Habari za Punde

Rais DK Shein azipongeza Serikali za Cuba na Oman kwa kuiunga mkono Zanzibar katika miradi ya kimaendeleo

 
STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
  Zanzibar                                                                    27.12.2016
---
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameipongeza Serikali ya Oman na  Serikali ya Cuba kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuendeleza miradi ya maendeleo sambamba na kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya Zanzibar na nchi hizo.

Akizungumza kwa nyakati tofauti wakati alipokutana na Mabalozi wa nchi hizo Ikulu mjini Zanzibar hivi leo, Dk. Shein alizipongeza nchi hizo kwa kuendeleza uhusiano na ushirikiano wa kihistoria ambao umekuwa chachu katika kuimarisha juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kujileta maendeleo.

Akizungumza na Balozi wa Cuba katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anaemaliza muda wake wa kazi hapa nchini, Jorge Luis Lopez Tormo, Ikulu mjini Zanzibar, viongozi hao walisisitiza haja ya kuendelea kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya pande mbili hizo.  

Katika Mazungumzo hayo, Dk. Shein alisema kuwa Cuba ina historia kubwa katika juhudi za kuiunga mkono Zanzibar kwenye sekta za maendeleo hasa sekta ya afya kwani tokea mwaka 1964 nchi hiyo imekuwa ikileta madaktari wake kuja kufanya kazi hapa Zanzibar.

Alieleza kuwa mbali ya madaktari hao kuja kufanya kazi kwa kutoa huduma ya afya kwa jamii hapa nchini, Cuba imekuza uhusiano wake kupitia sekta hiyo kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuanzisha chuo cha Udaktari ambacho tayari kimeshaanza kuza matunda kwa kutoa Madaktari Wazalendo.

Aidha, alisema kuwa mbali ya ushirikiano wa sekta ya afya alieleza haja ya kuanzishwa ushirikiano katika sekta ya utalii kutokana na Cuba kupiga hatua kubwa katika sekta hiyo.

Dk. Shein alisema kuwa Zanzibar ina mengi ya kujifunza kutoka kwa ndugu zao wa Cuba kutokana na nchi hiyo kujiimarisha kwenye sekta ya utalii sambamba na vyanzo vyake vya utalii yakiwemo maeneo ya kitalii likiwemo eneo maarufu la ukanda wa kitalii la ‘Varadero’.

Sambamba na hayo, Dk. Shein alisema kuwa ushirikiano huo pia, utahusisha mji Mkongwe wa Zanzibar na ule mji Mkongwe wa Havana ambao yote kwa pamoja ina historia kubwa pamoja na vivutio kadhaa  vya kitalii ndani yake.

Pia, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kwa mara nyengine tena kutoa mkono wa pole kwa kifo cha kiongozi shupavu na mpigania haki za wanyonge marehemu Fidel Castro, na kumtumia salamu Rais Raul Castro za kumtakia afya njema yeye na wananchi wa Cuba ili waendelee kulijenga taifa hilo.

Dk. Shein alisisitiza haja kwa nchi hiyo kuunga mkono azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuwasomesha madaktari wazalendo katika vyuo vikuu vya afya nchini humo kupitia kada maalum za udaktari kwa kiwango cha elimu ya juu kwa ufadhili wa SMZ.

Nae Balozi Jorge Luis Lopez Tormo alimuhakikikishia Dk. Shein kuwa Cuba inathamini sana uhusiano na ushririkiano wa kihistoria kati yake na Zanzibar na kuahidi kuendelea kuudumisha.

Balozi huyo wa Cuba kuwa miradi yote ya maendeleo inayoishirikisha nchi yake itaendelezwa kwa juhudi kubwa huku akimueleza Dk. Shein kuwa nchi yake itafarajika kwa kuwepo ushirikiano katika sekta ya utalii.

BaloziTormo alisema kuwa kwa mwaka huu pekee,  Cuba imeweza kupokea watalii wapatao milioni tatu na nusu na kukiri kuwa mfanano wa miji mikongwe ya Zanzibar na Havana unaweza kuwa chachu katika kukuza utalii kwa pande zote mbili.

Mapema, Dk. Shein alifanya mazungumzo na Balozi Mdogo mpya wa Oman, Ahmed Bin Humoud Al Habsi, ambapo alitumia fursa hiyo kuipongeza Oman kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika harakati zake za kukuza uchumi na kuimarisha maendeleo.

Dk. Shein alieleza kuwa miongoni mwa juhudi zilizochukuliwa na Oman katika kuisaidia Zanzibar ni pamoja na ujenzi wa Chuo cha Afya kilichopo Mbweni pamoja na fedha taslim kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya Kiwanda cha Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali, msaada wa gari kwa ajili ya viongozi wa Serikali na misaada mengine ambayo nchi hiyo imeshawi kuitoa.

Aidha, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kumpongeza Sultan Qabous Bin Said Al Said na Serikali yake kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar na alimtaka  Balozi huyo wa Oman amfikishie salamu zake kwa kiongozi huyo.

Nae Balozi Ahmed Bin Humoud Al Habsi, ambaye amechukua nafasi ya Balozi Mdogo wa Oman aliemaliza muda wake wa kazi hapa Zanzibar, Ali Abdulla Al Rashdi alieleza kuwa Oman itaendeleza uhusiano na ushirikiano wake kati yake na Zanzibar na kupongeza hatua za maendeleo zilizofikiwa hapa nchini.

Aidha, Bin Mahmoud alisema kuwa Serikali ya Oman inatambua juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Dk. Shein za kujiletea maendeleo hivyo, Oman itaendelea kuziunga mkono juhudi hizo ili  Zanzibar izidi kupata mafanikio.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar


Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.