Habari za Punde

Timu ya Taifa ya Zanzibar Heroes Yakabidhiwa Msaada wa Fedha Kwa Ajili ya Maandalizi ya Kambi Yake.

Na Abubakar Khatib Kisandu, Zanzibar.

Baadhi ya Wanamichezo wameshaanza kujitokeza kuichangia timu ya Taifa ya Zanzibar (Zanzibar Heroes) ambayo inatarajiwa kwenda nchini Kenya kwenye Mashindano ya CECAFA Chalenj Cup.

Miongoni mwa wanamichezo hao waloanza kuichangia timu hiyo ni Mbunge wa Jimbo la Mpendae Salim Hassan Turky ambae amechangia Shilingi Milioni 3 pamoja na baadhi ya Vyakula kwaajili ya Kambi ya timu hiyo inayoanza rasmi Jumamosi.

Mbali ya Turky pia kampuni ya Ndege ya Assalam Air nayo imechangia Shilingi Milioni 2.

Kwa niaba ya Kampuni hiyo Ali Khatib Dai ametangaza kuchangia Milioni mbili ambapo amesema lengo lao ni kuwapa nguvu mashujaa hao wa Zanzibar.

Meneja wa timu ya Zanzibar Heroes Abdul wahab Haji Dau amewataka wanamichezo wengine kujitokeza kuichangia timu hiyo kwani bado hali yao si nzuri kifedha.

"Tunawashukuru hawa walioanza kuchangia leo, tunawaomba na Wadau wengine waichangie hii timu yao kwani bajeti yetu zaidi ya Shilingi milioni 80". Alisema Dau.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.