Habari za Punde

MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA AHUDHURIA UFUNGUZI WA MKUTANO WA CHOGM 2018

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Waziri Mkuu wa Uingereza Bi. Theresa May muda mfupi kabla ya kuingia kwenye ukumbi wa Mkutano Lacanster ambapo Wakuu wa Nchi na Serikali za Nchi za Jumuiya ya Madola Wanakutana jijini London kulia ni Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola Mhe. Patricia Scotland.Makamu wa Rais anamuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli kwenye mkutano huo
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan leo amehudhuria ufunguzi wa Mkutano wa Wakuu wa Serikali wa Jumuiya ya Madola (CHOGM) ambapo anamuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
Mkutano huo ambao Kaulimbiu yake ni “Kuelekea Mustakabali wa Pamoja” unafanyika chini ya Uenyekiti wa Waziri Mkuu wa Uingereza, Mheshimiwa Theresa May na umefunguliwa na Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Malkia Elizabeth wa Pili wa Uingereza.
Majadiliano ya Mkutano wa CHOGM 2018 yatajikita kwenye maeneo manne makuu ya kipaumbele ambayo yatajadili namna Jumuiya ya Madola inaweza kufikia mustakabali wenye ustawi zaidi; mustakabali endelevu zaidi; mustakabali wenye haki zaidi; na mustakabali wenye usawa zaidi.
Mijadala katika maeneo hayo ya kipaumbele itahusisha masuala mbalimbali ikiwemo, kukuza zaidi biashara na uwekezaji baina ya nchi za Jumuiya ya Madola kwa manufaa ya nchi wanachama na Jumuiya nzima; kukuza na kuendeleza misingi ya demokrasia; ajenda ya mabadiliko ya tabia nchi na maendeleo endelevu pamoja na masuala ya uhalifu wa kimataifa kama vile ugaidi, uhalifu wa kimtandao na usafirishaji wa binadamu.
Jumuiya ya Madola ilianzishwa mwaka 1949 kupitia Tamko la London ambalo lilikuwa ni matokeo ya Mkutano wa Mawaziri Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Madola.  Jumuiya ya Madola ina wanachama 53 ambapo kati ya hizo, nchi 19 ni za Afrika, 7 ni kutoka Asia, 13 ni kutoka nchi za Carribean na Mabara ya Amerika, 11 ni kutoka eneo la Pacific na nchi 3 ni kutoka Ulaya.
Makamu wa Rais pia alishahudhuria mikutano mbali mbali inayoambatana na mkutano huo ukiwemo mkutano wa Kuwawezesha Wanawake Kiuchumi pamoja na Mkutano wa Kutokomeza Malaria kabisa.
Katika mkutano huo uliofanyika jana Jioni, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan alipata fursa ya kuzungumzia hatua mbali mbali ambazo Serikali pamoja na Wadau wa Maendeleo wameweza kuzichukua kupambana na Malaria.
Makamu wa Rais alisema Tanzania uwekezaji uliofanyika Tanzania miaka 10 nyuma  imechangia kupunguza kwa kiasi kikubwa Malaria nchini ambapo inatazamia ifikapo mwaka 2020 kutakuwa na maralia chini ya asilimia moja.
Makamu wa Rais aliendelea kusema Tanzania inatambua mchango wa wadau wanaosaidia kupambana kuiondoa Malaria kabisa ambapo huduma mbali mbali zimeboreshwa .
Makamu wa Rais alisema kuwa kwa sasa Tanzania imepiga hatua kwa kuwa na viwanda viwili vya kutengeneza dawa za viua dudu dhidi ya Malaria.
Makamu wa rais alilishukuru Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO) kwa kutambua jitihada za Serikali ya Tanzania dhidi ya Mapambano na Malaria, pia alitoa shukran kwa Bill and Melinda Gates Foundation, Swaziland na Rwanda kwa jitihada vao za kuhakikisha Malaria inarudi nyuma.
Mkutano huo ambao ulihudhuriwa na Bill Gates pamoja na Prince Charles na Viongozi wengine wan chi za Jumuiya za Madola ulibeba kauli mbiu ya “ Tayari Kupambana na Malaria”
No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.