Habari za Punde

Mwamko Mdogo wa Kielimu Walionao Wananchi Wengi Ndio Unaopelekea Vitendo vya Udhalilishaji Vinavyoendelea. - IGP Sirro.

Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania {IGP} Simon Sirro Kushoto akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofika Ofisini kwake Vuga kujitambulisha Rasmi baada ya kuteuliwa hivi karibuni na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli kushika wadhifa huo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akifafanua  tatizo la Udhalilishaji dhidi ya Wanawake na Watoto linaloonekana kuathiri Jamii wakati akizungumza na  Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania {IGP} Simon Sirro.(Picha na – OMPR – ZNZ.)
Na. Othman Khamis OMPR.
Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania {IGP} Simon Sirro amesema mwamko mdogo wa kielimu walionao Wananchi wengi ndio unaopelekea ongezeko kubwa la vitendo vya udhalilishaji vinavyoendelea kushuhudiwa kufanyika kila kukicha katika maeneo mbali mbali hapa Nchini .

Alisema  baadhi ya Watu wakorofi  wamekuwa wakitumia udhaifu huo kwa kuendeleza vitendo viovu dhidi ya Wanawake na Watoto  ambao huathirika kiakili na kimwili na kuwapa wakati mgumu wa kuendelea na maisha yao ya kawaida ndani ya Jamii inayowazunguuka.

IGP Simon Sirro alieleza hayo wakati alipofika Ofisini kwa  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Vuga Mjini Zanzibar kujitambulisha rasmi baada ya kuteuliwa  hivi karibuni na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli kushika wadhifa huo.

Kamanda Sirro alimueleza Makamu wa Pili wa Rais  wa Zanzibar kwamba  katika kukabiliana na vitendo hivyo viovu vinavyoonekana kuleta fadhaa inalazimika kwa Jamii wakati huu kubadilika kwa kuwa tayari kutoa ushahidi pale wanaposhuhudia vitendo hivyo.

Alisema kesi yoyote inategemea kuendeshwa katika misingi na taratibu za Kisheria kwa kuzingatiwa ushahidi unaotolewa  na mashahidi ili haki inapotolewa iende sambamba na stahiki ya pande zote husika.

Kamanda sirro aliitahadharisha Jamii inayopenda kulalamika zaidi kwamba nje ya kukosekana kwa ushahidi wa tuhuma zozote zinazowasilishwa Polisi na hatimae kwenye Ofisi ya Muendesha Mashtaka maana yake hakuna kesi itakayoendelea hata kama kuna mtu aliyedhulumiwa.

Alisema zipo kesi nyingi za udhalilishaji hasa zile za utelekezaji wa familia zinazofanywa na baadhi ya Wanaume zaidi upande wa Tanzania Bara zinazofikia zaidi ya asilimia 80%  na kusababisha familia husika kukosa matunzo jambo ambalo huchangia ongezeko la Watoto wa Mitaani wanaokosa malezi ya Familia.

“Tunafarajika kuona kwamba  ipo Sheria ya adhabu dhidi ya Watu wanaotupa na kutelekeza Familia zao kwa upande wa Tanzania Bara ambayo imekuwa ikitumika na kupunguza matukio kama hayo ”. Alisema Kamnada  Simon Sirro.

Akizungumzia hali ya Amani Nchini  Tanzania Mkuu huyo wa  Jeshi la Polisi Tanzania  alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Nchi bado iko shwari licha ya matukio ya hapa na pale yanayoshuhudiwa katika Maeneo ya Rufiji.

IGP  Sirro kupitia  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaomba  Wananchi waendelee kushirikiana na vikosi vya ulinzi katika kutoa  Taarifa za matukio ya uhalifu, Ujambazi  na Uhujumu Uchumi kwenye maeneo yao ili vyombo vya Ulinzi vitumie maarifa yake katika kuwasaka wahalifu hao.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alilishauri Jeshi la Polisi kuongeza nguvu katika ujenzi wa Makaazi ya Askari wake ili kuondosha mfumo uliopo hivi sasa wa Askari wengi kuishi Mitaani pamoja na Raia.

Balozi Seif alisema kitendo hicho cha Askariu kuishi Mitaani kinaleta muhali sana kwao na kushindwa kuchukuwa hatua za kisheria dhidi ya Jamaa na marafiki pale wanapofanya makosa na baadae kuwasilishwa kwao.

Akigusia janga la Dawa za Kulevya Nchini Balozi Seif  alimueleza Kamanda Sirro kwamba tatizo hilo Bado linaonekana kuleta madhara  hasa kwa upande wa Visiwa vya Zanzibar kutokana na Vijana wengi kuonekana watumiaji wakubwa wa Dawa hizo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.