Na. Rajab Mkasab Ikulu.
Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Ali Mohamed
Shein ameutaka Umoja wa Wazazi Tanzania
kujipanga vyema baada ya kupata safu nzuri ya uongozi kuhakikisha Chama Cha
Mapinduzi (CCM) kinaendelea kukamata dola kwa upande wa Tanzania Bara na
Zanzibar.
Makamo Mwenyekiti huyo ambaye pia, ni na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza
la Mapinduzi Dk. Shein aliyasema hayo, huko katika ukumbi wa Jakaya
Mrisho Kikwete mjini Dodoma wakati akiufunga Mkutano Mkuu wa Umoja wa Wazazi wa
Tanzania ulioenda sambamba na uchaguzi mkuu wa Umoja huo.
Dk. Shein alieleza kuwa ana matumaini makubwa kuwa
Umoja huo utaiweza kazi hiyo kwa mashirikiano ya pamoja kutokana na uzoefu wao
mkubwa walionao sambamba na mafanikio makubwa yaliopatikana ndani ya Umoja huo.
Aliwapongeza Wajumbe wa Umoja huo kwa kumchagua kiongozi
Mchumi na kumtaka Mwenyekiti mstaafu Abdallah Majura Bulembo kupumzika kwa kuiendeleza
CCM kutokana na kuwa bado nafasi yake ya Ubunge wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania anayo.
Aidha, aliwapongeza Wajumbe hao kwa kuzingatia
vyema maelezo ya Mwenyekiti wa CCM Taifa Dk. John Pombe Magufuli kwa kuwachagua
na kupata viongozi bila ya kutumia hila na hilba na hatimae kuwapata viongozi
walio bora.
Makamu Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar, Dk. Shein
alitumia fursa hiyo kumpongeza Mwenyekiti mstaafu kwa kutumia juhudi na nguvu
zake kubwa sana katika kuuimarisha Umoja huo ambayo ulikuwa taabani hapo siku
za nyuma.
Rais Dk. Shein alimpongeza Rais Magufuli kwa
maelekezo aliyoupa Umoja huo ya kuwachagua viongozi walio bora na walioimara
ili waweze kuiendeleza Umoja huo uzidi kuimarika huku akisisitiza haja ya kuifanyia kazi hotuba
yake ya ufunguzi aliyoitoa kwani ina maelekezo mengi na mambo mazito.
Aliongeza kuwa Mwenyekiti mstaafu wa Umoja huo
ameweza kuifikisha mahali pazuri sana na Dk. Mndolwa Benard Edmund anapokea
kijiti kutoka kwake na kuendelea kuongoza pale alipopaacha yeye.
Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein aliupongeza Umoja
wa Wazazi wa Tanzania kwa kuwa na mitaji pamoja na miradi waliyoanzisha ukiwemo
mradi wa kujenga jengo kubwa la ghorofa kumi na nne 14, kwa ajili ya kitega
uchumi, mradi ambao utatumia vyanzo vya mapato ya Jumuiya ya Wazazi.
Aidha, Dk. Shein amewataka viongozi wa Umoja huo wakiwemo
wale wastaafu kushirikiana na viongozi wapya huku akiwataka viongozi hao wapya kujidhatiti
katika kipindi cha miaka mitano kwa kushirikiana ili Jumuiya hiyo izidi kupata
mafanikio zaidi yaliokusudiwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM na katika nyaraka
nyengine za chama hicho ukiwemo Mpango Mkakati wa mwaka 2017-2022.
Pia, Dk. Shein aliwataka wale wote ambao
wamegombania nafasi mbali mbali katika Jumuiya hiyo lakini kura zao hazikutosha
wasikate tama kwani uchaguzi ni utaratibu wa kidemokrasia na huchaguliwa mtu
kwa sifa zake, uwezo na viwango vyake na jinsi anavyoshirikiana na wenzake
hivyo aliwataka wakusanye nguvu ili waje kugombania katika chaguzi zijazo.
Nae Mwenyekiti mpya wa Umoja huo Dk. Mndolwa
Benard Edmund aliwaahidi wana Umoja huo kuwa hatowaangusha na kusisitiza kuwa
aliomba nafasi hiyo ili apate kuwatumikia kwa moyo wake wote, akili na uwezo
wake wote katika kuhakikisha CCM inaendela kushinda chaguzi zote zikiwemo za
Serikali za mitaa za mwaka 2019.
Mwenyekiti huyo alieleza atahakikisha kuwa Umoja
huo unajitegemea kutokana na uzoefu wake wa taaluma ya uchumi na kueleza kuwa
atahakikisha anasimamia utawala bora na kupambana na rushwa na kuhakikisha
katika kipjndi kifupi maslahi ya wafanyakazi wa Umoja huo yanasimamiwa na
madeni hasa ya ndani yanakwisha.
Mapema akitangaza matokeo ya uchaguzi wa Umoja huo
Jerry Slaa alimtangaza Dk. Mndolwa Benard Edmund mshindi wa nafasi ya
Mwenyekiti kwa kupata asilimia 68.06 za kura zote na Haidar Haji Abdallah kuwa
Makamo Mwenyekiti.
Wengine waliochaguliwa katika nafasi tatu za
Wajumbe wa Baraza Kuu kwa upande wa Tanzania Bara ni Lulu Abbas Mtemvu, Sudi
Kassim Sudi, Stephan Hiral Ngonyani na nafasi kwa upande wa Zanzibar ni Habiba
Ali Mohammed, Ali Issa Ali na Christina Joram Antoni.
Kwa upande wa nafasi za Ujumbe wa Halmashauri Kuu
ya CCM Taifa kwa Tanzania Bara waliochaguliwa ni Namelock Edward Sokoine, Paul Herman Kirigini
na Mohamed Nassoro Ngingite na kwa upande wa Zanzibar ni Amina Ali Mohamed na
Suleiman Juma Kimea na nafasi Vijana aliechaguliwa ni Omary Ajili Kalolo.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment