Habari za Punde

Hafla ya makabidhiano ya Taasisi ya Wakala wa Serikali wa Uchapaji

 Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohamed Aboud Mohamed akisaini Hati ya makabidhiano ya Taasisi ya Wakala wa Serikali ya Uchapaji iliyohama kutoka Wizara yake na kuhamia Wizara ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale.
Anayeshuhudia akisubiri  na yeye kusaini hati hiyo upande wa Kulia ya Waziri Aboud ni Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale Mh. Mahomud Thabit Kombo.
 Waziri Mohamed Aboud Mohamed wa Pili kutoka Kulia akimkabidhi hati ya makabidhiano ya Taasisi ya Wakala wa Serikali wa Uchapaji  Waziri wa Habari. Utalii na Mabo ya Kale Mh. Mahmoud Thabit Kombo wa pili kutoka Kushoto.
Wa kwanza kutoka kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Shaaban Seif  Mohamed na wa kwanza kutoka Kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale Bibi Khadija Bakari Juma.

Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale Mh. Mahomud Thabit Kombo akizungumza machache baada ya makabidhiano ya Taasisi ya Wakala wa Serikali wa Uchapaji 

Picha na – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis Ame, OMPR
Uongozi wa Wizara ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale umeshauriwa kuhakikisha kwamba Watendaji wa Kiwanda cha wakala wa Serikali wa Uchapaji wanaendelea kupatiwa mafunzo ya Teknolojia ya Kisasa ili waweze kukidhi mahitaji yanayokwenda sambamba na maboresho ya kiwanda hicho yaliyofanywa na Serikali Kuu.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohamed Aboud Mohamed alisema hayo katika hafla fupi ya makabidhiano ya Taasisi ya Wakala wa Serikali wa Uchapaji iliyohamishwa kutoka Ofisi hiyo na kuhamia Wizara ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale.
Hafla hiyo fupi iliyoambatana na utiaji saini makabidhiano hayo yaliyofanywa na Waziri Aboud na mwenzake Waziri wa Habari Mh. Mahmoud Thabiti Kombo ilifanyika katika  Ukumbi wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Vuga Mjini Zanzibar.
Waziri Mohamed Aboud alisema Kiwanda cha Wakala wa Serikali kilipo Maruhubi kimekamilika ufungwaji wa mashine Mpya za Kisasa za Uchapaji lakini changamoto iliyopo ni kwa baadhi ya mashine Mpya kukosa Wataalamu jambo ambalo Watendaji wa Kiwanda hicho watalazimika kujikita zaidi katika kujipatia mafunzo hayo.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuzingatia umuhimu wa Kiwanda cha Wakala wa Serikali wa Uchapaji ililazimika kukipatia Vifaa vya Kisasa ili kiendane na wakati wa sasa wa sayansi na Teknojia.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kwamba lengo la Serikali Kuu la kuanzisha Taasisi hiyo ni kuwatumikia Wananchi pamoja na Taasisi za Umma na zile Binafsi katika masuala yotye ya Uchapaji.
Mheshimia Mohamed Aboud Aboud aliikumbusha Wizara itakayosimamia uendeshaji wa Taasisi hiyo ya Wakala wa Serikali wa Uchagapi kujali maslahi ya watendaji wake kwa lengo la kuendelea kuwapa motisha wa utekelezaji wa jukumu lao kubwa kwa Taifa.
Akipokea jukumu la usimamizi wa Wakala wa Serikali wa Uchapaji Waziri wa Habari. Utalii na Mambo ya Kale Mh. Mahmoud Thabit Kombo alisema Serikali Kuu tayari imeshatoa Muongozo unaoagiza kazi zote za Taasisi za Umma zichapishwe Kiwanda cha Wakala wa Serikali wa Uchapaji.
Waziri Mahmoud ambae ndie aliyepewa jukumu la kuhakikisha machapisho ya Taasisi za Serikali yanapelekwa Kiwanda cha Uchapaji cha Wakala wa Serikali atahakikisha  anafuatilia kazi zote za Taasisi hizo.
Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale aliipongeza Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa juhudi kubwa iliyochukuwa  ya kusimamia uimarishaji wa Kiwanda hicho jambo ambalo limeleta faraja kwa Serikali na Jamii kwa ujumla.
Alisema kazi iliyobakia kwa sasa ni kuhakikisha kwamba Wafanyakazi wa Kiwanda cha Uchapaji cha Wakala wa Serikali wanajikita zaidi katika kujipatia Elimu huku Wizara ikiwaunga mkono katika suala hilo muhimu.
Wakala wa Serikali wa Uchapaji ni miongoni mwa Taasisi za Serikali zilizobahatika kuhamia usimamizi sehemu nyengine kutfuatia mabadiliko yaliyofanywa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi hivi karibuni.
Akitoa shukrani katika hafla hiyo Naibu Waziri Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mihayo Juma N’hunga aliushauri Uongozi wa Kiwanda cha Wakala wa Serikali wa Uchapaji kuangalia uwezekano wa kupatya kazi nyengine za Nje.
Mh. Mihayo alisema ili Kiwanda hicho kijiendeshe na kujitegemea chenyewe Uongozi wake unapaswa kuangalia pia masoko ya upande wa Tanzania Bara  kwa lengo la kutunisha mfuko wake.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.