Habari za Punde

Balozi Seif ayapokea matembezi ya UVCCM yaliyohitimishwa Afisi Kuu ya CCM

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akivishwa Skafu na Vijana wa Chipukizi kabla ya kuyafunga matembezi wa UVCCM yaliyohitimishwa hapo Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Mjini Zanzibar.

 Vijana wa UVCCM wapatao 400 wakihitimisha matembezi yao ya kuadhimisha miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyopokelewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hayupo pichani.

 Balozi Seif akipokea Picha ya Muasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Aman Karume iliyotumiwa na Vijana hao katika matembezi yao Wa kwanza kutoka kulia ni Kaimu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM Tanzania Ndugu Shaka Hamdu Shaka NA Makamu Mwenyekiti wa Umoja huo  Bibi Mboni Muhita.
 Balozi Seif akipokea Picha ya Muasisi wa Muungano wa Tanganyka na Zanzibar  Marehemu Mwalimu Julius K. Nyerere iliyotumika kwenye matembezi hayo.
  Vijana wa UVCCM wakimkabidhi Bendere ya Zanzibar Balozi Seif waliyoitumia kama kielelezo kwenye matembezi yao ya kuunga mkono sherehe za kutimia miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
 Balozi Seif akipokea Bendera ya  Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania iliyotumiwa na Vijana hao kwenye matembezi yao tokea  walipoanza juzi katika Kijiji cha Donge Mkoa wa Kaskazini Unaguja.

Picha na –OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis, OMPR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Taifa linawategemea Vijana  wakati wowote katika dhana nzima itakayothibitisha kwamba wanasimamia kwa vitendo Mapinduzi katika kuondoa maovu yote yanayolikabili Taifa.

Alisema Serikali zote mbili ile na Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na iIe ya Mapinduzi ya Zanzibar zinataka kuona  Vijana wake wanakuwa chem chem ya Maendeleo badala ya kuwa dimbwi la matatizo mitaani.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati akiyafunga Matembezi ya Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi { UVCCM } kuunga mkono maadhimisho ya sherehe za kutimia miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964  hapo Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Mjini Zanzibar.

Alisema Vijana ambao ndio warithi wa kulinda Mapinduzi ya Zanzibar dhana iliyoanzishwa  na muasisi wa Mapinduzi hayo Mzee Abeid Amani Karume wana wajibu wa  kusimamia vita vya mapambano dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya, udhalilishaji wa wanawake na watoto,  uonevu  pamoja na ufisadi.

Balozi Seif alikariri maneno ya Marehemu Mzee Abeid Amani Karume yaliyoeleza maana halisi ya Mapinduzi daima ambayo sio kupindua watu bali ni kuondoa matendo mabaya katika jamii na kusimamia haki na mazuri yote.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  itaendelea kuondoa matendo yote maovu ikiwemo uzembe, uonevu na ubaguzi mambo yanarejesha nyuma au kukwamisha juhudi za Taifa  za kuleta Maendeleo ya Umma.

Alieleza faraja yake kuona ushiriki wa Vijana katika matembezi hayo ni mkubwa kiasi kwamba wanalidhihirishia Taifa na Viongozi wake jinsi gani walivyokomaa  kisiasa pamoja na utayari wao unathibitisha kwamba wako imara kutetea kwa vitendo Mapinduzi ya Zanzibar yaliyoondoa madhila ya Kikoloni.

Akizungumzia changamoto kubwa zinazowakabili Vijana hasa  ukosefu wa ajira ambalo limekuwa likizikumba nchi mbali mbali Duniani  Balozi Seif alisema Takwimu za Kimataifa zinathibitisha wazi kwamba zaidi ya Vijana 73 Milioni wanakadiriwa kuwa hawana ajira.

Alisema kwa bahati mbaya mara nyingi changamoto hii ya ukosefu wa ajira kwa Vijana huhusishwa kuwa ndio chanzo cha vitendo viovu vinavyofanywa na Vijana katika Mataifa mbali mbali Duniani.

Balozi Seif alifahamisha kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  imeandaa Mipango imara ya kukabiliana na changamoto hiyo  hali inayobainisha kuwa sio nzuri na jamii imekuwa ikishuhudia nafasi moja ya ajira nchini kugombewa  na vijana zaidi ya 20.

Alisema miongozi mwa mipango hiyo ni kuongezwa kwa nafasi za  mafunzo ya amali Nchini ambapo Vituo Vipya  Viwili vya amali vinategemewa kujengwa  huko Makunduchi Mkoa Kusini  kwa upande wa Unguja na Mtambwe  Mkoa wa Kaskazini kwa upande wa  Pemba.

Balozi Seif alisema Vituo hivyo vitafanya idaidi ya vituo Vinne vya mafunzo ya Amali nchini vitakavyotegemewa kuchukuwa  idadi kubwa ya Vijana katika kupata taaluma  itayowasaidia kuwa na uwezo wa kujiajiri wao wenyewe hapo baadaye.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alielezea mpango mwengine wa uhakika uliobuniwa na Serikali wa kupambana na ukosefu wa ajira ni suala la kukuza uchumi kwa njia ya kukaribisha wawekezaji kwenye Sekta ya Utalii.

Alisema mradi mkubwa wa sekta ya Utalii unaotekelezwa na Kampuni ya Penny Royal wa Zanzibar Amber Resort wenye thamani ya Dola za Kimarekani Bilioni 1.6 wa ujenzi wa nyumba za wageni 1,900, viwanja vya michezo, uwanja wa ndege utatoa ajira kubwa kwa Vijana.

Mapema akitoa taarifa ya matembezi hayo Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM Tanzania Ndugu Shaka Hamdu Shaka  alisema Vijana wengi nchini huingia katika majaribu ya kudanganywa  historia ya Zanzibar  na kupelelekea kukejeli Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964.

Nd. Shaka alisema Mapinduzi ya Zanzibar  yametandikwa kwa  zulia la Umoja, Upendo na mshikamano chini ya majemadari waliofanya mapinduzi hayo ambao wanastahiki kuendelea kuenziwa na wananchi na Vijana wa kizazi cha sasa.

Alisema vilivyokuwa vikifanywa na watawala wa visiwa vya Zanzibar vilisababisha  vitendo vya unyanyasaji, uonevu na madhila yaliyochangia kuwakosesha haki zao za msingi wakwezi na wakulima wa Visiwa hivyi yakiwemo masuala muhimu ya huduma za msingi kama afya, elimu na umiliki wa ardhi.

Akitoa salamu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania anyesimamia Mazingira na Muungano Mh. Januari Yussuf  Makamba alisema Mapinduzi ya Zanzibar ni kielelezo tosha cha kujitambua kwa waafrika wa Visiwa vya Zanzibar.

Mh. Januari alisema Wakombozi wa Mapinduzi ya Visiwa vya Zanzibar wameacha urithi mkubwa kwa vijana wa Kizazi kipya unayostahiki kulindwa na kuendelezwa kwa faida na maslahi ya Wananchi wake.

Alisema njia pekee na sahihi ya kuendelea  kuimarika kwa Muungano wa Tanganyika  na Zanzibar  ni kudumisha Mapinduzi ya Zanzibar kupitia njia ya kuipatia ushindi CCM katika chaguzi zote zinazoendelea kufanyika hapa Nchini.

Matembezi ya Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi { UVCCM } kuadhimisha miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar  yaliyoshirikisha Vijana 400 yameanza juzi katika Kijiji cha Donge Mkoa wa Kaskazini Unguja na kumalizikia Afisi Kuu ya CCM  Kisiwandui.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.