Habari za Punde

WALIOPATIWA MIKOPO BODI YA ELIMU YA JUU ZANZIBAR WATAJWA

Na Khadija Khamis –Maelezo Zanzibar 26/10/2017

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Mh. Riziki Pembe Juma amesema Bodi ya Mikopo ya Elimu ya juu Zanzibar (BMEJZ) imekamilisha kazi ya uteuzi wa waombaji kwa awamu ya kwanza ambapo jumla ya waombaji 1,021  wa ngazi ya  mbali mbali wamepatiwa mikopo
.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisni kwake Mazizini, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali amesema Bodi imefanya uteuzi huo kwa mujibu wa vigezo vilivyowekwa pamoja na vipaumbele vya Serikali.

Alisema Bodi ya Mikopo ya Elimu ya juu Zanzibar ilitoa fomu za maombi 2,675 na fomu zilizorejeshwa ni 2,458.

Akitoa mchanganuo wa walioteuliwa kupatiwa mikopo, Mh. Riziki alisema shahada ya kwanza wanafunzi 983, shahada ya uzamili 34 na shahada ya uzamivu ni wanafunzi wanne.

Alisema jumla ya shilingi 3.7 biioni zinatarajiwa kutumika kulipia gharama za masomo pamoja na posho za wanafunzi kwa waombaji wa mikopo walioteuliwa katika awamu ya kwanza
.
Alisema BMEJZ katika mwaka wa masomo 2017/2018 imepanga kuwapatia mikopo ya Elimu ya Juu waombaji 1,600 shahada ya kwanza, shahada ya uzamili na shahada ya uzamivu.

Waziri Riziki amewataka waombaji ambao hawakuteuliwa katika awamu ya kwanza wawe na subira wakati BMEJZ inaendelea na awamu nyengine za uteuzi wa majina ya waombaji wa mikopo na inasubiri udahili mpya wa Kamisheni ya Vyuo  Vikuu ya Serikali ya Muungano wa Tanzania (TCU).

Akizungumzia uteuzi wa nafasi za ufadhili wa masomo zinazotolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa wanafunzi waliofanya vizuri zaidi mitihani yao ya kidato cha cha sita kwa mwaka 2017/18, Waziri wa Elimu alisema nafasi hizo zimeongezwa na kufikia 15, mwaka jana zilitolewa nafasi 10.

“Nafasi za ufadhili wa masomo wa SMZ zimeongezwa na Mh. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kutoka 10 za mwaka uliopita hadi kufikia 15 mwaka huu hii inatokana na kuongezeka vijana waliofaulu daraja la kwanza kutoka 50 na kufikia 88 mwaka huu,” alibainisha Waziri wa Elimu.

Aidha alisema jumla ya shilingi 64.00 milioni zinatarajiwa kutumika kulipia gharama za masomo kwa wanafunzi waliopata ufadhili wa masomo wa SMZ kwa vyuo vya ndani ya Tanzania

 Waziri wa Elimu aliwakumbusha wazazi kuwapa ushauri mzuri watoto wao wenye sifa stahiki wajiunge na masomo ya kidato cha sita au diploma kabla ya kujiunga na masomo ya shahada ya kwanza ili kuwajengea mustakabali mzuri wa masomo na ajira baada ya kuhitimu masomo yao.

Aliwashauri kuachana na tabia ya kuwapeleka nje ya nchi kujiunga na masomo ya shahada ya kwanza watoto waliomaliza kidato cha nne ambao hawana sifa za kwenda vyuo vikuu kwa vigenzo vya Tanzania.

Nae Mkurugenzi wa Bodi ya Mikopo na Elimu ya Juu Zanzibar Idi Khamis Haji  aliwakumbusha wale wote waliopatiwa mikopo A kutimiza wajibu wao wa kurejesha mikopo hiyo kwa hiyari mara baada ya kuhitimu masomo yao ili kuepukana na adhabu .

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.