Habari za Punde

WADAU WAOMBWA KUJITOKEZA KUDHAMINI MIRADI INAYOLENGA KUTATUA CHANGAMOTO KATIKA JAMII

Na: Frank Shija – MAELEZO

WADAU waombwa kujitokeza na kuongeza kasi ya udhamini wa miradi inayotekelezwa kwa malengo ya kukwamua jamii kuondokana na changamoto mbalimbali wanazo kabiliana nazo.

Hayo yamebainishwa leo Jijini Dar es Salaam na Katibu wa Mradi wa Binti Jitambue  Bi. Lilian Boniface wakati wa mkutano wao na wahandishi wa habari kuhusu tathmini ya utekelezaji wa mradi huo kwa kipindi cha miezi 11.

Awali akifafanua changamoto walizokumbana nazo katika utekelezaji wa mradi huo Lilian amesema uhaba wa rasilimali fedha imekuwa kikwazo kikubwa kwao katika kutekeleza kwa ufasaha malengo ya mradi huo katika baadhi ya maeneo.

“Nitumie fursa hii kutoa wito kwa Serikali na wadau wote wa maendeleo kutoa  ufadhili kwa ajili kuimarisha utekelezaji wa mradi huu wa “Binti Jitambue” ili wasichana wengi zaidi waweze kunufaika na mradi huu muhimu kwao,” alisema Lilian.

Kwa upande wake Meneja wa Mradi wa Binti Jitambue, Sara Bedah Akwisombe amesema kuwa licha ya changamoto wanazokumbana nazo wamefanikiwa kuwafikia watoto wa kike wenye umri kati ya miaka 10 hadi 16 wapatao 4000 nakuwapatia elimu juu ya Afya ya uzazi,, makuzi na kujitambua.

Aliongeza kuwa tathmini ya mradi huo imebaini kuwa takribani asilimia 80 ya wazazi hawapati muda wa kukaa na kuwaelimisha watoto wao juu ya masuala mbalimbali yanayohusu malezi na makuzi.

Katika kutekeleza azma hiyo mwaka 2017 mradi huu pia utatekelezwa katika mkoa wa Tanga ikiwa ni muendelezo wa jitihada za kuwasaidia watoto wa kike kujitambua na kutambua thamani na fursa zao katika jamii.

Binti Jitambue ni mradi ambao umeanzishwa tarehe 30 Januari, 2016, kwa lengo la kusaidia utipatikanaji wa elimu ya afya ya uzazi, malezi na makuzi, elimu ya kujitambua utu na thamani kwa watoto wa kike, ambapo awamu ya kwanza umetekeleza katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Kirimanjaro chini ya uratibu wa Taasisi ya Tanzania Youth Vision Association (TYVA) ya jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.