Balozi wa Tanzaznia nchini Kuwait, Dkt. Mahadhi J. Maalim,
akiwa katika picha ya pamoja na Bw. Fouad Alghanim, Mwenyekiti wa Umoja wa
Makampuni ya Fouad Alghanim. Kushoto kwa Mhe. Dkt. Mahadhi ni Bw. Sami M.
Al-Farhan, Makamu Wa Rais wa Umoja huo wa Makampuni ya Fouad Alghani
anayeshughulikia masuala ya uwekezaji wa Kimataifa na mwanzo upande wa kulia ni
Bw. Iman Njalikai, Mkuu wa Masuala ya Utawala katika Ubalozi wa Tanzania
Kuwait.
Mhe. Dkt. Mahadhi Juma Maalim, Balozi wa Tanzania
nchini Kuwait akiwa katika mazungumzo na Bw. Fouad Alghanim, Mwenyekiti wa
Umoja wa Makampuni ya Fouad Alghanim.
Balozi wa Tanzania nchini Kuwait Mhe. Dkt. Mahadhi Juma Maalim, , amemtembelea Mwenyekiti wa Umoja wa Makampuni ya Fouad
Alghanim, Bw. Fouad M. T. Alghanim ofisini kwake tarehe 1 Septemba 2016.
Umoja wa Makampuni ya Fouad Alghanim, unajumuisha
zaidi ya Makampuni ishirini ambayo yanajihusisha na masuala mbalimbali ikiwemo
uwekezaji, nishati, mafuta na gesi, usafirishaji, miundombinu, biashara ya
magari, masuala ya anga na ndege, mawasiliano, ujenzi wa makazi ya kisasa,
masuala ya ulinzi, utalii na afya.
Katika mazungumzo hayo, Mwenyekiti huyo alieleza
matarajio yake juu ya ziara atakayofanya hivi karibuni kutembelea Tanzania ili
kujionea fursa mbalimbali za uwekezaji zinazopatikana. Mwenyekiti huyo
alimfahamisha mheshimiwa Balozi kuwa licha ya kutokuwa na shughuli za kiuchumi
nchini Tanzania, Umoja huo unatekelezaji miradi mbalimbali katika nchi za
jirani za Uganda, Rwanda na kwingineko. Aliongeza kuwa, Umoja huo una nia ya
kuwekeza katika sekta mbalimbali Tanzania hususan miundombinu.
Kwa upande wake, Mhe. Dkt. Maalim, alimshukuru
Mwenyekiti huyo kwa kuonesha nia ya kutembelea Tanzania na kuona fursa
mbalimbali za uwekezaji. Vilevile, alimshauri kuangalia namna ambavyo Umoja huo
unaweza kushirikiana na Serikali pamoja na Sekta binafsi hususan katika suala
la ujenzi wa makazi ya kisasa katika Makao Makuu mapya ya Serikali mjini
Dodoma.
Aidha, Mhe. Dkt. Maalim, alipongeza kitendo cha Mwenyekiti
huyo kuamua kufanya ziara Tanzania na kumuahidi kuwa Ubalozi wa Tanzania Kuwait
upo tayari kutoa ushirikiano utakaohitajika ikiwepo kuwapatia taarifa muhimu
kuhusu uwekezaji nchini Tanzania, pamoja kuwakutanisha na wadau muhimu katoka
sekta binafsi na ile ya umma.
No comments:
Post a Comment