BARAZA la
Mawaziri kutoka Umoja wa Nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika la Udhibiti
Utakasishaji Fedha Haramu (The East and Southern Africa Anti Money Laundering
Group-ESAAMLG), linatarajia kukutana
Tanzania tarehe 08 Septemba 2017 mjini
Zanzibar.
Taarifa
iliyotolewa na kitengo cha mawasiliano serikalini, Wizara ya Fedha na Mipango,
imesema mkutano huo umepangwa kufanyika katika hoteli ya
Zanzibar Beach Resort
Mazizini nje kidogo ya manispaa ya Zanzibar.
Kwa mujibu
wa taarifa hiyo, mkutano huo utatanguliwa na ule wa maafisa waandamizi
(Makatibu wakuu), utakaoanza Septemba 2 hadi 6, mwaka huu katika ukumbi wa
hoteli hiyo.
Katika
mkutano huo, pamoja na masuala mbalimbali yatakayojadiliwa, Serikali ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, itatumia fursa hiyo kuwasilisha taarifa ya hatua
iliyofikia katika utekelezaji wa mpango wa chombo cha kimataifa
kinachoshughulikia udhibiti wa utakatishaji wa fedha haramu, “The Financial
Action Task Force (FATF) ulioasisiwa mwaka 2009.
Mpango huo
ulizitaka nchi wanachama kufanya tathmini ya utekelezaji wa maazimio
yaliyainishwa kwenye FATF, katika maeneo mbalimbali ya kisheria, kisera,
miongozo ya kitaasisi zikiwemo sekta za fedha na maeneo ya ushirikiano wa
kimataifa.
Lengo ni
kubaini jinsi nchi wanachama zilivyojipanga katika kudhibiti suala la
utakasishaji fedha haramu na ufadhili wa ugaidi (Anti-money Laundering and
Combating the Financing of Terrorism).
Katika
mkutano huo, mbinu na mikakati mbalimbali itakayosaidia kudhibiti utakasishaji
fedha haramu na ufadhili wa ugaidi zitajadiliwa, hatua ambayo italeta matokeo
chanya na kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi na kufikia maendeleo tarajiwa
katika nchi wanachama ikiwemo Tanzania.
Tanzania ni
miongoni mwa nchi waanzilishi wa umoja huo ulioasisiwa jijini Arusha mwaka
1999. Nchi nyengine ni Uganda, Kenya, Mauritius, Namibia, Seychelles na
Swaziland ambazo zilisaini makubaliano (Memorandum of Understanding-MOU).
Hatua ambayo
ilipelekea Makao Makuu ya Sekretariati ya Umoja huo wenye nchi wanachama 18,
ambazo ni Angola, Botswana, Ethiopia, Kenya, Lesotho, Madagascar, Malawi,
Mauritius, Msumbiji, Namibia, Rwanda,
Afrika Kusini, Swaziland, Seychells,
Tanzania, Uganda, Zambia na Zimbabwe kuwa jijini Dar es Salaam Tanzania.
Kwa sasa
Tanzania ndio Mwenyekiti wa umoja huo kwa kipindi cha mwaka mmoja, baada ya
kupokea uenyekiti kutoka Jamhuri ya Zimbabwe iliyomaliza muda wake mwezi huu wa
Agosti 2017 ambapo Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango
(MB), ambae pia ni Mwenyekiti (President of the Council) atakaeongoza mkutano
huo.
IMETOLEWA
NA:
KITENGO CHA
MAWASILIANO SERIKALINI
WIZARA YA
FEDHA NA MIPANGO-TANZANIA
29 AGOSTI
2017
No comments:
Post a Comment