Habari za Punde

Mkutano wa kutathmini masuala ya Ukimwi kwa kipindi cha mwaka mmoja wafanyika Zanzibar

  Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika linalosaidia huduma za afya Tanzania (thps) Dkt Redemta Mbatia akitoa maelezo katika Mkutano wa wadau juu ya masula ya Ukimwi uliofanyika katika ukumbi wa Hotel ya Verde iliopo Mtoni Mjini Zanzibar.
 Naibu Spika wa Baraza Wawakilishi  Mgeni Hassan Juma akifungua Mkutano wa wadau wa Ukimwi   uliofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Verde iliopo Mtoni Mjini Zanzibar  (kulia) Mwenyekiti Kamati ya Ustawi wa Jamii Mwaasha Khamis (kushoto) Mkurugenzi Mtendaji (thps) Redemta Mbatia na Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Asha Ali Abdulla.
 Msaidizi Meneja wa Kitengo Shirikishi Ukimwi Homa ya Ini kifua kikuu na Ukoma Issa Abeid Mussa akiwasilisha mada juu ya hali halisi ya maradhi ya Ukimwi hapa Zanzibar.
 Baadhi ya washiriki wa mkutano wa wadau wa Ukimwi wakisikiliza mada zilizokuwa zikiwasilishwa katika mkutano huo.
Mgeni Rasmi Naibu Spika wa Baraza la wawakilishi Mgeni Hassan Juma akimkabishi cheti cha ufanyakazi bora kwa huduma za Maabara ya huduma za ukumwi CTC  katika Hospitali ya Mnazimmoja Najaat Mohamed Khatib.


Picha na Abdalla Omar Maelezo  Zanzibar

Na Mwashungi Tahir      Maelezo Zanzibar      29-6-2018.
Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Mgeni Hassan Juma amesema jitihada zaidi  zinahitajika katika   mapambano   dhidi ya   ukimwi hasa katika makundi maalum ikiwa ni pamoja na wanaotumia madawa ya kulevya kwa njia ya kujidunga, wanaotumia madawa ya kulevya na  wanaojamiana kwa   jinsia moja.
Makundi hayo yapo kwa asilimia 2-19 hali ambayo bado haijaridhisha  na elimu zaidi inatakiwa itolewe kwa makundi hayo ili waweze kujitambua na kuweza kujikinga na kupata maambukizi ya virusi vya Ukimwi.
Hayo ameyaeleza huko katika ukumbi wa Verde Hotel ulioko mtoni   wakati alipokuwa akiufungua mkutano siku moja wa wadau wa kupambana na Ukimwi ambao umeweza  kutathmini kazi kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendeleza jitihada zake kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo kwa kuwapatia huduma mbali mbali wanaoishi na virusi vya Ukimwi sambamba na kutoa elimu ili kwa jamii ili kuondosha maambukizi mapya.
Amelishukuru Shirika Tanzania Health Promotion Support  (thps) kwa kazi kubwa wanayoifanya ili kunusuru makundi hayo kwa kuwapatia taaluma ambapo kwa kiasi kikubwa baadhi yao wameacha kutumia dawa za kulevya na kujidunga.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa shirika la  Tanzania Health Promotion Support (Thps) Redempta Mbatia amesema taasisi yao imekuwa ikishirikiana sana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa lengo la kupambana na Ukimwi ambapo kwa kiasi kikubwa kumeweza kufanikiwa.
Amesema katika mapambano hayo wameweza kuwapa mafunzo ya kuwajengea uwezo kwa wafanyakazi wa sekta ya Afya, kuwapatia huduma na elimu kwa wale  ambao wanaoishi na virusi vya ukimwi.
Alisema kwa wale ambao wako katika makundi hatarishi wameweza kuwapatia taaluma ya  kuweza kupunguza athari walizozipata kwa wale ambao tayari wameathirika kwa kuwapatia huduma za kupunguza maambukizo.
 Mapema Msaidizi Meneja wa Kitengo Shirikishi Ukimwi Homa Ini Kifua kikuu na Ukoma Issa Abeid Mussa amesema jitihada kubwa zinafanyika katika kupambana na ukimwi ili ifikapo mwaka 2030 kuweza kuondosha kabisa maambukizi ya Ukimwi.
 Alisema kutokana na hatua mbali mbali zinazochukuliwa ikiwa na pamoja na ushirikishwaji wa  utoaji wa taaluma kwa wananchi na utoaji wa huduma nzuri kwa wananchi kumeweza kufanikiwa kwa asilimia 90 hapa nchini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.