Habari za Punde

Maafisa wa Jumuiya ya Maradhi Yasioambukiza Zanzibar Watoa Taaluma Kwa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu Zanzibar.

Rais wa Mtandao wa wanafunzi wa Kimataifa Zanzibar Bakari Juma Bakari akitoa maelezo juu ya mhadhara wa wazi wa maradhi yasiyoambukiza (NCD) uliofanyika Chuo Kikuu cha Zanzibar (ZU) Kempasi ya Mpendae Mjini Zanzibar. Kulia ni afisa kutoka Jumuiya ya Maradhi yasiyo ambukiza Zanzibar Omar Abdalla Ali.
Afisa wa Jumuia ya maradhi yasiyoambukiza Omar Abdalla Ali akianzisha mhadhara wa wazi juu ya maradhi hayo ulioandaliwa na Mtandao wa wanafunzi wa Kimataifa Zanzibar katika Kempasi ya ZU Mpendae
Meneja wa Jumuiya ya Muungano wa Maradhi yasiyoambukiza Zanzibar Zuhura Saleh Amourakitoa takwimu ya maradhi ya kisukari duniani na hali ya maradhi hayo kwa Zanzibar katika mhadhara wa wazi ulioandaliwa na Mtandao wa wanafunzi wa Kimataifa wa Zanzibar katika kempasi ya ZU iliopo Mpendae.
 Baadhi ya wanafunzi walioshiriki mhadhara wa wazi wa maradhi yasiyoambukiza wakifuatilia mhadhara huo uliofanykika Kempasi ya ZU iliyopo Mpendae, Mjini Zanzibar.
Mmoja wa wanafunzi walioshiriki mhadhara wa wazi wa maradhi yasiyoambukiza katika kempasi ya ZU Mpendae Mohd Awesu akiuliza swali katika mhadhara huo.Picha na Makame Mshenga.

Na Ramadhani Ali – Maelezo.
Mwamko mkubwa wa kufanya mazoezi unaonekana sehemu nyingi za Zanzibar bado  haujasaidia sana kupunguza maradhi yasioambukiza na hatimae maradhi hayo yanaendelea kuwasumbua wananchi wengi.

Meneja wa kitengo cha maradhi yasiyoambukiza Omar Mwalimu alisema hayo kwenye mhadhara wa wazi wa wanafunzi wa vyuo vikuu ulioandaliwa na Mtandao wa Kimataifa wa wananfuzi wa Zanzibar uliofanyika Chuo Kikuu cha Zanzibar Kempasi ya Mpendae.

Alisema kufanya mazoezi ni moja ya sababu ya kupunguza kuongezeka maradhi yasiyoambukiza lakini tatizo ni chakula bora chenye mchanganyiko wa vitu mbali mbali kimekuwa kikikosekana kwa wananchi wengi.

Alisisitiza kuwa kufanya mazoezi kila siku ni jambo la msingi katika kuimarisha afya za wananchi  lakini kuwa muangalifu katika matumizi ya chakula cha kila siku ni kitu muhimu zaidi katika kupambana na maradhi yasiyoambukiza.

Meneja huyo aliwashauri wananchi kubadili tabia na kuwataka kutumia matunda na mboga kwa wingi na kupunguza chakula chenye vichocheo vya kupata maradhi yasiyoambukiza ambayo yamekuwa yakiuwa watu wengi zaidi hivi sasa duniani.

Meneja wa Jumuiya ya Muungano wa Maradhi yasiyoambukiza Zanzibar Zuhura Saleh Amour alisema kisukari ambayo ni moja ya maradhi yasiyoambukiza yamekuwa yakipoteza maisha ya wananchi wengi duniani na nchi zinazoathirika zaidi ni nchi zinazoendelea.

Aliwataka wanafunzi wa vyuo vikuu na wananchi wa kawaida kujenga utamaduni wa kupima afya zao mara kwa mara kwani maradhi hayo yanachukua muda mrefu kugundulika kama mtu hajapima afya yake.

Aliwashauri kuacha kutumia bidhaa zinazotokana na tumbaku kwa vile imegundulika kuwa matumizi ya tumbaku ni miongoni mwa mambo yanayohatarisha kupata maradhi yasiyoambukiza.

Aidha a
lisisitiza umuhimu wa kuweka mbele kujikinga na maradhi hayo kwani yanapokupata matibabu yake yanakuwa magumu na yanachukua muda mrefu kuondoka.

Akifungua mkutano huo, Afisa wa kitengo cha maradhi hayo Omar Abdalla alisema Zanzibar imeongeza maradhi ya homa ya ini, maradhi ya kinywa na ajali kuwa ni miongoni mwa maradhi yasiyoambukiza.

Alisema maradhi hayo mapya na yale maarufu ya sinikizo la damu, saratani, kisukari na maradhi yanayoambukiza kwa njia ya hewa yanachukua asilimia 43 ya vifo vyote vinavyotokea Zanzibar.

Wanafunzi walioshiriki mhadhara huo walikishukuru kitengo cha maradhi yasiyoambukiza kwa kuwapa taaluma kubwa ambayo imewawezesha kujuwa sababu na njia ya kujikinga na maradhi hayo.

Waliahidi kuwa  watakuwa walimu wazuri wa kuwaelimisha wananchi wenzao na kuwa mfano wa kuigwa na wananchi wengine katika sehemu wanazoishi ili kuona wanajikinga na maradhi hayo. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.