Habari za Punde

Balozi Seif aahirisha Mkutano wa Nane wa Baraza la Tisa la Wawakilishi

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiahirisha Mkutano wa Nane wa Baraza la Tisa la Wawakilishi Zanzibar katika Majengo ya Baraza hilo yaliopo Chukwani  Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
  Baadhi ya Mawaziri wa SMZ na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wakifuatilia Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar iliyowasilishwa na Balozi Seif.
  Baadhi ya Manaibu Mawaziri wa SMZ na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wakifuatilia Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwenye Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Mwakilishi wa Jimbo la Tunguu Mh. Simai Mohamed Said  wa kwanza kutoka Kulia na Mwakilishi wa Jimbo la Chake Chake Mheshimiwa Suleiman Sarahan Said wakiwa makini kufuatilia Hotuba ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar iliyowasilishwa Barazani.


Picha na – OMPR – ZNZ.



Makamu wa Pili wa Rais  wa Zanzibar  Balozi Seifg AliI ddi amewaomba Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar  kutosubiri kero zinazowakabili Wananchi kuziwasilisha wakati wa vikao vya Baraza la Wawakilishi kwani kufanya hivyo ni kuchelewesha ufumbuzi wa kero zijazowakabili Wananchi wao.


Akiahirisha Mkutano wa Nane wa Baraza la Tisa la Wawakili Chukwani Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar Balozi Seif alisema Serikali kupitia Mawaziri wake iko tayari kusikiliza, kufuatilia na kurekebisha matatizo watakayoyagundua ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa kazi zao.




Alisema Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi ni Sehemu ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Hivyo sifa yake kubwa Serikali hiyo kuwa ni sikivu kwa lolote linalowasilishwa likiwa na maslahi ya Wananchi walio wengi Nchini.

Balozi Seif alieleza kwamba Wawakilishi bado wanabeba jukumu zito la kuisimamia Serikali Kuu kwa lengo la kuleta ufanisi katika shughuli inazozitekeleza




Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifahamisha kwamba moja ya kero kubwa iliyokuwa ikiwasumbuwa Wananchi kwa kipindi kirefu ni suala la usafiri wa Baharini kati ya Visiwa vya Zanzibar na Tanzania Bara
ambalo kwa sasa limeimarika vyema.




Alisema mbali ya kuwepo kwa Boti za  nyingi za abiria na mizigo zinazomilikiwa na Watu Binafsi, lakini Serikali kwa upande wake  nayo imekusudia  kuwa na vyombo vyake  vya usafiri ili kutoa huduma ya uhakika kwa Wananchi wake.




Alieleza kuwa hivi karibuni Serikali imeshakamilisha ununuzi wa Meli ya Mafuta ambayo inategemewa kuwasili Nchini sio muda mrefu, wakati matayarisho ya ununuzi wa Meli nyengine ya Abiria yako katika hatua za
mwisho.




Balozi Seif alisema lengo la Serikali ni kuwa na usafiri wa uhakika wa abiria pamoja na mizigo ili kuchochea ukuaji wa uchumi nchini kwa vile maumbile ya Zanzibar ni Visiwa vinavyohitaji kuwa na usafiri wa uhakika.




Kwa upande wa usafiri wa Anga ambao pia ni kichocheo cha  cha Uchumi, Balozi Seif  akiwa mtendaji Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar alisema  Serikali katika kipindi cha muda mfupi ujao itaendelea na ujenzi wa Jengo Jipya la abiria katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Aman Karume.




Alifahamisha kwamba mradi huo utakapokamilika utaongeza uwezo wa Taifa wa kupokea na kuhudumia ndege nyingi zaidi kutoka Mataifa ya Nje.




Balozi Seif alieleza kuwa Kiwanja hicho ambacho kitakuwa cha kisasa kitasaidia kuimarisha biashara ya Utalii ambayo hivi sasa ndio inayochangia kwa kiasi kikubwa pato la Taifa kwani ndio sekta inayoingiza fedha nyingi za Kigeni katika Taifa.




Akigusia zao la Karafuu ambalo ndio tegemeo la uchumi wa Taifa kwa sasa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema uchumaji na ununuzi wa zao katika msimu huu unaoendelea inakwenda vyema.



Balozi Seif aliwaomba Wananchi hasa wakulima kujitahidi kuanika karafuu zao kwenye majamvi ili wapate karafuu zenye daraja zuri linalokubalika.




Alisema Serikali kwa nia njema ya kuwasaidia Wananchi wake na Wakulima wa karafuu bado inanunua zao hilo kwa bei kubwa licha ya kupungua kwa bei katika soko la Dunia.




Alifahamisha kwamba Shirika la Taifa la Biashara Zanzibar{ZSTC} linanunua karafuu kavu za daraja la kwanza kwa bei ya shilingi 14,000/- , daraja la Pili shilingi 12,000/- na daraja la kwanza shilingi 10,000/-.




Akizungumzia changamoto zinazolikabili zao hilo hadi Tarehe 13 Disemba 2017 Balozi Seif alisema tayari Wananchi 153 wameanguka kwenye Mikarafuu ambapo kati yao wamefariki Dunia.




Alieleza kwamba Serikali kupitia shirika la Taifa la Biashara Zanzibar itaendelea kulipa stahiki za Watu waliohusika na mitihani.




Baraza la Wawakilishi Zanzibar limepokea kujadili na hatimae kupitisha miswaada Minne ya sheria ambayo ni pamoja na Mswada wa Marekebisho ya sheria mbali mbali na kuweka masharti bora ndani yake.




Miswada mengine ni, mswada wa sheria ya kuanzisha Wakala wa Maendeleo ya Viwando vidogo vidogo, na vya kati na mambo mengine yanayohusiana na hayo, Mswada wa sheria ya kuanzisha Wakala wa Usajili wa Matukio ya Kijamii Zanzibar na kuweka Vifungu vya usajili na Mambo mengine yanayohusiana na hayo pamoja na mswaada wa sheria wa kufuta sheria ya Uchaguzi Nambari 11 ya Mwaka 1984 na kutunga sheria ya Uchaguzi ya
Mwaka 2017 na masuala Mengine yanayohusiana na hayo.




Baraza la Wawakilishi Zanzibar limeahirishwa hadi Jumatano ya Tarehe 7 Febuari mwaka 2018.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.