Chumba cha chini ya bahari Pemba, chatimiza malengo la
Mapinduzi
Na Haji Nassor, Pemba
‘’JAMANI hicho chumba kinkaa vipi….!!!!….. lakini kiko kweli
au ni wazungu tu wanchomoka’’
‘’Tuseme kiko kweli,
haya wapita vipi………mambo makubwa…ivyo chumba kikae chini ya bahari kisha puunzi
wavuta vipi……?
‘’Mie sio kama si amini
vooo….!!!!……lakini wapita vipi hata
usirowe….. maana sote hapa twajua kuwa chini ya bahari kuna maji.
Kauli hizi zilisambaa
mithili ya mafuta ya taa, kwenye uwekaji wa jiwe la nanga la Chumba cha chini
ya bahari, kwenye hoteli ya Manta resort ilipo takriban kilomita 50 kutoka mji
wa Chake chake.
Manta resort ni hoteli
ya kitalii iliopo kijiji cha Mkangaale Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini
Pemba, lakini hili la chumba cha chini ya bahari, wenyeji na walioshuhudia
awali hawakuamini, je wewe unae soma makala hii vipi? nifuate.
Masuali mengi na mazito,
wananchi kadhaa waliiohudhuria hapo, walikua wakiuliza na hakukua na hata mmoja
aliekuwa akitoa jawabu, likiwadhaniwa kua ni la kweli.
Suali kubwa ambalo
lilitawala kwenye sakafu za vyumba vya akili vya watu, lilikuwa je unavutaje
pumzi kwenye chumba hicho……!!!!…?
Wapo waliodiriki kusema,
kuwa tokea milango ya biashara huria, iliotokana na Mapinduzi matukufu ya mwaka
1964, sasa kila kitu kinawezekana na kila jambo la maendeleo litwasilisi
Zanzibar.
Kwa siku ya uzinduzi wa
chumba hicho, wakati wa kufika kwa mgeni rasmi matarajiwa wa kuweka jiwe la
nanga la chumba hicho (under water room) ambae ni Makamu wa Pili wa rais
Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alifika.
Awali kulitanguliwa na
hutuba yake, kwenye shamra shamra za kusherehekea miaka 49 ya Mapinduzi ya
Zanzibar kwa wakti huo, laki wengi wao hawakuwa na hamu ya hutuba, bali ni
kutaka kujua chumba hicho cha kitalii kikoje.
Masuali haya yakaanza
kujibiwa na wakati huo aliekuwa Waziri wa Habari Utamaduni Utalii na Michezo
Said Ali Mbaruok, baada ya kudokoa kidogo, juu ya kuwepo kwa chumba hicho
ambacho kutoka kwenye fukwe ni kama mita 300, sawa na viwanja vitatu vya mpira
wa miguu.
‘’Ngudu wananchi, wakati
huu tukisherehekea miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar, sasa sekta ya utalii
inacho cha kujivunia na kutembea kifua mbele’’,alianza hivyo.
‘’Maana muda mfupi ujao
tutawamalizia kiu yenu ya kutaka kujua juu ya chumba hicho cha chini ya bahari
na hili ni ishara ya kupevuka na kutanuka kwa sekta ya utalii’’,alieleza Waziri
huku akitabasamu.
‘’Mapinduziii…!!!!…..daimaaa…jamani leo tunafuraha..tena
Mapinduziii…. daimaa akaitikiwa huku wananchi wakiwa makini kweli na kuvutiwa
na chumba cha chini ya bahari ambacho mtu anaweza kulala.
Wakati huu
tukisherehekea miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar, kwa wananchi wa Zanzibar na
hasa walioko Pemba, ni jambo la kujivunia kwa Serikali kupitia Wizara ya Habari,
hasa sekta ya utalii maana mradi huo ni mwanzo kwa baraza la Afrika.
Miaka hii 53 ya
Mapinduzi Zanzibar chumba hicho, kimeshatimiza miaka mitatu, kikiendelea kuwepo
chini ya bahari.
Chumba hicho kilicho
kwenye bahari, ni chamba cha kwanza duniani, lakini ni cha pili, baada ya kile
kilichoko nchini Sweden lakini kikiwa kwenye ziwa la maji baridi.
Hapa sasa ndio unapoona
umuhimu wa kuyalinda na kuyaenzi Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, ambayo
leo hii kila kona na chochoro ya visiwa vya Unguja na Pemba, neema yake
imeshafika.
“Leo ndugu wananchi
tumeshajikomboa leo, na kila mmoja wetu nitahakikisha atakaa na kuishi kwa
mazingira bora, na sasa hakuna tena kutawaliwa’’,alisema kwenye moja ya hutuba
yake rais wa kwanza wa Zanzibar marehemu Abeid Amani Karume.
Sasa hapa, ndio unapoona
umuhimu na faida ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, ambayo yaliwakombowa
wazanzibar na viongozi kuitangaaza Zanzibar kiutalii, na leo hii tukiadhimisha
miaka 53, Kisiwa cha Pemba chang’ara kwa kukua utalii.
Chumba hicho kwa njia
moja ama nyengine, kimeanza kufungua ukurasa mpya wa utalii wenye hadhi na wa
daraja la kwanza, hasa kwa vile chumba hicho ndio pekee kwa bara la Afrika.
Yote kwa yote, chumba
hicho (under water room), kila anefika kwenye fukwe ya hoteli ya Manta resort
Makangale, anashindwa kuamini mia juu ya mia, kwamba chumba hicho kinaweza
kulaliwa na watu bila ya kupoteza uhai.
Meneja wa hoteli hiyo
Matthew Saus kutoka Sweden, ambae anasema kuwa ujenzi wa chumba hicho
umegharimu kiasi cha dola laki tano za Marekani.
‘Mimi na mwenzangu
tulifika Pemba miaka kumi iliopita, na tukaanza harakati hizo za kujenga chumba
cha chini ya bahari, na taasisi kadhaa zilitukubalia, na leo hii tukiwa kwenye
sherehe za Mapinduzi ndio tumefikia hapa’’,alieleza.
Chumba hicho pamoja na
kuonekana cha maajabu makubwa, lakini wakati ukiwa umelala au unajipatia
chakula, basi hapo samaki wa aina zote, watakupita karibu sana na kutaka
kuwagusa huku ukizuiwa na viambaza maalum vya chumba hicho mitihili ya kioo
kigumu cha plastiki.
Kwa hili la chumba cha
chini haliishia tu kama sherehe lakini Mapinduzi ya Zanzibara ya mwaka 1964,
sasa yametinga duniani hasa kwenye sekta ya utalii, na kuziacha nchi zote za
bala la Afrika nyuma.
Chumba hicho, ambacho ni
cha kwanza duniani kuwepo kwenye maji ya bahari na ni cha pili baada ya kile
kilichoko nchini Sweden, kwenye Ziwa la maji baridi, ni ishara kwamba Zanzibar
imeshatanuka kiutalii wa daraja la kwanza ndani ya miaka hii 53.
‘’Leo tukiadhimisha
miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar, ni nani engetarajia kuwa tungefika hapa
kwenye sekta ya utalii, hii yote ni faida ya Mapinduzi yale yaliotukomboa chini
ya Jemedari wa taifa hili marehemu Abeid Amani Karume’’, alisema Balozi wakati
huo.
Kwa hakika chumba hichi
ambacho kinatumia umeme wa sola (jua), ili kuwapa mwangaza wa kutosha wapendwa
watakao kua chini ya maji ya bahari, leo hii tunayo kila sababu ya kutembea
kifua mbele, kwa kujivunia Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.
Wakati tukiadhimisha
miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, alieonekana na furaha
kubwa na alidakiza kuwa, muda mrefu Zanzibar ilikuwa ikiwakumbatia wawekezaji wasio
na uwezo (uchwara), na ambao huekeza kwa muda mfupi na kisha kutimua (kurudi
kwao).
‘’Zamani kabla ya
kuwajua baadhi ya wawekezaji, tulikua kila anae kuja tunampa eneo, wengine
wakisharejesha gharama zao tu hao…. wanarudi kwao na kutuachia majengo lakini
kwa hasa nasema heko’’, alifafanua Makamu huyo wa pili.
Wakati leo hii
tukiadhimisha miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar, Sekta ya utalii inafungua
ukurasa mpya wa utalii Kisiwani Pemba na Zanzibar kwa ujumla, na hasa kwa vile
mradi huo ni mwanzo ndani ya bara la Afrika.
‘’Hichi chumba, nasema
kimeanza kufungua milango kwa watalii wakubwa na wa juu na matajiri wakubwa
duniania, maana sasa akina Bilget wakija watapata sehemu ya kiutalii kwa mujibu
wa hadhi na fedha zao’’,alieleza Mkuu wa Kamisheni ya utalii Pemba Suleiman
Amour.
Japo kuwa gharama ya
kukaa kwa usiku mmoja, kwa mujibu wa Meneja wa wa hoteli ni shilingi milion tatu
laki mbili na sabiini (3,270,000), lakini kama sio gharama kubwa, naamini
watalii wengi ambao wangetarajiwa kwenda ingekuwa ni hawa wa watalii wa ndani.
Chumba hicho, ambacho
kwa juu ni mithili ya boya ambalo linaumbile la mlango wa nyumba ya kawaida
unaweza kuingia humo kwa aina ya kushuka ngazi hadi chini, ambapo kumetajawa
kuwa unapokua humo samaki unawaona kwa karibu.
Chumba hicho
kilicholetwa hapo kutoka nje ya nchi kuta moja baada ya nyengine, unapokuwa ndani
yake unauwezo wa kuona umbali wa mita100, huku samaki na bustani ya bahari
ikiwa ndio bustani yako.
Kwa vile muwekezaji huyo,
ana nia ya kuongeza idadi ya vyumba vya aina hiyo katika eneo hilo, iwapo hicho
cha mwanzo ambacho ni cha majaribio kitafanikiwa vizuri.
Sasa tukiwa
tunaadhimisha miaka 53 ya Mapinduzi ya mwaka 1964, kazi sasa ipo kwa Wizara ya
Habari, kuzidi kukitangaaza Kisiwa cha Pemba na Zanzibar kwa ujumla, juu ya
utalii kwa wote wa daraja la kwanza.
Lengo la Mapinduzi pia
ilikuwa ni kukuza pato la wananchi, hasa baada ya kujitawala na sasa kwa vile watalii wameshatukubali nasema
hapa ndio pakuanzia kwani mjenga nchi ni mwananchi.
Mkuu wa Mkoa wa
Kaskazini Pemba Omar Khamis, hakukosa la kusema juu ya chumba hicho, kutokana na kujaa na
furaha yeye akawasisitiza wananchi kuendelea kutoa ushirikiano na mwekezaji
huyo.
Asha Ali Omar wa
Makangale, anasema uwepo wa chumba hicho, sasa kunadhihirisha kufikiwa kwa
malengo ya kweli ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.
“Leo tukiadhimisha miaka
53 ya Mapinduzi Zanzibar, mimi binafsi nnafuraha maana, utalii umetanua mbawa,
na yale malengo ya jemedari wetu yamefikiwa’’,alifafanua.
Muhidini Makame Haji wa
Mchanga mdogo, anasema hakuna mwananchi wala kiongozi wa Zanzibar, ambae
hajanufaika na Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.
“Kila mmoja leo
akisherehekea miaka 53 ya Mapinduzi Zanzibar, hakuna ambae hajala keki ya
taifa, iwe kwenye utalii, afya, elimu au miundombinu ya barabara’’,alifafanua
Aliishauria serikali
kila atakaeyabeza Mapinduzi ya Zanzibar kwa njia moja ama nyengine, ni vyema
akashughulikiwa maana, atakuwa hapendi maendeleo.
Kwa hapa sasa ni dhahiri
kuwa, Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, na leo hii tukiwa katika shamra
shamra za maadhimisho ya miaka 53, ni ukweli kwamba Utalii wa hadhi ya juu
umeshaweka nanga Kisiwani Pemba.
No comments:
Post a Comment