Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo Nd. Shaaban Seif Mohamed wa kwanza Kushoto pamoja na CDR- Hamadi Masoud Khamis wa Kikosi cha Kuzuia Magendo Zanzibar {KMKM} wakitia saini Mkataba wa ujenzi wa Nyumba ya Makaazi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Kisiwani Pemba hafla iliyofanyika Vuga Mjini Zanzibar.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Na Othman Khamis, OMPR
Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar leo imetiliana saini Mkataba na Kikosi cha Kuzuia Magendo Zanzibar {KMKM} juu ya Ujenzi wa Nyumba ya Makaazi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kisiwani Pemba.
Ujenzi wa Nyumba hiyo itakayojengwa sambamba na zile za Wafanyakazi wa Mheshimisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar utafanyika katika eneo la Kijiji cha Pagali kiliopo Magharibi ya Mji wa Chake Chake Pemba.
Kwa upande wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Saini hiyo imetiwa na Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo Nd. Shaaban Seif Mohamed wakati ule wa Kikosi cha Kuzuia Magendo Zanzibar imetiwa na CDR- Hamadi Masoud Khamis hafla iliyofanyika Vuga Mjini Zanzibar.
Akizungumza mara baada ya utiaji saini hiyo Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Shaaban Seif Mohamed alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeamua kujenga Nyumba ya Makaazi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ili kumjengea mazingira mazuri ya uwajibikaji anapokuwa Kisiwani Pemba.
Alisema Ujenzi huo licha ya kukabidhiwa Kikosi cha KMKM katika muelekeo wa kuzijengea heshima Taasisi za Serikali mbele ya Umma lakini pia zinastahiki kupewa kazi hiyo kutokana na uwajibikaji wao mkubwa kubwa unaofahamika.
Naye kwa upande wake CDR – Hamadi Masoud Khamis aliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa kukiamini Kikosi hicho kukabidhiwa jukumu hilo licha ya kazi nyengine ya ulinzi kilichokabidhiwa na Taifa.
Kamanda Hamad kwa niaba ya Mkuu wa KMKM na Wapiganaji wa Kikosi hicho aliahidi kwamba kazi waliyokabidhiwa watahakikisha wanaitekeleza na kuimamilisha katika kuzingatia muda waliopangiwa.
Ujenzi wa Nyumba ya Makaazi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Pagali Chake chake Pemba unatarajiwa kugharimu jumla ya Shilingi za Kitanzania Bilioni Moja, Mia Sita na Sitini na Nne, Laki Moja, Thamanini na Tisa, Mia Saba na Thamanini na Tisa { 1,664,189,789/-}.
No comments:
Post a Comment