Habari za Punde

Waziri atembelea Taasisi ya Nyaraka, wakala wa uchapishaji

 KITABU kilichosheheni kazi ya utafiti iliyofanywa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, baada ya kukamilisha masomo yake ya udaktari (PHD) mwaka 1988.
 WAZIRI wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar Mahmoud Thabit Kombo, akiangalia vitabu vya utafiti wa PHD za Rais wa Zanzibar awamu ya tano Dk. Salmin Amour Juma (alichokishikilia) na kile cha Rais wa sasa Dk. Ali Mohamed Shein (kilicho mezani), alipotembelea Taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu, Kilimani mjini Unguja.  

WAZIRI wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale Mahmoud Thabit Kombo na wasaidizi wake, wakipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Wakala wa Serikali wa Uchapaji Zanzibar Muhammed Suleiman Khatib, kuhusu utendaji kazi wa mitambo mipya.


MKURUGENZI wa Wakala wa Serikali wa Uchapaji Zanzibar (ZAGPA) Muhammed Suleiman Khatib (Kushoto), akimueleza Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale Mahmoud Thabit Kombo, na watendaji aliofatana nao, namna gazeti la Zanzibar Leo linavyopitia njia mbalimbali za uchapishaji.

GAZETI lililojulikana kwa jina la KWEUPE toleo Namba 76, la tarehe 10 Agosti, 1963 ambalo lilikuwa likichapishwa Zanzibar, kama linavyoonekana lililohifadhiwa kwenye taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu Kilimani mjini Unguja.

PICHA ZOTE NA SALUM VUAI, MAELEZO-ZANZIBAR 



Na Salum Vuai, MAELEZO

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar, imesema inajipanga kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazoikabili Taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu iliyoko Kilimani mjini Unguja, ili ifanye kazi kitaalamu zaidi.

Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale Mahmoud Thabit Kombo, akiwa katika ziara ya kuzitembelea taasisi zilizo chini ya wizara yake leo Mei 4, 2018, amesema teknolojia ya kisasa inahitajika katika kutunza na kuhifadhi kumbukumbu za kihistoria ili ziendelee kuishi miaka mingi bila kuharibika.   

Alieleza kuwa, katika kufanikisha suala hilo, tayari Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imesaini mkataba na wenzao wa Oman, utakaotoa fursa kwa wafanyakazi wa taasisi hiyo kupatiwa mafunzo yatakayowawezesha kutumia vifaa vya kisasa katika kuhifadhi kumbukumbu hizo.

Mkataba huo uliosainiwa mwanzoni mwa wiki hii mjini Muscat nchini Oman wakati Waziri huyo alipofanya ziara pamoja na viongozi kadhaa wenye dhamana ya kutunza nyaraka na mambo ya kale, pia utaangalia uwezekano wa kuipatia vifaa vya kisasa taasisi hiyo.

“Ziara yetu tuliyoifanya nchini Oman hivi karibuni, imefungua milango ya matumaini kupata msaada wa utaalamu na vifaa kwa ajili ya kutunza nyaraka na kumbukumbu nyengine za kale kwa njia za kisasa zikiwemo za kieletroniki,” alisema Waziri Thabit.

Waziri huyo amesema Oman ambayo ina uhusiano wa kihistoria na Zanzibar kwa miaka mingi sasa, imeonesha dhamira ya kweli kusaidia katika jambo hilo, fursa aliyosema serikali inapaswa kuichangamkia kikamilifu ili nyaraka muhimu za nchi na nyenginezo, zidumu katika hali nzuri na kutumika kwa shughuli mbalimbali ikiwemo tafiti.     

Mapema, Mkurugenzi wa taasisi hiyo Salum Suleiman Salum pamoja na wakuu wa vitengo tafauti, walisema wanafanya kazi katika mazingira magumu, kutokana na ukosefu wa vifaa vya kisasa, pamoja na kutokuwa na nafasi ya kutosha kutunza nyaraka na kumbukumbu muhimu za taifa.

Waziri huyo na wasaidizi wake, pia walitembelea Wakala wa Serikali wa Uchapaji Zanzibar (ZAGPA) Maruhubi, ambako pamoja na mambo mengine, walishuhudia mitambo ya kisasa inayotumika kuchapishia nyaraka, majarida, kalenda, risiti na vitu vyengine mbalimbali.

Mkurugenzi wa Wakala huo Muhammed Suleiman Khatib, alisema pamoja na mafanikio wanayopata, wanakabiliwa matatizo katika kuhifadhi vifaa kutokana na ghala ndogo waliyonayo ambayo haikidhi mahitaji.

Hata hivyo, aliziomba taasisi za serikali, binafsi pamoja na watu mbalimbali, wenye kuhitaji huduma za uchapishaji, kuutumia wakala huo akisema sasa umeimarishwa kwani mitambo yake ni ya kisasa na yenye kutoa machapisho yenye viwango bora.

Waziri Thabit, pamoja na kushauri njia mbalimbali za kuimarisha utendaji wa taasisi alizozitembelea, aliahidi kuzifanyia kazi changamoto zilizoelezewa ili kuleta ufanisi na tija katika taasisi hizo na serikali.

Aidha aliwapongeza wafanyakazi na viongozi wa taasisi hizo kwa moyo wao wa kizalendo katika kuwajibika, huku akiwashajiisha kujifunza zaidi ili kwenda sambamba na ulimwengu wa kisasa.

Akitoa muhtasari baada ya kukamilisha ziara hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale Khadija Bakari Juma, alisema wamejifunza mengi katika uhalisia wa taasisi hizo.

“Ziara hii na nyengine zilzotangulia awali katika taasisi zetu, zimetupa mwanga wa kujua namna ya kujipanga ili kutekeleza majukumu yetu katika dhamana  hizi mpya tulizokabidhiwa na Mheshimiwa Rais, na tunaahidi tutashirikana kwa manufaa ya nchi yetu,” alieleza.

IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO-ZANZIBAR
4 MEI, 2018  


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.