Habari za Punde

UJAMAA NA MUEMBELADU KUSUKUMANA KOMBE LA MTOANO

Na: Abubakar Khatib Kisandu, Zanzibar.

Wakongwe wa Soka Visiwani Zanzibar timu ya Ujamaa Sports Club inayoshiriki ligi daraja la Pili Taifa Unguja watakipiga na timu ya Muembeladu ambayo inacheza ligi daraja la Pili Wilaya ya Mjini kwenye Mashindano ya Kombe la Mtoano mchezo utakaopigwa Kesho Ijumaa saa 10:00 za jioni katika Uwanja wa Amaan.

Huo ni mchezo wa mwisho katika hatua ya 16 bora ambapo hapo inatafutwa timu moja itakayoungana na timu saba zitakazocheza hatua ya robo fainali kwenye Mashindano hayo yaloandaliwa na chama cha Soka Wilaya ya Mjini.

Timu 7 ambazo tayari zimeshatinga hatua ya robo fainali kufuatia kushinda michezo yao ya awali ni Polisi Bridge, Negro United, Hawai, Shaba, El hilal, Raskazone na Polisi.

Mashindano hayo yameshirikisha vilabu vya madaraja tofauti vikiwemo vya ligi kuu soka ya Zanzibar, Daraja la Kwanza Taifa, Daraja la Pili Taifa, Daraja la Pili Wilaya na Daraja la Tatu ambapo mchezo wa kwanza robo fainali utachezwa siku ya Jumatatu Septemba 11, 2017 kati ya SHABA kutoka Pemba dhidi ya Police Bridge mchezo utakaopigwa majira ya saa 10:00 za jioni katika uwanja wa Amaan.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.