STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 17.10.2017
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewapongeza wanafunzi wa Zanzibar waliopata
Daraja la kwanza wa Kidato cha Nne na Kidato cha Sita na kuwaeleza kuwa elimu
haina mbadala.
Hayo aliyasema leo wakati
akizungumza na wanafunzi waliofaulu Daraja la Kwanza katika mitihani ya taifa
ya Kidato cha Nne Ockoba 2016 na Kidato cha Sita Mei 20017, katika hafla
iliyofanyika ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi, Kikwajunu mjini
Zanzibar, ambapo pia, Dk. Shein aliwaandalia chakula maalum cha mchana
wanafunzi hao.
Hafla hiyo imehudhuriwa
na viongozi mbali mbali akiwemo Makamo wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali idd,
Mawaziri, Manaibu Mawaziri, Makatibu wakuu na watendaji wengine wa Serikali, Dk.
Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tokea awamu yake ya Kwanza
ya uongozi hadi hivi leo imekuwa ikitilia mkazo sekta ya elimu.
Alisema kuwa Serikali
imechukua uwamuzi wa makusudi wa kutangaza elimu bure kwa lengo la kuwataka
vijana wote wenye uwezo na wasio na uwezo waweze kusoma na kupata elimu
inayohitajika huku akieleza kuwa ongezeko la wanafunzi waliofanya vizuri mwaka huu
ni kubwa ikilinganishwa na miaka ya nyuma.
Aliwaeleza wanafunzi hao
kuwa bado kazi ya kusoma wanayo ambayo ni kazi ngumu na kuwataka waongeze
jitihada kwani hakuna kazi ngumu kama kusoma lakini akawasibitishia kuwa
wataiweza licha ya ugumu uliopo.
Aidha, aliwataka wanafunzi
hao kwa wale watakaopata fursa ya masomo kwa kwenda nje ya nchi wakumbuke
kurudi nyumbani baada ya kumaliza masomo yao ili waje kuitumikia nchi yao “Mtu
kwao ndio ngao”, alisisitiza Dk. Shein.
Sambamba na hayo, Dk.
Shein alitangaza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mwaka huu itatoa
nafasi 15 za ufadhili wa masomo kutokana na wingi wa wanafunzi mwaka huu, kwani
mwaka jana ilitoa nafasi 10 kama hizo.
Nae Waziri wa Elimu na
Mafunzo ya Amali Zanzibar, Riziki Pembe Juma aliwapongeza wanafunzi hao na
kuwataka kuongeza bidii sambamba na kuachana na vishawishi vya aina zote
ambavyo havitowapelekea kufikia malengo waliyojipangia.
Mapema Katibu Mkuu wa
Wizara hiyo, Khadija Bakari Juma kwa niaba ya Wizara hiyo alitoa pongezi kwa
Dk. Shein kwa kutoa mwaliko huo rasmi kwa mara nyengine tena hivyo kutimiza
ahadi ya kukutana na uongozi wa Wizara pamoja na wanafunzi waliofanya vizuri na
kuwapongeza pamoja na kuwashauri.
Alieleza kuwa hatua hiyo
inathibitisha kwa kiasi gani Rais Dk. Shein anathamini, anajali na yupo tayari
kwa dhati ya moyo na yuko tayari kulisimamia suala la utoaji wa elimu bora kwa
wanafunzi wa Zanzibar na hasa walio wanyonge.
Katibu Mkuu huyo
alieleza kuwa wanafunzi waliohudhuria katika hafla hiyo ni 328 waliofaulu kwa
kiwango cha Daraja la Kwanza kutoka katika skuli mbali mbali za Zanzibar za
Serikali na Binafsi.
Aliongeza kuwa Miongoni
mwa wanafunzi 240 ni wa Kidato cha Nne ambao ni sawa na asilimia 1.76 ya
wanafunzi 13,647 waliofanya mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2016 wakiwemo
wanaume 6,051 na wanawake 7,596.
Aidha, alieleza kuwa
ufaulu huo ni ongezeko la wanafunzi 121 ikilinganishwa na wanafunzi 119
waliofaulu kwa kiwango cha Daraja la Kwanza Kidato cha Nne kwa mwaka 2015.
Sambamba na hayo, Katibu
Mkuu huyo alieleza kuwa wanafunzi 88 wa Kidato cha Sita wamefaulu kwa Kiwango
cha Daraja la Kwanza ambao ni sawa na asilimia 6.2 ya wanafunzi 1,504
waliofanya mtihani wa Kidato cha Sita Mei 2017.
Kwa maelezo ya Katibu
Mkuu huyo, miongoni mwao wanafunzi 744 ni wanawake na wanafunzi 760 ni wanawake
ambapo ufaulu huo ni ongezeko la wanafunzi 38 ikilinganishwa na wanafunzi 50
waliofaulu Daraja la Kwanza mwaka 2016.
Pamoja na hayo, Katibu
Mkuu huyo alieleza kuwa mafanikio hayo yametokana na juhudi mbali mbali za
uongozi wa Wizara ya Elimu, walimu, wanafunzi, wazazi na jamii kwa ujumla.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment