STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 24.11.2017

SERIKALI ya Oman imeahidi kuendeleza ushirikiano na
uhusiano wa kidugu na kihistoria uliopo kati yake na Zanzibar sambamba na
kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha
sekta za maendeleo.
Balozi wa Oman nchini
Tanzania Ali Abdalla Al Mahruqi aliyasema hayo leo Ikulu mjini Zanzibar
alipofika kwa ajili ya kujitambulisha na kufanya mazungumzo na Rais wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.
Katika mazungumzo hayo,
Balozi huyo wa Oman alimuhakikishia Dk. Shein kuwa Oman itaimarisha zaidi
uhusiano uliopo kati yake na Zanzibar na kupongeza juhudi zinazochukuliwa na
pande zote mbili katika kuendeleza uhusiano na ushirikiano huku akieleza
dhamira ya Serikali ya Oman kushirkiana na Zanzibar kuendeleza sekta ya elimu,
afya, uvuvi, utamaduni, gesi na mafuta.
Aidha, Balozi Al
Mahruqi alitumia fursa hiyo kutoa shukurani na pongezi kutoka kwa Sultan Qaboos
kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wananchi wake kwa namna walivyoupokea
ujumbe wa Serikali ya Oman uliofika Zanzibar kwa kutumia meli maalum ya Sultan
Qaboos iitwayo “Fulk Al Salamah”
iliyofika Zanzibar hivi karibuni.
Nae Dk. Shein kwa upande wake alitoa shukurani
kwa Sultan Qaboos bin Said kwa juhudi zake anazoendeleza katika kuimarisha
uhusiano na ushirikiano kati ya Oman na Zanzibar.
Dk. Shein alieleza
dhamira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuhakikisha kuwa uhusiano
huo wa kihistoria uliopo kati ya Zanzibar na Oman unaendelezwa kwa manufaa ya
pande mbili hizo.
Aidha, Dk. Shein
alitoa shukurani kwa juhudi zinazoendelezwa na Serikali ya Oman katika kuiunga
mkono Zanzibar kwenye sekta ya afya, elimu, utamaduni pamoja na uhifadhi wa Mji
Mkongwe huku akisisitiza uhusiano kati ya chuo kikuu cha (SUZA) na Chuo Kikuu
cha Sultan Qaboos cha Oman.
Alisema kwamba hivi
sasa nchi mbili hizo zina nafasi ya kushirikiana katika sekta ya mafuta na gesi
asilia kutokana na Oman kupiga hatua kubwa pamoja na uzoefu na utaalamu hali
ambayo itaisaidia Zanzibar kupata kujifunza kutoka kwa wataalamu wa nchi hiyo
na kukuza zaidi ushirikiano na uhusiano uliopo.
Sambamba na hayo, Dk.
Shein pia, alieleza haja ya Zanzibar kushirikiana na Oman katika kuimarisha
sekta ya uvuvi ambapo tayari Zanzibar imeanzisha Kampuni yake ya Uvuvi na
kuhitaji utaalamu na uzoefu kutokana Oman kwa kuzingatia kuwa wananchi na
Serikali ya nchi hiyo zimepiga hatua hatika sekta hiyo.
Dk. Shein alitoa
shukurani kwa Serikali ya Oman kwa azma yake ya kulifanyia ukarabati jengo la
Beit al Ajab pamoja na kukubali kulifanyia ukarabati jengo la “People Palace” kwani nyumba hizo historia kubwa kwa Zanzibar
huku akiahidi kuzifikisha salamu za shukurani kwa wananchi kutoka kwa Sultan
Qaboos kufuatia mapokezi ya ugeni uliokuja kwa meli ya “Fulk Al Salamah”
Wakati huo huo, Rais Dk. Shein
alikutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa
Indonesia nchini Tanzania Rotlan Pardede, Ikulu mjini Zanzibar ambapo
Balozi huyo alieleza azma ya nchi yake kuimarisha ushirikiano na Zanzibar
katika kuimarisha sekta ya elimu ambapo nchi hiyo imeahidi kutoa ufadhili
kupitia progmramu maalum.
Aidha, Balozi Pardede
alimueleza Dk. Shein kuwa Serikali yake itahakikisha inashirikiana na Zanzibar
katika kuendeleza na kuliimarisha zao la mwani pamoja na kuimarisha sekta ya
uvuvi huku akipongeza mashirikiano yaliopo katika sekta ya biashara kati ya
Zanzibar na Indonesia ambapo ndani ya miaka mitatu iliyopita wafanyabiashara
zaidi ya 400 walifanyabiashara nchini humo.
Balozi Pardede alitumia
fursa hiyo kutoa mwaliko kwa Zanzibar katika Mkutano maalum kati ya nchi hiyo
na nchi za Afrika mwezi April mwakani, mkutano ambao utajikita katika masuala
ya uchumi, kilimo, mikakati ya kuimarisha viwanda na ujenzi, teknolojia, na
masuala ya kifedha hatua ambayo itazidisha uhusiano kati ya nchi hiyo na
Zanzibar.
Nae Dk. Shein kwa
upande wake alimueleza Balozi huyo kuwa Zanzibar na Indonesia zina historia na ushirikiano mkubwa kabla ya Mapinduzi
ya Januari 12, 1964 ambapo yalizidi kuimarishwa kuanzia mwaka 1964 na kumuahidi
kuwa Zanzibar itaendeleza uhusiano na ushirikiano huo.
Dk. Shein alitoa
pongezi kwa mafanikio makubwa yaliofikiwa na nchi katika kuimarisha sekta ya
kilimo hasa kilimo cha mpunga, uvuvi, utalii, biashara na sekta nyengine ambapo
mbali ya mafanikio katika sekta ya kilimo pia ina uzoefu wa kulisarifu zao la
mpunga kwa kulifanya vyakula mbali mbali vyenye ladha tofauti.
Dk. Shein katika
mazungumzo hayo alisisitiza haja ya Serikali ya Indonesia kuiunga mkono
Zanzibar katika sekta ya uvuvi kutokana na mafanikio iliyopata nchi hiyo .
Alisisitiza kuwa ni
vyema ikiwa Zanzibar itaimarisha ushirikiano katika kuendeleza uvuvi wa kisasa
hasa katika kufuata makubaliano ya mkutano wa Jumuiya ya Nchi zinazopakana na
Bahari ya Hindi (IORA) uliofanyika mjini Jakata Indonesia mnamo mwezi Machi
mwaka huu ambapo Dk. Shein alihudhuria.
Aidha, Dk. Shein
alifuirahishwa na dhamira ya Indonesia ya kutaka kushirikiana na Zanzibar
katika kilimo na usarifu wa zao la mwani ambapo Balozi huyo alieleza kuwa nchi
yake inajipanga kimarisha ushirikiano katika zao la mwani ambapo badala ya
kuliuza kama mali ghafi litatengenezewa vitu mbali mbali tena hapahapa nchini.
Sambamba na hayo, Dk.
Shein alieleza haja ya nchi hiyo kushirikiana na Zanzibar katika kuimarisha
sekta ya utalii hasa ikizingatiwa kuwa nchi hiyo imepiga hatua kubwa katika
sekta hiyo na kusisitiza haja kwa Wizara zinazohusiana na utalii kati ya nchi
mbili hizo kuwa na mashirikiano sambamba na kuwa na uhusiano kati ya kisiwa cha
kitalii cha Bali kiliopo nchini humo na Zanzibar.
Pia, Dk. Shein
alieleza haja ya kuiamrisha uhuasiano kati ya vyuo vikuu vya nchi hiyo pamoja
na vyuo vya Zanzibar kikiwemo chuo kikuu cha Taifa cha (SUZA), huku viongozi
hao kwa pamoja wakisisitiza haja ya kutembeleana kati ya viongozi na wananchi wa
nchi mbili hizo kwa lengo la kuimarisha uhusiano, utaalamu na kujifunza mambo
mbali mbali.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024
2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment