Habari za Punde

Umuhimu wa zao la karafuu wazidi kuongezeka

Na Kautahr Ishaka, Maelezo, Pemba


Umaarufu na umuhimu wa zao la karafuu unazidi kuongezeka Zanzibar,  siku hadi siku, hasa katika awamu hii ya saba, kutokana na jitihada maalum zinazochukuliwa na Mhe. Rais wa Zanzibar  Dkt. Ali Mohamed Shein,na viongozi mbali mbali, wakiwemo Mawaziri, Makatibu wakuu, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa wilaya  pamoja na Wafanyakazi wote wa ZSTC wakiongozwa na Mkurugenzi Mwendeshaji.

  Serikali kwa kuhakikisha kuwa lengo hilo la kuwanufaisha wakulima  na Wadau wa zao la karafuu  linatekelezwa vyema, ikaamua kuwa miongoni mwa kazi za Mfuko wa Maendeleo ya Karafuu ziwe ni hizi zifuatazo, ambazo zitamsaidia mkulima na mdau wa zao la karafuu moja kwa moja.

 Kufanya usajili wa Wakulima wanaomiliki na wanaokodi mashamba ya mikarafuu ili kurahisisha shughuli za utoaji wa huduma, Kusaidia miradi ya maendeleo ya miundo mbinu katika maeneo yenye mashamba ya mikarafuu, kutoa mikopo ya fedha taslimu kwa Wakulima na Wanaokodi karafuu kwa hatua za awali za uchumaji wa karafuu na ununuzi wa majamvi kwa kuanikia kuwakatia bima wachumaji wa karafuu watakaopata ajali wakati wakichuma karafuu.

Mkurugenzi Fedha wa ZSTC, Bwana   Ismail Omar Bai, akifafanua Msimu wa  mwaka 2016/17 alisema , ulikuwa ni msimu  mdogo ukilinganisha na msimu uliopita (2015/16), manunuzi ya karafuu yalianza mapema katika  mwezi wa Julai na yaliendelea vizuri  katika kipindi chote cha manunuzi.

Makisio ya vuno la mwaka mzima ilikuwa ni tani 2,810 ambapo manunuzi makubwa yalitarajiwa kupatikana katika kipindi cha  miezi ya Oktoba hadi Novemba 2016.

Alisema Shirika liliendelea  kufanya kazi kwa mashirikiano na Wadau wote katika harakati za kuendeleza juhudi za Serikali katika kuhakikisha kwamba Sekta ya karafuu  inakuwa endelevu.

Aidha, kutokana na mashirikiano hayo kutoka kwa Wadau mbali mbali Shirika liliendelea kufanya kazi kwa mafanikio makubwa ambapo Shirika kwa mwaka huu hadi kufikia tarehe 30/04/2017 limeshanunua karafuu jumla ya tani 2,266.2 zenye thamani ya Tzs 31.8 bilioni Kutoka kwa Wakulima Unguja na Pemba (Unguja tani 132.5 kwa thamani ya Tzs1.8 bilioni na Pemba tani 2,133.7 kwa thamani ya 29.9 bilioni.

Manunuzi hayo  ni sawa na asilimia  themanini na moja (81%) ya makadirio  yaliyowekwa kwa mwaka 2016/2017, makadirio kwa mwaka ilikuwa ni kununua tani 2,810 za Karafuu, ambapo Unguja tani 160.0 na Pemba 2,650.0.

Afisa Mdhamini wa ZSTC  Pemba, Abdalla Ali Usi alisema Shirika hilo la biashara limeonekana wazi kuwa limekuwa likifanya kazi zake kwa mafanikio makubwa hivyo haliko nyuma katika kutoa huduma za kijamii kila pale inapopata nafasi ikiwa linatoa misaada katika sekta ya Afya,Elimu na shughuli za kijamii,

ZSTC imefanikiwa kusaidia kutoa msaada wa madawati kwa skuli za Kisiwa Panza,Uweleni na Mjimbini huku ikitoa gari za kupakilia wagonjwa Mkoa wa Kusini Pemba pamoja na vituo vyake vyote kutumika katika shughuli kama maziko,maulidi na harusi vijijini.

Tujitahidi kupanda miche ya mikarafuu kwa wingi  na kuihudumia sifa na ubora unahitaji  kuimarishwa kwa kutumika vigezo vyote kuanzia kuchuma, kuzichambua na kuanika  kwa kutumia vifaa vinavyopaswa kutumika kwa kazi hizo.

Serikali ione ziada ya thamani ya wakulima wetu kwani “WAKULIMA WETU NDIO HAZINA YETU” bila ya mkulima wa karafuu hakuna mashamba ya mikarafuu na wala ZSTC hawataweza kununua karafuu hivyo, nguvu za makusudi za kumkomboa mkulima wa karafuu ziendelee kuwa endelevu ili kuwaneemesha wakulima wetu, jamii yetu na Taifa kwa ujumla.

Tuendeleze jitihada za Serikali, tuendeleze mshikamano uliopo wa kupiga vita  usafirishaji wa karafuu na miti ya mikarafuu  kwa magendo kwani kufanya hivyo ni kuua uchumi wa Nchi.

Zao hili ni lenye faida kubwa kwetu, tulitunze kwa kuhakikisha uvunaji hauleti taathira katika miti na kusababisha miti kupunguza uzazi, tujitahidi katika kuhakikisha  uzalishaji unafuata vigezo vyote vya  ubora ili  sifa ya karafuu za Zanzibar ibaki ulimwenguni kote.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.