Habari za Punde

Miili ya Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania { JWTZ } waliouawa Nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo { DRC } ilipowasili Zanzibar

 Miili ya Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania {JWTZ} ikiteremshwa kwenye ndege ya JW 8029 katika uwanja wa ndege wa  Kimataifa wa Abeid Aman Karume ikitokea Mjini Dar es salaam.
 Balozi Seif pamoja na Mkuu wa Jeshi la Nchi Kavu Meja General Sharif Sheikh Othman wakitoa heshima wakati Miili ya mwashujaa ikiteremshwa kwenye ndege.
 Balozi wa Kuweit Nchini Tanzania Bwana Jassem Alnajem wa kwanza kutoka kushoto akijumuika pamoja na Viongozi wa Kiserikali katika kuipokea Miili ya askari wa Tanzania waliouawa Nchini DRC Wiki iliyopita.
 Mawaziri mbali mbali wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakishuhudia kuwasili kwa Miili yaWanajeshi wa Tanzania waliouawa na waasi wa ADF Nchini DRC.
 Balozi Seif akiongoza Viongozi na Wananchi wa Zanzibar katika kuipokea miili ya Makeshi ya Tanzania yaliyouawa Nchini  Jamuhuri ya Kisemokrasi ya Congo.
 Majeshi ya Wananchi wa Tanzania wakiichukuwa Miili ya Askari wenzao wakiwasili katika Viwanja vya Makao Makuu ya Brigedia Nyuki Migombani kwa ajili ya kuagwa rasmi Kiserikali
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akitoa salamu za pole kwenye shughuli Maalum ya Kuiaga Miili ya Wanajeshi wa JWTZ hapo Migombani Mjini Zanzibar. 
 Balozi Seif akilaani kitendo cha wasi wa ADF Nchini DRC kuwashambulia walinzi wa amani wa JWTZ  waliouwa katika Vikosi vya Umoja wa Mataifa na hatimae kusababisha vifo vyao.
 Balozi Seif akiongoza baadhi ya Mawaziri na Viongozi wa Kitaifa katika kutoa Heshima za mwisho kwa askari Tisa wa Jeshi la Ulinziwa Tanzania hapo Migombani Mjini Zanzibar.
 Balozi Seif akiweka saini kitabu cha maombolezo kufuatia vifo vya askari Tisa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania hapo Migombani Mjini Zanzibar.
 Naibu Mufti  Mkuu wa Zanzibar Sheikh Mahmoud Mussa Wadi akiweka saini Kitabu cha maombolezo kufuatia vifo vya askari Tisa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania hapo Migombani Mjini Zanzibar.
 Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mheshimiwa Zubeir Ali Mulid akiweka saini Kitabu cha maombolezo kufuatia vifo vya askari Tisa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania hapo Migombani Mjini Zanzibar.
 Katibu wa Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Fadhil Soraga akitoa Dua kwa ajili ya kuwaombea Mashuja Askari wa Tanzania waliouawa na waasi wa ADF hapo Migombani.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akimfariji Mama wa Askari wa JWTZ  Iddi Abdulla Ali Mama Shinuna Juma hapo Migombani.
Picha na – OMPR – ZNZ.


Na Othman Khamis , OMPR

Huzuni, Majonzi pamoja na simanzi ilitanda ndani ya Nyuso za Wananchi wa Visiwa vya Zanzibar  wakati ndege iliyochukuwa Miili ya Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania { JWTZ } waliouawa Nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo { DRC } ilipotua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Aman Karume.

Miili ya Wanajeshi hao ililetwa Nchini Tanzania juzi kwa ndege Maalum ya Umoja wa Mataifa ikitokea DRC na kupelekwa moja kwa moja Makao Makuu ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania yaliyopo Lugalo Jijini Dar es salaam kwa ajili ya kukamilisha taratibu za kuiaga rasmi Kijeshi.

Ndege iliyowachukuwa Mashujaa hao wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania ya JW 8029 iliteremsha  Miili ya Askari Nassor  Daudi Ali, Issa Mussa Juma, Hassan Abdulla Makame na Hamad Mzee Kamna.

Wengine  kati ya askari hao Tisa ambapo Mmoja anapelekwa Kisiwani Pemba ni Ali Haji Ussi, Iddi Abdulla Ali, Juma Mossi Ali, Mwinchum Vuai Mohamed na Hamadi Haji Bakari.

Akitoa salamu za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema kuuawa kwa Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania {JWTZ} katika shambulio lililofanywa na Waasi wa ADF Nchini DRC ni la Kinyama lilikiuka misingi ya Haki za Binaadamu ambalo pia ni kinyume na makubaliano ya Ulinzi wa Amani wa Kimataifa.

Alisema Askari hao hawakutakiwa kupigwa, kupiga wala  kupigana kama walivyokuwa wakiwajibika bila ya kuwa na Silaha kubwa katika Ulinzi wa Amani Nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo { DRC}chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa {UN}.

Balozi Seif alitoa kauli hiyo wakati wa tukio Maalum la kuipokea na kuiaga Miili ya Askari  hao 9 kati ya 14 wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania {JWTZ} wakitokea Nchini DRC kupitia Dar es salaam baada ya kushambuliwa na waasi wa ADF na kuuawa Mwishoni mwa Wiki iliyopita.

Alisema  Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  imeshtushwa na Taarifa za shambulio dhidi ya askari hao wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania lililosababisha Vifo na hatimae kuleta simanzi na huzuni kubwa miongoni mwa Watanzania wote ambalo linastahiki kulaaniwa kwa nguvu zote.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa Niaba ya Rais wa Zanzibar, Wazanzibari na Watanzania wote anatoa mkono wa pole kwa wafiwa wote, ndugu, jamaa na marafiki pamoja na Wananchi wote kutokana na msiba huo mzito kwa Taifa.

Balozi Seif alisema msiba huo ni wa Taifa zima kwa vile umemgusa kila Raia wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo jamii kwa wakati huu inapaswa kulichukuwa tukio la vifo vya Mashujaa hao ni amri ya Mwenyezi Muungu, hivyo hawana budi kuupokea mmtihani huo.

Aliwakumbusha Wananchi hasa wale wanaoimani za Dini kurejea katika vitabu vya Dini inavyoelekeza na kufafanua wazi kwamba kila nafsi itaonja mauti na hivyo ndivyo wakati ulivyowakuta Mashujaa hao na tayari wanarejea kwa Muumba wao.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kwamba kilichobakia wakati huu ni kwa Wananchi pamoja na Ndugu na Jamaa wa Mashujaa hao kuwasindikiza kwa kuwaombea safari na malazi mema ili Mwenyezi Muungu awape ridhaa katika safari yao ya lazima.

Mapema Mkuu wa Jeshi la Nchi Kavu Meja General Sharif  Sheikh Othman akimuwakilisha Mkuu wa Majeshi ya ulinzi Tanzania  {CDF} Venance Mabeyo alisema ushirikiano wa Watanzania katika kuipokea Miili ya Mashuja hao umeleta faraja kwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania {JWTZ}.

Meja General Sharif alisema JWTZ ni jeshi la Wanbanchi ambalo jamii inahaki na wajibu wa kushirikiana katika shguhuli za kiulinzi na hata za Kijamii wakati unaporuhusu.

Kamanda Sharif alisema shambulio waliofanyiwa askari wa Jeshi la Tanzania katika ulinzi wa amani Nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo kamwe haliloteteresha Jeshi la Wananchi wa Tanzani aktika ulinzi huo wa Kimataifa.

Aliishukuru na kuipongeza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa jitihada zilizochukuwa katika kuratibu maandalizi ya Miili ya Mashuja hao hadi kuagwa rasmi Kiserikali na baadae kupelekwa kwenye makaazi yao ya kudumu katika Vijiji walivyozaliwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.