Habari za Punde

Spika Zuberi Asema Kukamilika Kwa Mradi Huo Kutaibadilisha Zanzibar katika Chati za Kimataifa.

Na. Mwashamba Juma
Spika wa Baraza la Wawakilishi Mhe.Zubeir Ali Maulid alisema Zanzibar inaelekea kukaa kwenye chati ya ramani ya kimataifa kutokana na kuimarika kwa sekta ya Utalii.
Mhe. Maulid aliyasema hayo huko ukumbi wa Z- Ocean Kihinani, wakati akifungua warsha ya siku moja kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuhusu mradi wa ujenzi wa kijiji cha Utalii Matemwe (Penny Royal) huko mkoa wa Kaskazini Unguja.

Alisema kukamilika kwa ujenzi huo kutaleta tiba ya changamoto ya ajira kwa wananchi wa Zanzibar nakueleza kuwa huduma za utalii zinawagusa moja kwamoja Wazanzibari.

Alisema sekta ya Utalii Zanzibar inatoa mchango mkubwa katika kupunguza makali ya maisha kwa wananchi wa Zanzibar kutokana na kuchangia kiasi kikubwa kwenye pato la taifa.

Alisema lengo la warsha hiyo ni kuwafahamisha Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuhusu maendeleo ya mradi huo kwani wao ni washauri wakuu katika masuala ya maendeleo ya nchi. Aidha Aliishauri Wizara ya Habari Utalii, Utamaduni na Michezo kukaa pamoja na Mamlaka ya Uwekezaji (ZIPA) pamoja na Idara ya Uhamiaji ili kusaidia ufanikishaji wa mradi huo.

Akizungumzia utekelezaji wa mradi wa ujenzi huo, Mwanasheria kutoka kampuni ya wanasheria ya Immma jijini Dar es Salaam ambae pia anasimamia mradi huo wa Matemwe (Penny Royal), Casper Msika alisema kampuni kupitia mradi wake wa “Amber Reasort” unampango wa kujenga miundombinu ya mawasiliano, barabara na huduma za jamii zikiwemo afya maji safi na elimu kwa wananchi wa Zanzibar na wakaazi wa kijiji cha Matemwe.

Alisema mradi pia unalengo la kuingia mikataba na maskuli na hospitali za kimataifa kwaajili ya kuwekeza katika kijiji cha Matemwe na kuongeza kuwa lengo la uwekezaji huo ni kutoa huduma bora za afya na elimu kwa Wanzibari ili kuwapunguzia gharama za kuzifuata nje ya nchi yao.

Kuhusu miundombinu ya barabara, umeme na maji safi alisema mradi unania ya kuzalisha umeme wake mwenyewe kwani utahitaji megawati 50 za umeme utakaotokana na nishati ya jua pamoja na taka taka zitakazozalishwa Zanzibar na wanakijiji cha Matemwe.

Aidha alisema mradi tayari umefanya mazungumzo na ZECO, ZAWA pamoja na Mamlaka ya barabara ambapo alieleza wana nia ya kujenga kilomita 22 zitakazozunguka eneo la Mashariki na Magharibi mwa kijiji cha Matemwe kuanzia kijiji cha Kidoti na kueleza kuwa tayari kilo mita 10 za ujenzi wa barabara hiyo umeanza.

Aliongeza kuwa mradi pia unalengo la kujenga nyumba za maendeleo zenye nia ya kutunza haiba ya Zanzibar ambazo zitapewa majina kutokana na uhalisia wa Zanzibar pamoja na kujenga kiwanja cha ndege kikubwa kwenye kijiji hicho cha Matemwe.

Akizungumzia maendeleo ya kilimo kwenye mradi huo, Casper alisema wanatajia kuchukua asilimia kubwa ya wanakijiji kwaajili ya kilimo cha mbogamboga ambao alieleza mradi utawapatia mafunzo, mbinu na vifaa vya kisasa vya kilimo kwaajili ya kuekeza kwenye sekta hiyo.

Hata hivyo alieleza mradi unatarajia kukukamilika baada ya miaka 15 nakuongeza kuwa utatekelezwa kwa awamu sita tofauti sambamba na kueleza awamu ya kwanza itakamilika baada ya miaka miwili kwa kutumia gharama za dola za kimarekani milioni 75 sawa na bilioni sita kwa thamani ya fedha za Tanzania.

Akitoa ufafanuzi wa mgogoro wa ardhi uliopo baina ya Wanakijiji cha Matemwe na Mwekezaji wa mradi huo wa Matemwe (Penny Royal), Waziri wa Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira Mhe. Salama Aboud Talib alieleza serikali ilibaini mgogoro huo baada ya mwekezaji kuanza kulipa fidia kwa wanachi kupitia wakala aliemteuwa mwenyewe bila kuishirikisha serikali.

Hivyo alieleza Wizara yake imeteuwa kamati maalum ya kuratibu malaalamiko ya wananchi chini ya uongozi wa Mkuu wa wilaya ya Kaskazini kwaajili ya kusimamia haki za wananchi.

Akizungumzia ukubwa wa eneo lililotolewa na serikali kwaajili ya mwekezaji huyo, Waziri Aboud alisema serikali imempa hekta 411.8 sawa na ekari 1000 kwa sharti la kuwalipa fidia, kujenga miundombinu ya barabara na maji safi kwa wanachi wa eneo hilo mbali na mikataba mengine na serikali.

Hata hivyo alisema serikali inategemea kupata mapato makubwa kutoka kwa mwekezaji huyo sambamba na kuwaahidi wananchi wa eneo hilo kutoa ushirikiano mzuri ambapo wakati huu serikali inasimamia na kutatuliwa malalamiko yao.

Mapema akizungumza na Wawakilishi wa Baraza la Wawakilishi, Mmiliki wa kampuni hiyo ya Matemwe (Penny Royal), Brian Thomas alisema mradi unalengo la kutoa fursa nyingi za ajira kwa wakazi wa Zanzibar na wanakijiji cha Matemwe.

“Mradi hautobadili maisha wa Wamatemwe pekee, bali ni kwa Wananchi wote wa visiwa vya Zanzibar” alisema Thomson.


Aidha alitumia fursa hiyo kumshukuru rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein kwa nia yake njema ya kuwaletea maendelo wananchi wa Zanzibar kususani kuondosha tatizo la ajira kwa vijana na kinamama wa vijijini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.