Habari za Punde

Maadhimisho ya siku ya Malaria Duniani katika ukumbi wa Wizara ya Afya Mnazimmoja Mjini Zanzibar.

 Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya Zanzibar Dkt, Fadhil Mohd Abdalla akimkaribisha Naibu Waziri wa Afya Harusi Said Suleiman kuzungumza na waandishi wa habari katika maadhimisho ya siku ya Malaria Duniani katika ukumbi wa Wizara ya Afya Mnazimmoja Mjini Zanzibar.

 Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Bi. Harusi Said Suleiman akizunguza na waandishi wa habari katika maadhimisho ya siku ya Malaria Dunia katika ukumibi wa mikutano wa Wizara ya Afya Mnazimmoja Mjini Zanzibar.

Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Bi. Harusi Said Suleiman akizunguza na waandishi wa habari katika maadhimisho ya siku ya Malaria Dunia katika ukumibi wa mikutano wa Wizara ya Afya Mnazimmoja Mjini Zanzibar.

 Mwandishi wa habari wa ITV/Radio One Farouk Karim akiuliza swali katika maadhimisho hayo yaliyofanyika kwa mkutano wa waandishi wa habari katika Wizara ya Afya Mnazimmoja
Meneja Kitengo cha Kumaliza Malaria Zanzibar Mwinyi Issa Khamis akijibu maswali ya waandishi wa habari katika maadhimisho ya siku ya malaria yaliyoadhimishwa kwa mkutano wa waandishi wa habari Wizara ya Afya Zanzibar
Picha na Makame Mshenga-Maelezo Zanzibar


Na Ramadhani Ali/Maelezo 

Naibu Waziri wa Afya Harusi Said Suleiman amesema pamoja  na mafanikio makubwa katika kupambana na Malari Zanzibar, bado shehia tano zinaendelea kutoa wagonjwa wa maradhi hayo zaidi ya asilimia tano.

Akizungumza na waandishi wa habari katika maadhimisho ya siku ya Malaria Dunia katika ukumibi wa mikutano wa Wizara ya Afya Mnazimmoja, amezitaja shehia hizo kuwa ni Tumbatu Jongowe, Miwani, Micheweni, Chukwani na Kiwengwa.

Hata hivyo amesema maambukizi ya malaria katika maeneo hayo yanasababishwa na  wasafiri wanaoingia na kutoaka nje ya Zanzibar mara kwa mara ambapo mwaka jana asilimia 55 ya wagonjwa waliogundulika walikuwa na tabia hiyo.

Amesema takwimu za Malaria Zanzibar zinaonyesha mafanikio mazuri ambapo mtu mmoja kati ya watu mia moja hupata ugonjwa huo katika jamii isipokuwa shehia hizo tano.

Naibu Waziri wa Afya amewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari za kujikinga na Malaria ikiwemo kutumia vyandarua vilivyotiwa dawa na kusafisha mazingira kwa lengo la kuondosha mazalio ya mbu wanaoeneza maradhi hayo.

Ameongeza kuwa Serikali kwa upande wake mwaka jana iligawa vyandarua 705,000 bila malipo na kufanya zoezi la kupiga dawa nyumba za wananchi ya kukinga malaria bila ya kuangalia vyeo vya wamiliki wa nyumba hizo licha ya kukabiliana na changamo nyingi katika kazi hiyo.

Amesema  baadhi ya wananchi wamekuwa wakikataa kupigiwa dawa nyumba zao kwa madai kwamba zinawaletea athari za afya jambo ambalo halina ukweli kwani dawa hiyo ni salama kwa afya.

Amekumbusha kuwa Sheria ya Afya ya Jamii na Mazingira ya mwaka 2012 pamoja na mambo mengine inasisitiza juu ya udhibiti wa mbu na mazingira hivyo wananchi watakaokataa kupigiwa dawa sheria itawabana.

“Watu wanaokataa nyumba zao kupigiwa dawa ya kukinga malaria bila sababu za msingi zinazokubalika, sheria hii itawabana na hatua muafaka zitachukuliwa dhidi yao, ” alisisitiza Naibu Waziri.

Meneja Kitengo cha kumaliza malaria Mwinyi Khamis alisema Zanzibar imeweka mikakati ya kumaliza kabisa malaria ifikapo mwaka 2023 hivyo juhudi za jamii na Wizara ya Afya ni muhimu.

Amesema mwaka jana watu watano walibainika kufa kwa malaria Zanzibar wakiwemo watoto wawili wenye umri chini ya miaka mitano.

Mapema akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Kinga na Elimu ya Afya Dkt. Fadhil Mohd amewashauri wananchi wasikubali kula dawa ya malaraia bila kupimwa na kuthibitishwa kuwa wanayo malaria.

Kauli mbiu ya maadhimisho hayo mwaka huu inasema Malaria bado ipo Zanzibar, chukua tahadhari.



No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.