Habari za Punde

Matukio ya uchomaji moto Pemba, wawili washikiliwa na Polisi kwa mahojiano

Haji Nassor na Hassan Khamis Pemba
MATUKIO manane ya uchomaji moto, yaliohusisha nyumba tano zinazoishi watu, ghala la kituo cha afya Kiuyu, tawi la CCM Tibirinzi Chakechake, yameripotiwa kuungua moto usiku wa kuamkia jana kisiwani Pemba.
Taarifa zilizopatikana na waandishi wetu zinaeleza kuwa, tukio la kwanza ni lile lililotokea Kangagani Jimbo la Kojani kwa nyumba mbili zinazokaliwa na watu 10, zikiungua moto baina ya majira ya saa 7:30 na saa 8:30 usiku.
Moto huo ambao haujajulikana chanzo chake, uliwasha nyumba mbili hizo ambazo ziko mbali mbali, na kupatikana chupa cha mafuta ya taa kwenye maeneo hayo.
Akizungumza na waandishi wetu, mmiliki wa nyumba iliokumbwa na kadhi hiyo, mwanzo Hadia Faki Ali (50), alisema awali alijihisi joto kali na ghafla akona moto unawake kwenye paa la nyumba yake.
“Hii nyumba yangu ni ya makuti, sasa nilishituka baada kujihisi joto, lakini ghafla nikaona mota mkali na ndipo nilipomuamsha mume wangu na kuamsha watoto’’,alisema.
Alieleza kuwa, baada ya hapo alipiga kelela usiku huo na ndipo majirani walipooanza kuuzima kwa kutumia maji na vitu kadhaa walifanikiwa kuviokoa na hakukuwa na mtu alipata jeraha.

Aliwataja waliokuwemo kwenye nyumba yake kuwa ni pamoja na yeye, muume wake Suleiman Mohamed (65), watoto wake Time Issa Faki (21), Saada Suleiman Mohamed (18), Hassan Hamad (16), Mohamed Suleiman Mohamed (12) na Lutfiya Abdalla (2) ambo wote walisalimika.
Katika tukio jengine kwenye shehia hiyo ya Kangagani ambapo nayo nyumba iliteketea paa moja na nusu la mkauti, mmiliki wa wake, alisema moto huo uliitokea muda mfupi baada ya nyumba ya awli ilio umbali wa uwanja wa mpira wa miguu kuungua.
Mmiliki huyo Hassan Salim Rashid (40), alisema majira ya 8:20 usiku alipata taarifa hiyo, kwa vile siku hiyo hakulala humo, na alipofika alishuhudia moto ukiwaka kwa kasi ingawa baadae wananchi walifanikiwa kuudhibiti.
“Mimi nawashukuru sana wananchi, maana baada ya kutokezea pamoja na kuwaka kwake kwa nguvu, lakini waliuzima kwa kutumia maji ingawa nyumba haifai kukaliwa’’,alifafanua.
Alisema kikwaida nyumba hiyo inaishi watu watatu ingawa kwa juzi hiyo, wote walikuwa hawapo na kijana alietakiwa kulala hakulala
Sheha wa shehia ya Kangagani Fakih Omar Yussuf, alisema matukio hayo yanamsataajabisha, huku akisema wale wote waliokumbwa na maafa hayo, shehia kwa upande wake itawafikiria.
“Tunao utaratibu wa kusaidiana yanapotokezea majanga kama haya, lakini sasa nimepata funzo kwamba, lazima tuendelee kuimarisha ulinzi kwa kutumia Polisi jamii’’,alifafanua.
Jirani wa nyumba hiyo, Zaina Ali Makame alisema baada ya kusikia moto moto, aliwaamsha watoto wake na kuzima umeme kwenye nyumba yake, na kisha kusaidia kuuzima na kufanikwa.
Aidha waandishi wetu pia baadae walitembelea jengo la Ghala la wizara ya Afya, ambalo zamani lilikuwa kituo cha Afya eneo la Kiuyu ambalo nalo limeteketea lote kwa moto.
Kwa mujibu wa mganga mkuu wa afya wa wilaya ya Wete dk Iddi Juma Mohamed, alisema ndani ya ghala hilo, kuliwa na dawa nusu tani, ambazo zilishapitiwa na muda zikisubiri taratibu za kuziangamiza.
Alisema pamoja na kuwepo kwa dawa hizo zilizoingizwa miezi mitatu iliopita, pia kulikuwa na vitabu vipya vya skuli ya Minungwini, milango 10, madirisha 14 na meza tatu kongwe mali ya Kituo cha Afya cha Mzambarauni kilivyovunjwa.
Kwa upande wake Afisa Mdhamini wizara ya Afya Pemba Mkasha Hija Mkasha, aliwashauri wananchi kujiwekea ulinzi kwenye majengo ya serikali yaliomo kwenye maeneo yao.
“Kwenye ghala hili ambalo zamani lilikuwa kituo cha Afya, sisi wizara hatuna utaratibu wa ulinzi, lakini ni nafasi ya wananchi kubuni ulinzi, maana waathirika wa mwanzo ni wao’’,alifafanua.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa kaskazini Pemba Hassan Nassir Ali, amethibtisha kutoka kwa matukio hayo katika mkoa wake, yakiwemo ya Gando na Micheweni.
Alisema pamoja na moto uliotokezea Kangagani na Kiuyu pia ameshapokea taarifa za kutokea matukio kama hayo, Shehia ya Gando ambako nako nyumba moja nayo imeteketea kwa moto.
“Ni kweli kwenye mkoa wangu usiku wa kuamkia Machi 12 jana, kumesharipotiwa matukio sita ya uchomaji moto, zikiwemo nyumba tano na ghala la Kituo cha Afya Kiuuyu’’,alifafanua.
Wakati huo huo nalo tawi la CCM Tibirinzi wilaya ya Chakechake na nyumba ya makaazi Ziwani, zimeripotiwa kuungua moto hapo jana.

Katika miezi mitatu sasa tayari kisiwani Pemba kumesharipotiwa matukio zaidi ya 13 ya nyumba na matawi ya vyama kuchomwa moto na watu wasiofahamika, ingawa kwa hayo ya jana watu wawili wanashikiliwa na Polisi Mkoa wa kaskazini Pemba kwa mahojiano.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.