Na
Abdi Shamnah
WAZIRI
wa Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Mhe. Rashid Ali Juma, amawataka wadau wa
Utalii wanaolenga kuitangaza Zanzibar katika maeneo mbali mbali ya dunia,
kuelekeza nguvu katika maeneo mapya yalioibuliwa.
Alisema
kuna umuhimu wa wadau hao kuelekeza nguvu zao katika kutangaza vivutio vipya
vya utalii, hususan vinavyogusa utamaduni wa Wazanzibari.
Changamoto
hiyo ameitoa ofisini kwake Kikwajuni, alipokuwa na mazungumzo na Mkurugenzi wa
Makampuni ya Naif Company Limited na Naif Engineering Company, Bi.Khadija Naif,
alipofika nchini kwa lengo la kuangalia vivutio vya utalii vilivyopo pamoja
kuwashajisha wajasiriamali wa Zanzibar kutangaza biashara zao katika nchi za Ghuba.
Alisema
kwa kipindi kirefu kumekuwa na juhudi za kuutangaza Utalii wa Zanzibar, kupitia
vivutio mbali mbali, ikiwemo historia, inayohusisha utawala wa kisultani,
fukwe, magofu na makumbusho.
Alisema
wakati umefika kwa wadau wa utalii nchini, kuutangaza utalii wa Zanzibar katika
nyanja za kiutamaduni na kubainisha kuwepo maeneo mengi, vikiwemo vyakula vya
asili vinavyoliwa na wenyeji.
Aidha
alisema eneo jengine ni kuhusiana na mavazi ya Wazanzibari, ambayo kimsingi
yanafanana na yale yanayovaliwa na wananchi wa nchi za Ghuba, sambamba na
urembo wa asili, ukiwemo ule utokanao na miti na rasilimali zake.
Aidha
alisema hatua ya UNESCO kuizawadia Zanzibar kuwa kituo cha Hifadhi ya
kimataifa, kutokana na uhifadhi wa kimaumbile wa misitu yake pamoja na wanyama
walio na tabia tofauti duniani, ni vyema wadau hao wakachukua jukumu la
kuitangaza.
‘UNESCO
imetuzawadia kwa kuwa na misitu ya kimaumbile, lakini pia tuna wanyama walio
tofauti na wengine wote duniani, tunao wanyama wenye uwezo kwa siku kula miti
mia moja ya aina tofauti, bila kuathirika, jambo ambalo sio la kawaida na
inapotokea kutaka kuathirika hutafuta makaa kama tiba’’, alisema.
Vile
vile Waziri huyo alisema kuanza kwa safari za mashirika tofauti ya ndege hapa
Zanzibar, ni ishara tosha kuwa utalii wa Zanzibar unaendelea kuimarika kadri
siku zinavyosonga.
Alisema
kutokana na juhudi mbali mbali zinazochukuliwa na wadau, asasi zisizo za
kiserikali na taasisi za Serikali, kuna mwelekeo mzuri wa kufikia malengo ya
kupokea hadi watalii 360,000 ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.
Waziri
Rashid alimpongeza Mkurugenzi huyo, kwa
uzalendo anaonesha katika kuutangaza utalii wa Zanzibar, na kuthibitisha hoja
kuwa utalii utaimarishwa na wadau wa sekta hiyo na sio taasisi za Serikali.
Nae,
Mkurugenzi Naif, alisema amefarijika mno kufika hapa Zanzibar, na kupata fursa
ya kutembelea maeneo mbali mbali pamoja na kuangalia vivutio vya utalii.
Alisema ametumia fursa hiyo kuwahamasisha
wajasiriamali wadogo wadogo wa Zanzibar kuandaa mazingira ya kutangaza bidhaa
zao katika nchi za ghuba.
Alisema
akiwa wakala wa utalii kutoka Saud Arabia atafanya kila juhudi kuhakikisha anautangaza
vyema utalii wa Zanzibar, pamoja na kuwaunganisha wajasiriamali wa Zanzibar ili
waweze kutumia fursa zilizopo nchini humo kwa kuuza bidhaa zao.
Aidha
alisema anakusudia kuwaunganishi kati ya wafanyabaishara wa Saud Arabia na wajasiriamali
wa Zanzibar ili waweze kutumia fursa za kupata bidhaa kutoka huko, kwa makubaliano
ya Kibenki, ili kujiendeleza kimaisha.
Katika
ziara hiyo Mkurugenzi huyo, alipata fursa ya kuzungumza na Mkurugenzi wa
Jumuiya ya wafanyabaishara, Wenye viwanda na wakulima,Bi. Munira Houmud na Waziri
wa Nchi Ofisi ya Rais, Mwenyekiti wa Baraza la Mpinduzi,Mhe. Issa Haji Ussi.
No comments:
Post a Comment