Habari za Punde

Rais Dk Shein: Michezo ina umuhimu mkubwa hasa kwa vijana   
STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar                                   25.04.2017
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa michezo ni sehemu ya maisha ya mwanaadamu na ina umuhimu mkubwa hasa kwa vijana na ndipo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeamua kwa makusudi kuiimarisha michezo na utamaduni maskulini.

Hayo aliyasema leo huko katika ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi  katika hafla ya kukabidhi vifaa vya michezo kwa skuli za Mikoa ya Unguja na Pemba vilivyotolewa na Mwakilishi wa Jimbo la Uzini, Mohammed Raza Dharamsi kwa ajili ya  mashindano maalum  ya  ‘UMOJA  CUP’ chini ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali.

Katika maelezo yake, Dk. Shein alisema kuwa Serikali inatambua kuwa katika maisha ya mwanaadamu yoyote michezo ina umuhimu,  kwani huleta mshikamano, kujuana, huburudisha na husaidia katika kujenga afya ya akili na kiwiliwili kwa vijana na watu wazima.

Dk. Shein alitumia fursa hiyo kueleza historia ya michezo  hapa nchini ikiwa ni pamoja na michezo katika skuli ambapo hata yeye mwenyewe binafsi alishiriki kikamilifu wakati huo huku akisisitiza kuwa michezo hudumisha umoja, udugu na kukuza ujasiri ambapo kwa hivi karibuni, michezo imekuwa ni chanzo kikubwa cha ajira.

Aliongeza kuwa pamoja na juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuendeleza michezo na utamaduni katika Skuli lakini katika miaka michache iliyopita hamasa ya michezo katika skuli ilionekana kushuka.

Hivyo, baada ya kuona hivyo alichukua juhudi za makusudi kutokana na ukereketwa wake wa michezo alichukua hatua kadhaa ikiwemo kuwaita wanamichezo mahiri wa zamani na wenye uzoefu mkubwa na kufanya nao mazungumzo kwa lengo la kurejesha na kuinua sekta ya michezo hapa nchini.

Alieleza kuwa miongoni mwa hatua za awali alizozichukua ni kuanzisha kwa Idara ya Michezo na Utamaduni katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, kuazisha mashindano ya riadha ya Wilaya, kugawa vifaa pamoja na mambo mengineyo.

Aidha, Dk. Shein alieleza kuwa katika kuendeleza na kuimarisha shughuli za michezo na  utamaduni katika skuli, Serikali itaendelea kutilia mkazo utekelezaji wa mipango ya kuimarisha michezo na sanaa ukiwemo Mpango wa Sport 55 na kupongeza hatua hiyo.

Akielez mipango ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha sekta ya michezo alisema kuwa Serikali ina mpango wa kujenga uwanja mpya utakaochukua watu 45,000 kwa wakati mmoja huko katika mji mpya wa Fumba sambamba na  imeshaamua kujenga kiwanja kimoja cha michezo katika kila Wilaya Unguja na Pemba na tayari kiwanja kilichopo katika Wilaya ya Kusini huko Kitogani kimeshakuwa tayari.

Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Mohammed Raza kwa upendo na uzalendo wake huo wa kuendelea kuunga mkono maendeleo ya sekta mbali mbali nchini ikiwemo sekta ya michezo na kupelekea kutoa vifaa hivyo kwa Wizara ya Elimu vikiwemo jezi, mipira, viatu, soksi, kikombe, medali za dhahabu na fedha, shinguard na vifaa vyenginevyo.

Pia, alitoa pongezi kwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa kuendelza sekta hiyo huku akitoa wito kwa Wizara hiyo  kuangalia uwezekano wa kuanzisha  mashindano katika skuli za msingi na Sekondari hasa mashindano kwa kutumia  ‘Inter houses’.

Nae Waziri wa Elimu an Mafunzo ya Amali Riziki Pembe Juma alimpongeza  Rais Dk. Shein kwa kuanzisha Idara ya Michezo na Utamaduni katika Wizara hiyo hatua ambayo imepelekea kuhamasika kwa michezo na kuaza kwa vuguvugu la michezo kama ilivyokuw kwa siku za nyuma.

Aidha, alitumia fursa hiyo kumpongeza na kumshukuru Mwakilishi wa Jimbo la Uzini, Mohammed Raza kwa hatua yake hiyo ya kuonesha mashirikiano makubwa kwa Serikali pamoja na Wizara hiyo ya Elimu na kumsifu kuwa ni kionozi anaetekeleza ahadi zake kwa vitendo.

Nae Mohammed Raza alimuhakikishia Rais Dk. Shein kuwa ataendelea kuiunga mkono Serikali katika kuendeleza sekta mbali mbali za maendeleo kwa kutoa misaada yake na kueleza kuwa ahadi zake zote alizoziahidi atazitekeleza.

Aliongeza kuwa juhudi hizo anazozichukua ni katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ambayo imesisitiza kuimarishwa kwa michezo, hivyo akiwa kiongozi na mkerekwetwa katika sekta hiyo ni vyema kuiendeleza na kuiimarisha sekta hiyo hapa nchini.

Pia, aliwaeleza wanafunzi ambao ndio walengwa wa vifaa hivyo kuwa mbali ya kucheza michezo mbali mbali katika skuli zao pia, ni vyema wakajua historia yao sambamba na kutambua mafanikio yaliopatikana kutokana na Mapinduzi ya Januari 12, 1964.

Sambamba na hayo, Raza aliahidi kutoa vifaa kwa ajili ya mashindano ya netiball kwa skuli za Unguja na Pemba huku akisisitiza ahadi yake ya kuzihudumia timu mbili za  Mkoa wa Kusini na Kaskazini Pemba zitakazokuja katika mashindano hayo hapa Unguja ambapo gharama zote za vifaa pamoja na huduma hiyo zitafikia milioni 25.

Mapema Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Khadija Bakari alisema kuwa Wizara imeelekeza nguvu zake katika usimamizi na utekelezaji thabiti wa shughuli zote za elimu zikiwemo utekelezaji wa Mpango wa ‘Sport 55’ unaolenga kuimarisha michezo katika skuli.

Aidha, aliongeza kuwa mikakati maalumu imeandaliwa na itatekelezwa kuanzia ngazi za skuli katika kurejesha shughuli zinzowajenga wanafunzi kuwa wakakamavu, wenye nidhamu na maadili mema, wanaofahamu mila, silka na desturi njema za Zanzibar.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.