STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 1.05.2017
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea na
utaratibu wake wa kuzilinda haki zote za wafanyakazi na kuimarisha maslahi yao hatua kwa hatua ili
waweze kumudu hali ya maisha pamoja na kuongeza ufanisi katika uzalishaji na
utoaji wa huduma kwenye sektka mbali mbali.
Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa aliyasema hayo
leo huko katika viwanja vya Mpira Mahonda, Mkoa wa Kaskazini Unguja katika
kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani, Mei Mosi ambayo kilele
chake hufanyika kila tarehe 01. Mei ya kila mwaka duniani kote.
Katika hotuba yake
aliyoitoa katika kilele cha maadhimisho hayo, Dk. Shein alisema kuwa kutokana
na kujali kazi na kuufahamu umuhimu wa wafanyakazi pamoja na kuufahamu wajibu
wake akiwa Rais wa Zanzibar amechukua hatua ya kupandisha mishahara na posho
mbali mbali kadri hali ya uchumi na ukuaji wa mapato inavyoruhusu.
Sherehe hizo ambazo
viongozi mbali mbali wa vyama vya siasa, Sekta binafsi na Serikali walihudhuria
akiwemo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd, Dk. Shein
aliongeza kuwa katika nyakati mbali mbali za uongozi wake katika kipindi cha
kwanza cha uongozi wake alipandisha mishahara mara tatu, mwaka 2011, 2013 na
mwaka 2015.
Aidha, alisema kuwa wakati
wa Kampeni za Uchaguzi wa mwaka 2015, aliahidi tena kuwea Serikali
atakayoiongoza katika kipindi cha pili mwaka 2015 na 2020 itaongeza kima cha
chini cha mshahara kwa sekta ya Umma kwa aslimia 100 kutoka TZS. 150,000
hadi TZS 300,000.
Kwa maelezo yake aliahidi
kuwa mabadiliko hayo ya mshahara yataanza mwishoni mwa mwezi wa April, 2017 na
kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumuwezesha pamoja na Serikali yake kwa kutekeleza
ahadi hiyo ambapo kuanzia mwezi uliopita wafanyakazi wote wa Sekta ya Umma
wameanza kufaidika na nyongeza hiyo ya mishahara.
Aliongeza kuwa ongezeko
hilo limetekelezwa kwa wafanyakazi na maafisa wa ngazi mbali mbali kwa viwango
tofauti vilivyowekwa na Taasisi zinazohusika kulingana na kwiango cha mshahara
anachokipata mfanyakazi.
Sambamba na hayo, Dk.
Shein pia, aliahidi kuwa Serikali itazishughulikia changamoto chache kama zitakuwepo kwa baadhi ya wafanyakazi zilizojitokeza
kulingana na utaratibu uliowekwa na kuwahakikishia wafanyakazi kuwa zitapatiwa
ufumbuzi wa haraka.
Pia, Dk. Shein aligusia
kupunguzwa kwa kwiango cha kodi ya mapato katika mishahara kutoka asilimia 13
hadi 9 kuanzia mwaka wa fedha 2016/2017, hatua hizo zote zimechukuliwa kwa
lengo la kuimarisha ustawi wa wafanyakazi na kuongeza ufanisi katika kazi.
Aisha, Dk. Shein alieleza
kuwa kwa wafanyakazi wanaowadharau wananchi wanapokweknda kupata huduma,
wanaowapuza, wanaowanyanayasa na wanaodai chochote ili wasaidie kutoa huduma
katika kipindi hiki Serikali itaongeza kasi na itaanza kuwachukulia hatua
Wakurugenzi wao, Maafisa Wadhamini wao na Makatibu Wakuu wao.
Na wale wote wenye tatbia
ya kutoroka kazini, kuchelewa kazini, wasiojali Kanuni zilizopo za Utumishi wa
Umma, wababaishaji na wanaojifanya hawajali na wababe, Serikali haitowavumilia
tena na watawajibishwa wao na kama hapana budi pamoja na viongozi wao wote
wataondoshwa kazini.
Alisisitiza kuwa uwezo wa
kuongeza mishahara unatokana na ongezeko la mapato na ukuaji wa uchumi, mambo
ambayo ni matokeo ya juhudi katika utendaji kwani mshahara ni ujira wa kazi na
mapato yanatoongezeka kwa juhudi katika kazini.
Akizingumzia suala la
mishahara hewa kutokana na ripoti aliyopelekewa hivi aribuni, Dk. Shein alisema
kuwa hapana atakae samehewa kwa atakebanika kufanya kosa na hapana atakaeonewa
au kudhulumiwa ambaye hajafanya kosa.
Pia, Dk. Shein alitoa wito
kwa wafanyabiashara na watoaji huduma ambali mbali, kuacha mtindo wa kuongeza
bei za bidhaa na huduma bila ya sababu za msingi kwani matokeo yake na wao
wanaweza kuathirika na wasije wakawalaumu wananchi na Serikali yao.
Kwa upande wa wafanyakazi
katika sekta binabsi, Dk. Shein aliwajuulisha kuwa taratibu za kisheria zinaendelea
ili kutangaza na kulipwa kwa kima kipya cha mishahara katika sekta hiyo.
Bila ya kwuasahau
wafanyakazi wa majumbani, Dk. Shein alitoa nasaha zake kwa waajiri wa
wafanayakzi hao kujenga utamaduni wa kuwathamini, kuwatambua rasmi, kuwapatia
stahikli zao, kuwawekea mazingira ya kazi yanayostahiki na wao wapate fursa ya
kujadiliana na waajiri wao kama zilivyo kada nyengine.
Nae Waziri wa Kazi,
Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto Maudline Cyrus Castico alieleza
juhudi zinazoendelea katika kulitafutia ufumbuzi suala la kima kipya cha
mishahara kwa sekta binafsi huku akitumia fursa hiyo kupongeza Rais Dk. Shein
kwa juhudi zake za kuwaenzi wafanyakazi.
Mapema Mwakilishi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO),
Albert Okelo akitoa salamu za Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo Tanzania, alitoa pongezi kwa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar kwa kuwajali wafanyakazi na kuwasamini pamoja na juhudi za Serikali za
kuanzisha Pensheni Jamii kwa wazee.
Katibu Mkuu Vyama Huru vya
Wafanyakazi Zanzibar, Khamis Mwinyi Mohammed alitoa pongezi kwa Dk. Shein kwa
kutekeleza ahadi yake ya kupandisha mishahara kwa kima cha chini sambamba na
kupongeza Serikali chini ya uongozi wake kwa kudumisha amani na utulivu na
kueleza baadhi ya mafanikio yaliopatikana katika uongozi wa Dk. Shein.
Mapema Dk. Shein alipokea
maandamano ya wafanyakazi wa Sekta ya Umma pamoja na Sekta binafsi na kabla ya
hotuba yake alitoa zawadi kwa wafanyakazi bora 16 kwa niaba ya wenzao 100
kutoka sekta ya Umma.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address:
2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment