Habari za Punde

Matukio 10 Makubwa ya Michezo Zanzibar 2017 yalivyoandaliwa na Mwanamichezo Abubakar Khatib Kisandu




1.YANGA KUCHAPWA 4-0 NA AZAM,  AZAM KUTWAA MAPINDUZI CUP MBELE YA SIMBA

(a) January 7,2017 katika uwanja wa Amaan Zanzibar, Yanga walipata kipigo ambacho hawatokisahau mbele ya Azam Fc kwenye mashindano ya kombe la Mapinduzi baada ya kuchapwa 4-0 na kupelekea kuwa kipigo cha pili kikubwa kwa Yanga kufungwa toka May 6 2012 alipofungwa goli 5-0 na Simba katika uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Magoli ya Azam FC siku hiyo yalifungwa na nahodha wao wakati huo John Bocco , Yahaya Mohamed  Joseph Mahundi  na Enock Atta.
(b) January 13, 2017 timu ya Soka ya Azam Fc ilitwaa Ubingwa wa Kombe la Mapinduzi 2017 baada ya kuifunga Simba bao 1-0 kwa bao lililofungwa na kiungo mkabaji Himid Mao Mkami dakika ya 13 mchezo uliopigwa katika uwanja wa Amaan.

 

2.ZIMAMOTO NA KVZ KUCHEZA CAF NA KUTOLEWA HATUA YA AWALI


Februari 19, 2017 wawakilishi wa Zanzibar na kwenye kombe la klabu bingwa na Shirikisho barani Afrika timu ya Zimamoto na KVZ zilitolewa katika hatua ya awali kwenye Mashindano hayo .


Kwenye klabu bingwa Zimamoto ilitolewa na timu ya Ferroviario Beira ya Msumbiji baada ya kufungwa mabao 3-1 katika mchezo wa mwisho wa ugenini ambapo awali nyumbani walishinda 2-1 hivyo wakatolewa kwa kufungwa jumla ya mabao 4-3.


Na kombe la Shirikisho timu ya KVZ nayo ilitolewa katika mashindano hayo baada ya kufungwa mabao 3-0 ugenini dhidi ya Messager Ngozi ya Burundi baada ya mchezo wa mwanzo uliochezwa Zanzibar KVZ walishinda 2-1, hivyo walitolewa kwa kufungwa jumla ya mabao 4-2.
3.ZANZIBAR KUPATA UANACHAMA KAMILI WA CAF


Machi 16, 2017 ilikuwa ni siku ya furaha kwa Wazanzibar ambapo katika mkutano uliofanyika Mjini Addis Ababa nchini Ethiopia Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) lilitangaza kuwa Zanzibar mwanachama mpya kamili wa 55 wa CAF.


4.MJINI ZANZIBAR WATWAA TENA UBINGWA WA ROLLING STONE

Julai 18, 2017 timu ya Kombain ya Mjini Unguja imefanikiwa kutwaa tena kombe la Mashindano ya Vijana ya Afrika Mashariki na Kati ya Rolling Stone baada ya kuichapa timu ya Fire Boys ya Karatu mabao 2-0 kwenye fainali iliopigwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere uliopo Mbulu Mkoani Manyara.


5.ZANZIBAR YAPOKONYWA UANACHAMA WA CAF

July 21, 2017 ni siku ya huzuni kwa Wazanzibar baada ya

Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) kuwapokonya Zanzibar uanachama wa kudumu wa 55 wa CAF, ambapo Rais wa Shirikisho hilo Ahmad Ahmad alisema haiwezekani nchi moja (Tanzania) kuwa na wanachama wawili kwenye shirikisho hilo, hivyo uanachama huo umedumu kwa siku 128 tu tangu Machi 16 hadi July 21, 2017.


6.MASHINDANO YA RIADHA YA KMKM YALINOGA

Oktoba 29, 2017 Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo Zanzibar (KMKM) kilifanya Mashindano ya mbio za Kilimita 10 ambazo zilianzia Makao Makuu ya KMKM Kibweni na kumalizika katika viwanja vya Maisara huku washiriki kutoka Kenya, Tanzania bara na Zanzibar walishiriki.


7.KWA MARA YA KWANZA ZANZIBAR KUFANYIKA SPECIAL OLYMPIC

Disemba 8, 2017 kwa mara ya kwanza Zanzibar yalifanyika Mashindano ya Olimpik Maalum katika uwanja wa Amaan, mashindano hayo yanashirikisha watu wenye ulemavu wa akili Tanzania nzima walishindana kwenye michezo mbali mbali ikiwemo Soka na Riadha.


8.ZANZIBAR HEROES, KUSHINDA NAFASI YA PILI, KUPOKELEWA KISHUJAA, KUPATIWA MILIONI 3 NA KIWANJA NA DK SHEIN


(a) Disemba 17, 2017 kwenye uwanja wa Kenyatta huko Machakos nchini Kenya timu ya Taifa ya Zanzibar (Zanzibar Heroes) ilishinda nafasi ya pili kwenye Mashindano ya Cecafa Senior Chalenj Cup baada ya kufungwa na wenyeji Kenya kwa Penalty 3-2 kufuatia dakika 120 kwenda sare ya 2-2.


(b) Disemba 18, 2017 Zanzibar Heroes iliwasili nchini wakitokea Kenya katika Mashindano ya Cecafa Senior Chalenj Cup ambapo msafara wa watu 45 ukiongozwa na Waziri wa Habari Utalii Utamaduni na Michezo Rashid Ali Juma uliwasili mchana katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Aman Karume kwa ndege maalum ya Kukodi.
Shangwe, Chereko, vifijo na nderemo vilitawala maeneo yote ya mjini wa Unguja maelfu ya wananchi na viongozi wa kiserikali walijitokeza kuwapokea mashujaa hao, licha ya ndege iliyowabeba watu hao kuchelewa kufika kwenye uwanja wa ndege wa Zanzibar (Abeid Amani Karume International Airport), kwa zaidi ya saa tatu lakini umati wa watu haukupungua hadi timu hiyo ilipowasili majira ya saa sita mchana, Kikosi hicho chini ya Kocha Hemed Suleiman Morocco, kilipowasili kilipokelewa na kupakiwa katika magari ya kifahari huku misururu ya watu wengi wakiwasindikiza kwa kuhinikiza shangwe na vigerere mpaka Mnara wa Kumbukumbu wa Mapinduzi Kisonge Michenzani Mjini Unguja.
Tukio hilo lilionekana kuwa kubwa sana huku wananchi wakisahaua kabisa tofauti zao za kisiasa na kuwa kitu kimoja katika kuwashangilia mashujaa hao, ambao walifanikiwa kushika nafasi ya pili nyuma ya Kenya ambao ndio walikuwa Mabingwa.

(c ) Disemba 23, 2017 ilikuwa ni siku ya kihistoria kwa timu ya mpira wa miguu ya Taifa ya Zanzibar,’Zanzibar Heroes’ baada ya Rais  wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein kuwazawadia viwanja vya kujenga nyumba pamoja na fedha taslim Shilingi milioni tatu kwa kila mchezaji na kiongozi wa timu hiyo.

Zawadi hizo alizitowa katika tafrija maalum iliyofanyika katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la zamani Kikwajuni mjini Zanzibar sambamba na taarab maalum aliyowaandalia timu hiyo iliyotumbuizwa  na kikundi cha Taifa cha Taarab cha Zanzibar kufuatia kufanya vizuri katika mashindano ya mwaka huu ya Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati ‘CECAFA’ na kupata nafasi ya pili.

Dk. Shein alitoa zawadi hiyo kwa kutimiza ahadi yake aliyoitoa siku moja kabla katika viwanja vya Ikulu mjini Zanzibar ambapo akitoa salamu zake na pongezi kwa wachezaji na viongozi wa timu hiyo alikataa kuzitaja zawadi hizo na ambazo jumla yake zilikuwa tatu na aliitaja ile ya taaraab tu na kusema mbili angezitaja siku hiyo.

Vigeregere, hoihoi na nderemo zilisikika katika ukumbi huo kutoka kwa wachezaji na viongozi wa timu hiyo pamoja na hadhara iliyohudhuria tafrija hiyo mara baada ya Rais Dk. Shein kuzitangaza zawadi hizo ambazo kila mmoja alikuwa anasubiri kwa hamu kuzisikia.

Rais Dk. Shein aliwakabidhi hundi ya Shilingi za Kitanzania milioni tatu kwa kila mchezaji na viongozi ambao kwa ujumla wao ni 33 huku akiwaeleza kuwa kwa upande wa viwanja watakabidhiwa si muda mrefu baada ya kukamilika hati zao na nyaraka nyengine muhimu kutoka kwa Wizara husika ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira.


9. ZU KUBEBA KOMBE LA VYUO VIKUU TANZANIA

Disemba 20, 2017 Timu ya soka ya Chuo Kikuu cha Zanzibar University (ZU) ilifanikiwa kutwaa kombe kwenye mashindano ya Vyuo Vikuu vya Tanzania (TUSA CUP) baada ya kuichapa Chuo cha St John cha Dodoma 4-0 mchezo iliopigwa huko Dodoma.

10. ZANZIBAR SAND HEROES KUSHINDA TAJI LA COPA DAR ES SALAM
Disemba 26, 2017 timu ya Taifa ya Zanzibar kwa upande wa soka la Ufukweni (Zanzibar Sand Heroes) ilitwaa kombe la Copa Dar es salam baada ya kuifunga Malawi mabao 3-2 kwenye mchezo wa fainali uliopigwa kwenye fukwe za Coco.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.