Habari za Punde

Wadau walia na DNA kumaliza ubakaji


Na Haji Nassor,
KILA ifikapo Oktoba 11 ya kila mwaka dunia huadhimisha siku ya mtoto wa kike ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni “Kumlinda mtoto wa kike ni wajibu”.

Katika kuadhimisha siku hiyo, ni vyema kwa kila mtu kumlinda mtoto wa kike dhidi ya vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia kama kauli mbiu inavyoeleza ambapo vitendo hivyo hupelekea watoto kuathirika kisaikolojia, kiakili na kimwili.

Zanzibar hali sio shuwari hasa kwa watoto wa kike kutokana na kufanyiwa vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia hasa vitendo vya ubakaji na mimba za utotoni.

Wakati dunia inaadhimisha siku hiyo, mratibu wa kanga Manenity Trust iliyopo katika Hospitali kuu ya Mnazi Mmoja aliwataka wasichana, kujiepusha na mambo yanayopelekea kupata mimba hasa wakiwa chini ya umri wa miaka 18.

Anasema vishawishi, kutojielewa ka watoto wa kike, jamii kutowalinda na utandawazi kunapelekea watoto kubakwa na kupewa ujauzito.

Hospital ya Mnazi Mmoja kupitia kituo cha mkono kwa mkono,  watoto wengi wa kike waliochini ya umri wa miaka 18 wamejifunguwa hospitalini hapo.

Anaeleza kuwa zaidi ya watoto 100 wamejifunguwa tokea mwezi wa Januari hadi mwezi Oktoba mwaka huu,  idadi ambayo ni kubwa haswa ikizingatiwa kuwa bado miili yao haijawa na uwezo wa kujifunguwa, lakini pia hawaja na uwezo wa kulea mtoto wakati wenyewe wanahitaji kulelewa.

Kati ya hao wengine walijifunguwa salama, ingawa wengine walikumbana na matizo kabla na baada ya kujifunguwa na baadhi yao kupoteza maisha kutokana na mimba za umri mdogo.

“Hata hao waliojifunguwa salama kunauwezekano mkubwa wa kupata matatizo baadae kutokana na miili yao bado haijakomaa”alisema Samira.

Chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania TAMWA kinasikitishwa sana na hali ya kuendelea kupewa ujauzito watoto walio chini ya umri wa miaka 18 hapa Zanzibar, jambo ambalo ni hatari kwa mustakbali wa watoto wa kike na wanawake kwa ujumla.

Ofisa kutoka Tamwa, Zanzibar Asha Abdi anasema wasichana wengi wanaopewa ujauzito wanakuwa wako katika masomo na wanahitaji kupata elimu.

Alisema licha ya harakati mbalimbali zinazofanywa na wadau wa masuala ya kijinsia lakini hali bado inaonekana kuwa ni mbaya kwa kuwa kesi hizo zinaongezeka mwaka hadi mwaka.

“Ni wazi kuwa baadae tutapata taswira mbaya kwa wanawake hapa Zanzibar kwa kuwa wengi wao wakishakujifungua ama kuolewa si rahisi kujiendeleza kimasomo”alisema Asha.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kituo cha mkono kwa mkono cha hospitali kuu ya Mnazi mmoja, jumla ya wasichana 112 wenye umri chini ya miaka 18 wamepewa ujauzito kutoka maeneo mbalimbali ya mjini Unguja katika kipindi cha mwaka 2015.

“Kwa mujibu wa kituo cha mkono kwa mkono kimesema kuwa wasichana hao ni wale tu walioripotiwa katika kituo hicho pekee baadala ya kutiliwa mashaka na wazazi ama walezi wao na wengine wamefikishwa hospitalini ya Mnazi mmoja kwa kujifungua”alisema.

Taarifa za zinasema kuwa kati ya wasichana hao 112 waliojifunguwa wasichana 18 wamefariki dunia katika kipindi cha kujifungua na 101 wamejifungua salama.

Lakini pia kituo hicho cha mkono kwa mkono. kimepokea kesi za ujauzito 84 kwa wasichana walio chini ya umri wa miaka mitano katika kipindi cha Januari hadi mwezi Ogasti mwaka huu.

Asha ambae pia ni mratibu wa mradi wa kukuza usawa wa kijinsia (GEWE), anasema kituo cha mkono kwa mkono cha Hospitali ya Mkoa Kivunge Kaskazini Unguja, kimepokea kesi 156 za udhalilishaji wa kijinsia na wengi wao zinawahusu watoto wa kike waliobakwa, kulawitiwa na kubebeshwa mimba.

Kesi zimeripotiwa kati ya mwaka 2015 hadi Mei mwaka huu ambapo wanawake waliofanyiwa vitendo hivyo ni 145 na wanaume ni 11.

“Kwa mwaka 2015 pekee kumeripotiwa kesi 118 kati ya hizo wanawake ni kesi 110 huku wanaume ni kesi nane (8), ambapo mwaka huu kuanzia Januari hadi Mei tayari kesi 38 zimesharipotiwa kituoni hapo na kati ya hizo wanawake ni 35 na wanaume ni watatu”,alifafanua.

Yeye anaona kukosekana kwa Mashine ya kuchukuza vinasaba (DNA) Zanzibar, kumeelezwa kuchangia kushindwa kuwatia hatiani wahalifu wanaowapa ujauzito watoto wa kike.

Sasa basi mwanasheri kutoka Jumuiya ya wanasheria wanawake Zanzibar, ‘ZAFELA’ Sada Issa anabainisha kuwa wahalifu hao baada ya kuwapa watoto ujauzito, huwa wanaukana ujauzito huo kwa kutokuwepo kwa DNA.

Anasisitiza kuwa, mhalifu huyo akishakana kuwa hahusiki na ujauzito huo,  inakuwa vigumu mno kumtia hatiani mpaka kupatikane kwa mashine ya DNA, ili kuweza kuchunguzwa vinasaba vya washutumiwa.

Kesi za watoto waliopewa ujauzito zinakwama kwa sababu jeshi la Polisi mpaka lipeleke vinasaba jijini Dar -es Salam kwa ajili ya uchunguzi na kisha kuendelea na kesi.

Aliwapigia magoti wasimamizi wa kesi za ubakaji,  kutenda haki kwa pande zote mbili kwa mlalamikaji na mlalamikiwa ili sheria iweze kuchukua mkondo wake na kuweza kukomesha mtendo hayo.

Waendesha mashitaka wanasema kwa sauti kubwa, misingi mikuu ya mashtaka ipo katika ushahidi na kesi bila ya ushahidi haiwezi kufikishwa mahakamani na wahalifu kupewa adhabu.

Mzazi wa mtoto mwenye kesi ya ubakaji na kupewa ujauzito kutoka Mtambile, anesema kumekuwepo na changamoto nyingi katika ufuatiliaji wa kesi za ubakaji, ikiwemo baadhi ya watu kushindwa kutoa ushahidi.

“Mimi naamini tatizo hili sio tu kwamba ni uzembe wa polisi,  lakini ni wakati sasa kesi hizi iwepo DNA  hapa Zanzibar, maana kw akuitegemea ilioko Dar –es Salaam kesi zitakaa zaidi ya mwaka mmoja matokeo hayajarudi kutoka Muhimbili”,alisema.

Mwanaharakati wa kutokomeza mimba za umri mdogo mjini Chakechake Khadija Hussein Makame, anasema jamii imekuwa ikililaumu jeshi la polisi pekee, bila ya wao kujiangalia wanavyokuwa wazito kutoa ushahidi mahakamani.

Alisema kuwa asilimia 90 ya kesi za ubakaji na mimba za utotoni zinaishia kwa kusuluhishana katika ya walalamikaji na walalamikiwa na kesi hizo kuzimaliza wenyewe.

Lakini Mwanasheria Ali Haidari, anasema kuwa kunamapungufu mengi ya sheria ambayo yanaweza kuelekea mtoto kukosa haki zake na kukutana na masuala ya udhalilishaji wa watoto.

Alisema zipo changamoto ambazo zinawagusa watoto hasa katika masuala ya sheria mfano sheria ya adhabu.

Alisema sheria hiyo ya adhabu na 6 mwaka 2004 ambapo sheria hiyo imezungumza mambo mazuri sana lakini katika masuala ya watoto kunamapungufu katika kulinda haki yake hasa kipengele cha 14.

“Kifungu hicho kinasema mtoto wa kiume aliyechini ya umri wa miaka miaka 14 atadhaniwa kuwa hawezi kufanya kitendo cha kujamiyana…..bado kunawatetezi wa haki za watoto tunamashaka na sheria hiyo”,alisema.

Alisema kifungu chengine kinachokizana na maslahi ya mtoto 126 ambacho kimeweka adhabu ya kupatikana kwa hatia ya kubakwa kwa mwanamke au mtoto kuweka adhabu ya kifungo cha miaka 30 pamoja na faini lakini uzoefu unaonesha kuwa faini hazilipwi.

Mwanaharakati wa mambo ya watoto, Salama Mbarouk anasema sheria ya mtoto namba 6 ya mwaka 2011 ya Zanzibar, kunabadhi ya vifungu viangaliwe tena ili kuweza kuyalinda maslahi ya watoto.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.