Habari za Punde

Watendaji Mamlaka ya ununuzi wapewa mafunzo ya kiutendaji


Baadhi ya watendaji wa mamlaka ya manunuzi wakiwa katika mafunzo ya Kiutendaji huko katika ukumbi wa Maktaba Chake Chake -Pemba.


PICHA NA JAMILA ABDALLA SALIM -MAELEZO.

 Ofisa Mdhamini Wizara ya Fedha Pemba , Ibrahim Saleh Juma, akifunguwa mafunzo ya kiutendaji kwa watendaji wa Wizara hiyo wakiwemo, maofisa manunuzi wamikoa ,Watendaji wa mamlaka ya manunuzi , mabaraza ya miji
na halmashauri huko katika ukumbi wa mikutano wa maktaba Chake Chake-Pemba.

PICHA NA JAMILA ABDALLA SALIM-MAELEZO.
Baadhi ya watendaji wa mamlaka ya manunuzi wakiwa katika mafunzo ya Kiutendaji huko katika ukumbi wa Maktaba Chake Chake -Pemba.

PICHA NA JAMILA ABDALLA SALIM -MAELEZO.


NA/JAMILA ABDALLA –MAELEZO-- PEMBA.  


Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar , haiko tayari kuona fedha za Serikali zinapotea kiholela kutokana na watumishi wake  kufanya matumizi yasiyozingatia sheria za fedha na manunuzi .

Afisa mdhamini Wizara ya Fedha Pemba, Ibrahim Saleh Juma,
aliyasema hayo  wakati akifunga mafunzo ya wiki moja juu ya usimamizi wa sheria ya manunizi na uondoaji wa mali za umma kwa watendaji wa mamlaka ya manunuzi,Maofisa manunuzi wa Mikoa Mabaraza ya Miji na Halmashauri huko katika ukumbi wa mikutano  wa maktaba kuu Chake Chake.

Alieleza wizara ya Fedha haitosita kuwachukulia hatua za kinidhamu watendaji watakao bainika kufanya udanganyifu katika manunuzi ya mali za Umma kwani kufanya hivyo ni kurudisha nyuma  juhudi za kukuza uchumi wa nchi.

Afisa mdhamini  huyo, alifahamisha kwamba Serikali inatumia zaidi ya asimia 75% ya manunuzi ya vifaa na huduma za Serikali, hivyo aliwataka watendaji hao kuacha tabia ya kufanya kazi kwa mazoeya na kutumia  fursa walioipata ya mafunzo kuondoa mizozo na migogoro wakati wa utekelezaji wa majukumu yao kutokana na kulalamikiwa kwa kiasi kikubwa.

Aidha mdhamini huyo, aliwataka watendaji hao kuwa na imani na Serikali yao kwa kufanya kazi kwa bidii na uzalendo na pale wanapohamishwa katika eneo moja kwenda eneo jengine la kazi waone kuwa ni utaratibu wa kisheria na sio adhabu.

Naye mkufunzi wa mafunzo hayo, Onesmo France, aliwataka washiriki hao kuwa waangalifu  na mikataba wakati wa utekelezaji wa miradi na kuweka kumbukumbu za manunuzi  wakati mradi unaendelea  ili kujiepusha na migogoro inayoweza kujitokeza.
“Ili kuitendea haki  sheria ya manunuzi na uondoaji wa mali za Umma sheria no. 26 ya 2016  ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar , juu ya usimamizi na manunuzi  ndio sababu kuu ya mafunzo haya kuwajengea uwezo  katika uwajibikaji  wa shughuli za  maendeleo” , alisema Mdhamini  Ibrahim.

Akizungumzia suala la changamoto wanazokabiliana nazo  Watendaji hao, Ibrahim, alisema  pamoja na mapungufu  yaliyopo na changamoto ndogo ndogo  tayari  Wizara ya Fedha imeanza kuzifanyia kazi na  isiwe sababu kwa watendaji hao kudumaa na kuendelea kuwepo kwa kero zinazolalamikiwa katika manunuzi.

“Kiukweli makae mkijuwa kwamba ZPPDA, CAG, Anti Corruption na vyombo vyengine havitavumilia  vitendo vya rushwa ,udanganyifu na uzembe   na kusababishia hasara Serikali”, alisema Mdhamini huyo.

Alifahamisha  uteuzi wa maafisa hao  umefanywa kutokana na vigezo na viwango vya elimu zao , hivyo kufanya uzembe katika manunuzi na mikataba isiyofuata sheria haitovumiliwa, kwa kufanya ukaguzi kila mara  na atakaebainika  kufanya udanganyifu wa aina yoyote ataadhibiwa kisheria .

Onesmo France, mkufunzi wa mafunzo hayo amesisitiza mikataba  isiyo na hasara kwao na  wakandarasi,uwekaji sahihi  wa kumbukumbu ,mawasiliano katika usimamizi na uwajibikaji wenye tija ,misingi na maadili ya manunuzi na uondoaji wa mali za Serikali,sifa na vigezo vya uhalali wa zabuni,taratibu za kufanya thamani ,Uandaaji wa ripoti na utunzaji wa mikataba  ili kuepuka migogoro isiyo ya lazima.

“Migogoro katika kazi haiwezi kuwa na nafasi pindi mtakapofanya kazi kwa kufuata  sheria na taratibu ambazo zimewekwa kwa mujibu wa sheria unaotambulika “,alisema Mkufunzi huyo.

Kwa upande wa washiriki waliitaka wizara ya fedha kuwaandalia tena mafunzo kama hayo yenye kutowa muongozo katika utendaji wa majukumu yao kwani ni mafunzo ambayo yatawawezesha kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi.

Hivyo walisema  muda ambao umewekwa kwa mafunzo waliyopewa ulikuwa ni mdogo ukizingatia na wingi wa mada zilizowasilishwa na ni mada  muhimu kwao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.