Habari za Punde

Mkutano wa Baraza la Vijana Zanzibar

Na Ali Issa –Maelezo Zanzibar.

Serikali imetoa fursa kwa vijana  kutengeneza sheria yao ili kuwawezesha kutekeleza shughuli zao katika Nyanja mbalimbali za kimaisha.

Hayo yamesemwa huko katika ukumbi wa wasanii Rahaleo na Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Ayuob Muhamed Mahmoud wakati akifungua mkutano wa dharura wa baraza la Vijana Taifa uliojadili kanuni, malengo na mpango mkakati wa baraza hilo.

Amesema mpango huo ni fursa pekee kwa vijana iwapo wataitumia vizuri hivyo amewataka kuwa makini wanapoijadili na kupitia vifungu vya kanuni na miongozo mengine ya baraza hilo.

Amewashauri wakati wa kuijadili taarifa hiyo kuhakikisha wanaingiza vipengele muhimu ambavyo wanahitajiwa kutekelezewa na Serikali.

“Jengeni mipango iliyobora kwa ajili yenu vijana na Serikali ipo tayari kuhakikisha mipango hiyo inatekelezwa,”alisema Ayuob.

Aidha aliwataka vijana wawe mstari wa mbele kwa kufanya kazi kwa kujitolea pamoja na kuthamini juhudi za viongozi na uhuru wa taifa lao

Mkuu huyo wa Mkoa aliishauri Wizara ya Kazi,Uwezeshaji Wananchi ,Vijana Wanawake na Watoto kulifungua Baraza hilo rasmi kutambulika kisheria kwani linajumuisha vijana wote wa Zanzibar kupitia ngazi za shehia, wilaya na mikoa.

Nae katibu Mtendaji wa Baraza hilo Khamis Faraji Abdalla alisema lengo la mkutano huo ni kupitia vifungu vya kanuni, mpango mkakati na vipengele vyengine vya kumuelekeza kijana umuhimu wake kitaifa katika harakati zake za kila siku.

Hata hivyo alisema mpango huo unavipengele vingi vya utekelezaji kwa vijana na ameahidi wataipitia ikiwa ni pamoja na kazi za kamati, nembo ya baraza,utaratibu wa nidhamu kwa vijana, mfumo wa mawasiliano kutoka ngazi ya shehia hadi taifa, dua na kiapo cha baraza.

Katibu huyo alimuhakikisha Mkuu wa wa Mkoa kwamba  watayafuata na kuyafanyia kazi maelekezo yake kama alivyoagiza.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.