapinduzi na wanapaswa waachane nazo kwa vile bila ya kuielewa Historia hawawezi kuwa wazalendo wa kweli.

Balozi Seif aliwakumbusha Vijana hao wa Umoja wa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu na Taasisi ya Elimu ya Juu kuelewa matukio ya udhalilishaji yaliyoukumba Uchaguzi  uliopita wa Mwezi Oktoba Mwaka jana ambapo baadhi ya akina mama walilazimika kupewa talaka na waume zao kwa sababu tu za Itikadi za Kisiasa.

Alisema hiyo ni  miongoni mwa mifano hai iliyoshuhudiwa na wananchi walio wengi Nchini ikifanana na ile iliyowahi kufanyika katika chaguzi za wakati wa kudai Uhuru wa Nchi hii  vitendo visivyozingatia haki za binaadamu ambavyo vijana wasomi hao wanapaswa kujifunza ili waepukwe kudanganywa kila kukicha.

Akizungumzia kuhusu suala ya uchaguzi wa marudio unaotarajiwa kufanyika Tarehe 20 mwezi huu Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitoa wito kwa wasomi hao wa vyuo Kikuu kutoa jibu sahihi la kitaalamu linalofafanua kwa nini baadhi ya wanachama wa CCM wana tabia ya kupuuza kushiriki kupiga kura.

Balozi Seif alisema Chama cha Mapinduzi kinafuatilia kwa makini majadiliano ya wasomi hao wa vyuo Vikuu na kuahidi kuyafanyia kazi mapendekezo watakayotoa  kwa kuelewa kuwa mawazo yao ni muhimu kwa uhai wa chama hicho na ndio maana CCM iliamua kuanzisha Mkoa wa Vyuo Vikuu Nchini.

Alisema mara nyingi wanachama wa Chama cha Mapinduzi hupuuza kwenda kupiga kura kitendo kinachosababisha baadhi ya Majimbo kutokufanya vizuri wakishindwa kufahamu kwamba uchaguzi ni kura, bila ya kura za kutosha chama cha Siasa hakiwezi kushinda.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwatoa hofu Wananchi wote wa Zanzibar kuwa uchaguzi wa marudio unatarajiwa kuwa salama, hivyo ni wajibu wa kila Mwananchi kuitumia haki yake ya Kidemokrasia kwa kumpigia kura mgombea wa chama anachokipenda.

Mapema Mwenyekiti wa Umoja wa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu Wilaya ya Dimani Nd. Abdulaziz Saleh Khamis alisema wasomi wengi kwa muda mrefu wamekuwa wakiendelea na tabia ya kuipa mgongo Serikali  kwa kutoitendea haki.

Nd. Abdulaziz alisema vijana wengi bado wanaendelea kusomeshwa na Serikali katika nyanja mbali mbali, lakini hatma yake wanashindwa kuitumikia Serikali na Wananchi wake  walioamua kutumia rasilmali yao ya kodi kuwajengea mazingira bora ya Kitaaluma.

Akigusia uchumi Mwenyekiti huyo wa Umoja wa Wanafunzi wa vyuo Vikuu alisema Taasisi yoyote inayoanzishwa iwapo haikulenga kwenye uchumi uanzishwaji wake utaendelea kuwa na mashaka.

Alisema uchumi wa Taifa utaendelea kuimarika na kuleta tija kwa ushiriki wa pamoja wa wadau wote wakiwemo wasomi wa vyuo vikuu kama suala la amani na utulivu litakuwepo kabla na baada ya uchaguzi mkuu wa marejeo.

Aliiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ile ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kuhakikisha kwamba hali ya amani inakuwepo kwa  kutoa fursa kwa wananchi na Taasisi za umma kuendelea na harakati zake za kimaisha za kila siku.

Akimkaribisha mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa Kongamano hilo  la Wanafunzi wa vyuo Vikuu Wilaya ya Dimani Mwenyekitii wa CCM Mkoa wa Magharibi Nd. Yussuf  Moh’d  Yussuf alisema CCM Mkoa huo utaendelea kuwajengea mazingira bora vijana wake kwa lengo la  kuwapa nyenzo madhubuti  itakayowawezesha kulitumikia Taifa lao kwa upendo na uzalendo.

Nd.Yussuf alisema Taifa lolote wakati wote huwa likitegemea vijana wake ambao ndio wachapa kazi wa baadaye katika kuona Taifa linaendelea kupiga hatua za Maendeleo na Uchumi kwa faida ya Jamii yake.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.