Habari za Punde

Kamati ya ‘Shihata’ yachiriza machozi Mkamandume Pemba


Na Haji Nassor, PEMBA
KAMATI ya Mifugo, Utalii, Uwezeshaji, na Habari ya Baraza la wawakilishi imesema haikuridhishwa na hali mbaya iliopo eneo la kihistoria la Mkamandume Pujini wilaya ya Chakechake Pemba, na kuiagiza Idara husika kuliokoa haraka eneo hilo.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Ali Suleiman Shihata, wakati walipofika eneo hilo kwa ajili ya kulikagua na kusikitishwa kutokana na kuanza kupotea kwa historia ya majengo.
Alisema ukisoma historia iliomo kwenye mitandao, au vitabu vya ndani na kisha kuliona dhahiri eneo hilo ni ukweli usiofichika kuwa, hali ni mbaya.
Mwenyekiti huyo alisema, katika hilo wala hakuna la kufichana maana ukweli unaonekena, kuwa historia ya majengo ya asili ya eneo hilo la Mkamandume, limeanza kupotea.
“Mimi hapa sijaona kitu, nashuhudia mawe yalioporomoka na makuta, sioni jambo lolote, jamani huo ndio ukweli lazima wizara na Idara husika zijipange haraka’’,alifafanua.
Nae mjumbe wa Kamati hiyo, mwakilishi wa Jimbo la Welezo Unguja, Hassan Khamis Hafidh alisema hakuna kitu kikubwa cha kuwavutia watalii kwenye eneo hilo.
“Ukisikia historia ya eneo hili, na hadithi zilivyo na kisha kutembelea hapa, wala hakuna jambo jipya, lazima wizara hapa ipaimarishe’’,alifafanua.
Mapema kamati hiyo ilishauri wizara ya habari kuwepo mfanyakazi saa 24 kwenye eneo hilo la kihistoria, ili kuwaepusha watembeza watalii kujipenyeza na kuikosesha mapato serikali.
Akitoa maelezo ya eneo hilo, Kaimu Mkuu wa Idara ya Makumbusho na Mambo ya Kale Pemba Salim Seif alisema, kwa sasa kutokana na kutoimarishwa kuna uhabwa wa wageni wanaotembelea.
“Tatizo jengine lililopo hapa, ni baadhi ya watembeleza watalii, kuja kisiri siri na kuwaleta wageni na kisha mapato kuingiza mfukoni mwao’’,alifafanua.
Mkurugenzi mipango sera na utafiti wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Zanzibar Mahamoud Omar Hamad, alisema wizara inaandaa kitabu maalumu cha pamoja kinachoelezea historia ya eneo hilo.
“Kwa sasa tumegundua kuwa, kila mtu anahistoria yake juu ya eneo la Mkamandume, na inawezekana ikawa ni moja ya sababu ya kukosa wageni’’,alifafanua.
Kwa upande wake Afisa Mdhamini wa wizara hiyo Pemba, Khatib Juma Mjaja, alisema pamoja na matayarisho ya kitabu hicho, lakini kwa sasa wanaandaa vipindi, ili kuyatangaaza maeneo kama hayo.
“Tunampango kwa kushirikiana na shirika la utangazaji Zanzibar, ZBC kufanya vipindi vya hazina yetu iliofichika, ambapo kinayaibua maeneo kama haya ya Mkamandume’’,alieleza.

Kamati ya Mifugo, Utalii, Uwezeshaji, na Habari awali ilitembelea eneo hilo, chumba cha chini ya bahari Makangale, Vuma wimbi eneo la kujifurahisha kwa wananchi na kisha kufanya majumuisho uwanja wa michezo Gombani.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.