Na Mwandishi wetu, Pemba
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kusini Pemba, Shekhani Mohd Shekhani amesema kwamba hali ya amani na utulivu Mkoani humo inaridhisha sana hivi sasa na wananchi wasiwe na wasiwasi wa maisha yao na mali zao.
Amesema madai yanayotolewa na wananchi juu ya kuongezeka kwa vijana wanaotumia madawa ya kulevya ,wizi ,na kuhatarisha amani ya nchi yasiwatie hofu, kwani vijana hao tayari wamesha dhibitiwa na jeshi hilo ambapo vijana saba kesi zao zinashughulikiwa na vyombo vya sheria.
Kamanda Shekhani amesema hayo wakati akifanya mazungumzo yake na vyombo vya Habari kisiwani Pemba ,na kutoa ufumbuzi wa masuala yaliyoulizwa na wananchi wa shehia ya Choga na Matale juu ya ongezeko la vijana wanaotumia madawa ya kulevywa wizi na uvunjifu wa amani.
Wananchi hao wamedai wamekosa imani na Jeshi hilo kutokana na wahalifu wanaopelekwa vituoni na makosa mbali mbali kurudi wakati huo huo kama ni wasafiri ,jambo ambalo kamanda amesema lisiwatie wasi wasi kwani Jeshi hilo linafuata sheria na taratibu za kudhibiti wahalifu na hakuna Rushwa yoyote inayotolewa.
Amesema hali ya amani imeongezeka kwa kiasi kikubwa katika maeneo ya Choga ukiliganisha na hali ilivyokuwa hapo kabla, ambapo makundi ya wahalifu yaliyokuwa yakiwasumbua wananchi yamedhibitiwa na kuwa jeshi hilo litaendelea na msako wake kupambana na wahalifu na kutoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano na Jeshi hilo na kuliimarisha vikosi vya Polisi Jamii.
No comments:
Post a Comment