Habari za Punde

Wakulima wa mwani watakiwa kujiepusha na vitendo vya udanganyifu wanapouza mwani

Na Salmin Juma, Pemba

WAKULIMA wa zao la mwani  Kisiwani  Pemba wametakiwa kujiepusha na vitendo vya udanganyifu kwa kuchanganya  takataka , majani pamoja na mchanga katika magunia ya mwani ili kuongeza uzito wakati wanapokwenda kuuza mwani wao .

Akizungumza na wakulima wa zao hilo wa  mikoa miwili ya Pemba katika Ukumbi wa mikutano wa kilimo Weni , Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Uvuvi Mussa Aboud Jumbe amesema kuwa kitendo hicho kimechangia kushuka bei ya zao hilo .

Amesema kuwa wapo baadhi ya wakulima ambao wamekosa uwaminifu na hivyo kufanya vitendo ambavyo havikubaliki kisheria kwa kuongeza vitu visivyo hitajika lengo lao ikiwa ni kuongeza uzito ili waweze kupata fedha nyingi .

Amesema , ni vyema kila mkulima kuacha vitendo vya udanganyifu na azingatie suala la kuimarisha usafi wa mwani , jambo ambalo litazidi kuyashawishi makampuni yanayonunua zao hilo kuweza kuongeza bei wenyewe na kuwanufaisha zaidi wakulima wengi.

“Wapo wakulima ambao sio waaminifu ambao wamekuwa wakichanganya takataka , majani na mchanga kwenye maguni ya mwani wanapokwenda kuuza  ili kuongeza uzito jambo ambalo linachangia kushuka bei ya zao hilo ”alisema .

Aidha akizungumzia suala la utitiri wa kampuni zinazonunua zao hilo , Mkurugenzi amesema Serikali inakusudia kukutana na kampuni hizo ili kujua uhalali wake , mitaji yao pamoja na ofisi zao na kampuni itakayobainika kutotimiza masharti itazuiwa kununua zao hilo .

“Katika Ofisi yangu  yapo majina ya kampuni zaidi ya 18 yanayojihusisha na ununuzi wa mwani lakini baadhi ya mengine hayana ofisi , mitaji yao hayaeleweki na nyingine kutokuwa na uhalali  kisheria wa kufanya kazi hiyo , tutafanya uhakiki na ambazo hazitatimiza masharti tutaziondoa ”alifahamisha.

Naye Rashid Omar Matar kutoka Shumba Mjini Wilaya ya Micheweni akizungumza kwa niaba ya wakulima wenzake  ameiomba Serikali kuingilia kati suala la kushuka bei ya zao hilo kutokana na kwamba limekuwa likisaidia jamii katika kukabiliana na ukali wa maisha.

Amesema ni vyema Serikali kulichukua zao hilo na kuliingiza katika mazao yanayoshuhulikiwa na Shirika la Taifa la Biashara Zanzibar (ZTSC) kama ilivyo  kwa zao la karafuu .

“Zao la mwani ni mkombozi kwa wananchi wenye kipato cha chini ,hivyo tunaiomba Serikali ilichukuwe na kuliingiza kwenye orodha ya mazao yanayonunuliwa na Shirika la ZSTC kama ilivyo kwa zao la karafuu ”alishauri.

Hata hivyo washiriki wa kikao hicho wamepongeza hatua ya serikali ya kutaka kuboresha bei ya zao hilo na kuahidi kuendelea kuzalisha licha ya bei  ya sasa ya shilingi 400 kwa kilo kuwa haikidhi haja kulingana na ugumu wa kazi yenyewe.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.