Habari za Punde

HISA ZA MAENDELEO BANK ZAFANYA VIZURI SOKONI TANGU ZIZINDULIWE NA WAZIRI WA FEDHA

 Waziri wa Fedha na Mipango Mh. Dk. Philip Mpango akizungumza na wageni waalikwa katika hafla ya uzinduzi rasmi wa uuzaji hisa za Maendeleo Bank PLC uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Hisa za Maendeleo Bank zimeendelea kufanya vizuri  sokoni tangu kuzinduliwa kwa mauzo ya hisa hizo rasmi Septemba 18, tukio ambalo lilifanywa na Waziri wa Fedha na Mipango Mh. Dk. Philip Mpango.Watanzania wengi wameonekana wakiitikia wito wa kuwekeza katika soko la mitaji kwa kufika katika matawi ya Maendeleo Bank ya Luther House, Mwenge na  Karikakoo, matawi yote ya CRDB nchini, Uchumi Commercial Bank na Mawakala wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) walioidhinishwa kuuza hisa.Akizungumzia maendeleo ya ununuzi wa hisa hizi, Mkurugenzi Mtendaji wa Maendeleo Bank Bw. Ibrahim Mwangalaba alisema “Tumeingia wiki ya tatu sasa katika zoezi letu la uuzaji wa hisa, tumeona watanzania wengi wakijitokeza na kwa kweli sisi kama benki tuna matumaini makubwa  ya kufikia lengo ambalo tumekusudia”.Pia tunaendelea kuisaidia Serikali katika kutoa elimu ya uwekezaji katika masoko ya mitaji na faida zake kwa watanzania na nchi kwa ujumla. Waziri wa Fedha na Mipango Mh. Dk. Philip Mpango akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa uuzaji hisa za Maendeleo Bank PLC. Pamoja nae kutoka kushoto ni Askofu Ambele Mwaipopo, Askofu Mkuu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani Askofu Dk. Alex Malasusa, Mkurugenzi Mtendaji wa Maendeleo Bank Bw. Ibrahim Mwangalaba na Mwenyekiti wa Bodi ya Maendeleo Bank Bw. Amulike Ngeliama.
Mwitikio wa watanzania katika kununua hisa, kujitokeza kuuliza maswali ili kuelewa zaidi juu ya mambo haya ni suala la kujivunia kwetu kwani tunafanya mambo makubwa mawili kwa wakati mmoja,  moja ni kuuza hisa lakini la pili ni kusaidia juhudi za Serikali juu ya kutoa elimu ya namna gani watanzania wanaweza kuwekeza katika hisa” aliongeza Mwangalaba.
Uwekezaji katika hisa ni mfumo wa uwekezaji unaomuwezesha muwekezaji nafasi ya kumiliki kampuni na kupata gawiwo pale kampuni inapopata faida.  Pia hisa ni njia ya ukuzaji wa thamani ya fedha yako pale hisa zinapopanda.
Pia hisa zinaweza kutumika kama dhamana ya kujichukulia mkopo katika benki.
Mkurugenzi huyo amewasihi watanzania wengi zaidi kuchangamkia hisa za Maendeleo Bank ili waweze kuwa sehemu ya uchumi wao kwa kumiliki sehemu ya benki hiyo. Hisa za Maendeleo Bank zinaendelea kuuzwa hadi Novemba 3, 2017.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.