Habari za Punde

Wanafunzi sekondari Mahonda wapagawa wakifanya Mtihani wa darasa la 12

Na Othman Khamis, OMPR


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewakumbusha Wazee Nchini kuendeleza Dua kupitia Kamati za Skuli kabla ya Wanafunzi wa Skuli zao kuanza kufanya Mitihani yao ili kuwaepusha Wanafunzi wao kukumbwa na vitendo vya kupagawa wakati wakiendelea na mitihani yao.

Alisema wanafunzi  wanalazimika kuwa na akili timamu pamoja na utulivu wakati wanapofanya Mitihani yao ikiwa ni daraja ya kupimwa uwezo wao kitaaluma kama wanaweza kuendelea na taaluma yao ya juu baada ya mitihani hiyo.

Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akizungumza na Uongozi wa Kamati za Skuli za Msingi na Sekondari za Mahonda kufuatia Wanafunzi wa Darasa la 12 la Skuli hiyo kukumbwa na kizaa zaa cha kupagawa wakati wakiendelea kufanya Mtihani wa somo la Geography  mchana wa Tarehe 5 Oktoba mwaka huu skulini hapo.

Balozi Seif ambae pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda akiwapa pole Walimu, Wanafunzi, Uongozi wa Kamati ya Skuli  pamoja na Wazazi alisema wanafunzi lazima wajengewe mazingira mazingira mazuri ya kutafuta elimu katika misingi ya amani.

Alisema uongozi wa Kamati ya Skuli ya Mahonda unapaswa kutafakari katika kutafuta mbinu za kukabiliana na matukio kama hayo kwa vile tayari masuala ya kuchagawa yameshawahi kutokea katika mitihani iliyopita kwenye skuli hiyo.

Alifahamisha kwamba taifa linahitaji kuwa na vijana waliotaalamika kimaadili na kitamaduni lengo ni kuwarithisha dhamana ya kulitumikia Taifa lao kwa upendo na uzalendo uliotukuka.

Akitoa taarifa ya tukio hilo la kuchagawa kwa wanafunzi wa darasa la 12 wanaoendelea na Mitihani yao hivi sasa Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Sekondari ya Mahonda Mwalimu Rashid Abdullah alisema jumla ya wanafunzi 22 walipagawa na Mmoja kuzimia wakati wakifanya Mitihani ya somo la Geography.

Mwalimu Rashid alisema baadaye kufuatia kisomo kilichoendeshwa na wazazi wa  pamoja na walimu wa Skuli hiyo kiliwezesha wanafunzi sita kupata nafuu na kuendelea na mitihani yao kama kawaida.

Alisema siku iliyofuata tatizo hilo likaendelea tena hadi kilipop[itiushwa kisomo chengine na hatimae wanafunzi hao wakaendelea kufanya Mitihani yao kama kawaida.

Akitoa shukrani kwa niaba ya Uongozi wa Kamati ya Skuli za msingi na Seokondari Mwenyekiti wa Kamati hiyo kwa upande wa Sekondari Bwana Salum Gharibu alilipongeza Jeshi la Polisi kwa hatua lililochukuwa la kukabiliana na tatizo hilo.

Bw. Gharib alisema Uongozi wa Kamati yake kwa kushirikiana na walimu na wazazi wa wanafunzi wa skuli hiyo walilazimika kusoma dua maalum kwa nia ya kumuomba Mwenyezi Muungu kuwaondoshea kadhia hiyo iliyoleta sintafahamu wakati mzito wa mitihana ya watoto wao.

Mapema Msaidizi Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Msingi ya Mahonda Mwalimu Sabina Hassan Choum alielezea kusikitishwa kwake  na  tabia ya baadhi ya Watu wa Mtaa kuacha husda dhidi ya watoto wao walioko katika kipindi cha mpito kuelekea katika daraja nyengine ya Taaluma.

Bibi Sabina alisema vitendo vya shirki vilivyoshuhudiwa na baadhi ya walimu na wanafunzi hao wakati wa asubuhi kabla ya kadhia hiyo vikihusisha mayai yaliyoandikwa Quran mbali ya kwenda kinyume na maarisho ya Imani za Dini lakini pia vinachangia kuvunja moyo walimu na wanafunzi hao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.