Habari za Punde

Wadau wa Sheria watakiwa kuusimamia vyema mswaada wa utowaji huduma za sheria nchini

NA/ SALAMA NASSOR--- PEMBA.

OFISA Mdhamini Wizara ya nchi ofisi ya Rais,katiba,Sheria utumishi wa Umma na Utawala bora Pemba, Masoud Ali Mohamed, amewataka wadau wa Sheria nchini kuusimamia mswaada wa sheria juu ya utowaji wa huduma za sheria ili iweze kuwafikia jamii.

Kauli hiyo ameitowa wakati alipokuwa akifunguwa mafunzo ya siku moja yaliofanyika katika ukumbi wa Nyaraka Chake Chake , ambapo  alisema jamii haina uwelewa mkubwa juu ya mswada huo hivyo aliwaomba wadau hao kushirikiana kwa pamoja kwa kutowa elimu ili iweze kufikia malengo yalio kusudiwa.

Alieleza taaluma hiyo iweniendelevu kwa    ajili kuendeleza Taifa na sio vyema kuiwacha njiani wakati wapo wengi wanaihitaji.

“Jamii wakipatiwa elimu juu mswada huo ulionzishwa basi kutaondokana na malalamiko pamoja na kukosa huduma zao wakati wanapokabiliwa na matatizo na wanakuwa wanakosa uwezo wa kujikwamuwa kutokana na hali zao kuwa ni duni”,alisema.

Akitowa maada katika mafunzo hayo, Saleh Said Mubaraka, alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwasaidia watu ambao hawana uwezo wa kulipia huduma za sheria hivyo Serikali imeamuwa kuwanzisha wadau wa sheria ili waweze kufanya kazi.

Aliwataka wadau kuusoma vizuri ili kutowa maelekezo katika mswaada huo kabla ya haujapitishwa na baraza la Wawakilishi ili wananchi uwafikie wakati muwafaka.

Alifafanuwa kwa kusema mswaada huo ni kuhakikisha kila mwananchi anapata haki zake za msingi kwa mujibu wa sheria.

“Ikiwa mswaada huu utapita wananchi watafaidika hususani kwa wale walengwa waliokusudiwa ambao wasiojiweza na kutaondokana na malalamiko yaliokuwa yanajitokeza wakati wanapotaka kupatiwa haki zao”,alisema.

Ofisa huyo, aliwataka wanasheria kuwa makini katika kazi zao na wasiwe wanaangalia upande mmoja kwani wao wanajukumu kubwa katika nchi kinyume na hivyo kutapelekea malalamiko yasiokuwa ya lazima.

Kwa upande wao washiriki katika mafunzo hayo, Ofisa Mipango  kutoka kituo cha huduma za sheria, Safia Saleh Sultan, alisema ameyapokea vyema mafunzo hayo kwani kwani Serikali imefanya juhudi kubwa kwani haujabaguwa mtu.
Aliitaka Wizara hiyo kutowa elimu kwenye vyombo vya habari kwani wakifanya hivyo watafaidika wananchi walio wengi hususani wa vijijini.
Naye Ofisa upelelezi Dawati la kijinsi na watoto, Hamad Faki Ali, alisema mswaada huo utapelekea kuleta maendeleo kwa jamii na pia watapata kutetea haki zao.
Alisema jamii haina elimu ya haki na kujuwa sheria na hupelekea kupata Changamoto nyingi, lakini mswaada huo ukipita watajuwa haki zao kwani umechanganya mambo mengi na haukuweka ubaguzi.
Hivyo aliomba kuweko mashirikiano ya pamoja kwa wadau wote , ili kuhakikisha muswada huo unaeleweka kwa Wananchi wote.

  


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.