Na Takdir Ali, Maelezo-Zanzibar
WAJUMBE wa Baraza la Wawakilishi, leo wamewachagua wajumbe watano kuunda Tume ya Bajeti ya Baraza hilo.
Waliopita katika uchaguzi huo na kura walizopata zikiwa kwenye mabano, ni Hamza Hassan Juma (71), Salha Muhammed Mwinjuma (69), Lulu Msham Abdallah (72), Rashid Ali Juma (71) na Hamad Abdallah Rashid aliyepata kura 70.
Akizungumza kabla ya uchaguzi huo, Naibu Spika Mgeni Hassan Juma, amewaambia wajumbe hao kwamba tume ya bajeti ni nguzo muhimu katika uendeshaji wa shughuli za chombo hicho.
Kwa hivyo aliwataka kufanya kazi zao kwa umahiri, weledi na uaminifu ili kuisaidia serikali katika kutekeleza majukumu yake ya kuwaletea wananchi maendeleo.
Wakitoa shukurani zao, wajumbe hao wateule wamewashukuru wajumbe wa baraza hilo kwa kuonesha imani kubwa kwao, na kuahidi kutumia uzoefu walionao kuhakikisha masuala ya bajeti yanakwenda vizuri.
Hamza Hassan Juma, alisema kamati iliyo imara, italiwezesha baraza kuwa madhubuti na kuipitia vyema bajeti kabla ya kuwasilishwa vikaoni.
Aidha amewataka wajumbe hao wawape ushirikiano kikamilifu ili lengo la kamati hiyo liweze kufikiwa.
No comments:
Post a Comment