Habari za Punde

Man Utd 0-3 Tottenham: Mourinho Ataka Waandishi wa Habari Wamuheshimu Baada ya Kipigo

Kipigo cha Jumatatu usiku dhidi ya Tottenham ndio kikubwa zaidi kwenye ligi kwa Mourinho kwenye uwanja wa nyumbani toka aanze maisha ya ukocha.

Kocha wa Manchester United Jose Mourinho amewataka waandishi wa habari kumuheshimu baada ya timu yake kupata kipigo cha magoli 3-0 wakiwa uwanja wa nyumbani dhidi ya Tottenham.
Mourinho akionekana kukerwa na maswali ya waandishi, alinyanyuka kitini na kukatisha mahojiano na wanahabari baada ya mchezo huo uliopigwa katika uga wa Old Trafford.
Kipigo hicho cha Jumatatu usiku ndio kikubwa zaidi akiwa uwanja wa nyumbani toka aaze maisha yake ya ukocha, na pia kwa mara ya kwanza amepoteza michezo miwili kati ya mitatu ya mwanzo ya ligi.
"Nimeshinda mataji mengi ya ligi (ya England EPL) kuliko makocha wote 19 (wa timu nyengine zinazoshiriki EPL) ukiwaweka pamoja," amesema Mourinho. "Nimeshinda mataji matatu na wao mawili."
"Heshima, heshima, heshima bwana," aling'aka Mourinho akitoka kwenye chumba cha mikutano ya wanahabari.
Goli la kichwa la nahodha Harry Kane na mawili mengine yaliyofungwa na Lucas Moura yameipa ushindi wa tatu mfululizo Tottenham na kuwapandisha mpaka nafasi ya pili kwenye msimamo wa EPL.
Mourinho, raia wa Ureno amenyenyua taji la EPL mara tatu kwa vipindi viwili tofauti akiwa na Chelsea, wakati Pep Guardiola na Manuel Pellegrini wakishinda mara moja kila mmoja wakiwa na Manchester City.
Mreno huyo pia ameshinda mataji mawili ya ligi ya Ureno akiwa na Porto, mawili Italia akiwa na Inter Milan, na moja Uhispania akiwa na Real Madrid. Pia ameshinda mataji mawili ya klabu bingwa Bara la Ulaya. Taji kubwa zaidi alilolitwaa na Man United ni kombe la Europa mwaka 2017.
"Mnataka kama kufanya muujiza juu ya timu yangu, ambayo ilicheza vizuri na kwa mpango, tulikuwa vizuri sana lakini mmekuja hapa na mnajaribu kuugeuza mkutano huu kwa kuniangushia mzigo wa lawama," alifoka Mourinho.
Alipoulizwa namna United walivyojilinda dhidi ya Spurs, alikuwa na haya ya kusema: "Samahani. Inabidi uniambie kitu gani ni muhimu zaidi maana sielewi. Pale ninapopata ushindi, ninapokuja hapa mara nyingi tu mnaniambia hamkufurahishwa na namna timu ilivyocheza."

'Wachezaji hawamtaki Mourinho'

Mshambuliaji wa zamani wa Blackburn na Chelsea, Chriss Sutton ameiambia BBC kuwa inaonekana kama wachezaji wa Man United hawamtaki kocha wao.
Sidhani kama Spurs walikamia mchezo toka dakika za awali, lakini pale walipoweka mguu chini, wakaitawala timu ambayo haina uongozi. Kuna lawama nyingi zinatolewa kwa sasa na wachezaji wanaonekana hawataki kucheza chini yake (Mourinho)."
Kwa mujibu wa Sutton, kwa kiwango kilichooneshwa na kama kocha angekuwa ni Louis van Gaal basi mashabiki wangekuwa wanaimba nyimbo za kutaka atimuliwe.
"Rekodi ya Mourinho ni nzuri kweli, lakini kama Man United wanataka kukubaliana na uduni, basi hiyo ndiyo hali yao kwa sasa. Man City na Liverpool wapo katika kiwango tofauti kabisa," amesema Sutton na kuongeza, "Ni aibu kupokea kipigo cha 3-0 na sijui baada ya hapa, wao kama timu au kocha wataelekea wapi."

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.