Habari za Punde

DC: Waacheni Wanasheria Wafanye Kazi Zao

Na.Haji Nassor - Pemba.

MKUU wa wilaya ya Mkoani Hemed Suleiman Abdulla, amewataka viongozi mbali mbali, kuwaacha wanasheria kutekeleza wajibu wao, badala ya kuwaingilia kwenye majukumu yao, kwani kufanya hivyo  ni kudhoofisha utendaji wao wa kazi.

Alisema wanasheria wamekuwa wakitekeleza wajibu wao kama walivyo watendaji wengine, amboa hawapendi kuingiliwa utendaji wao, hivyo ni vyema na wao wakaachiwa kufanya majukumu yao waliopangiwa kwa mujibu wa sheria.

Mkuu huyo wa wilaya, ametoa tamko hilo, Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ZLSC tawi la Pemba, alipokuwa akifungua mafunzo ya siku mbili, juu ya haki za binadamu kwa makadhi, marakani na wazee wa mahakama na kusema wanasheria wanafanya kazi zao vyema.

Alisema wamekuwa wakitoa msaada mkubwa wa kisheria kwa wananchi, kabla ya kutaka kufungua mashauri yao mahakamani, hivyo iwapo watakuwa wanaingiliwa kwenye kazi zao, hawawezi kufikia malengo yao.

Alisema kama viongozi watatumia vibaya nafasi zao, na sasa kuamua kuwaingilia wanasheria wakati wanapotekeleza majukumu yao, ufanisi wa kazi kwao hauotokuwepo.

“Hivi tunayo oifisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka, Kituo cha Huduma za sheria na hata vyombo kama mahakama na Polisi, wamekuwa wakiwasaidia wananchi kisheria, lakini kama tukiwaingili sisi viongozi ufanisi hautokuwepo”,alifafanua.

Katika hatua nyengine Mkuu huyo wa wilaya ya Mkoani, amewataka wazee wa mahakama, makadhi na makarani kisiwani Pemba, kuendelea kufanya wajibu wao kwa kufuata sheria na kaununi zilivyo, hata kama kufanya hivyo, hakutowaridhisha watu wengine.

Mapema Mratibu wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar Fatma Khamis Hemed, amesema makadhi, makarani na wazee wa ,mahakama ni nguzo muhimu kwenye kuendesha kesi mbali mbali.

Hivyo alieleza ndio maana, Kituo kimeamua kuwapa mafunzo ya haki za binadamu kwa vile haki hizo ni wajibu wa kila mmoja kuzitunza za mwenzake ili na za kwake zitunzwe.

Akiwasilisha mada uwajibikaki na utendaji wa haki Mwanasheria Dhamana wa Afisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka Pemba, Ali Rajab Ali alisema kwenye kutekeleza majukumu ya umma, hakupaswi kwa mktoa uamuzi kuegemea upande mmoja.

“Nguzo za kutekeleza wajibu na haki, unaonekena kwenye maeneo matano, ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa majukumu, kufuatwa kwa mujibu wa sheria na kutoa huduma kwa kiwango kinachotakiwa”,alifafanua.

Wakichangia mada kadhaa washiriki wa mafunzo wameziomba mamlaka husika, kuhakikisha kwa wazee wa mahakama kuwa ofisi maalum ya kukaa kabla ya kuanza kwa uendeshaji wa kesi badala ya utaratibu wa sasa wa kuchanganyika na wanaosubiri huduma.

Mzee wa mahakama Chakechake Abdalla Nassor Mauli, alisema haipendezi kuona wanapofika mahakamani kuchanganyika na mashahidi, watuhumiwa na watu wengine wanaotaka huduma Makamani.

Aidha Kadhi ya mahakama ya rufaa Daud Khamis Juma, alisema elimu ya utendaji kazi, inapaswa kuwepo kila baada ya muda, maana ukumbushaji hauna muda malum.

Akighairisha mafunzo hayo, Afisa Mipango wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ZLSC tawi la Pemba, Khalfan Amour Mohamed, alisema makadhi na makarani wanayonafasi kubwa ya kupatikana kwa haki mahakamani.

Katika mafunzo ya siku mbili mada kadhaa zilijadiliwa, ikiwa ni pamoja na changamoto na mtizamo wa jamii kwa mahakama za kadhi na wazee wa mabaraza, haki za binadamu, maadili ya makadhi na wazee wa mahakama pamoja na huduma kwa wateja.                    

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.