Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akizungumza na Viongozi mbali mbali na Wanadiaspora katika Kongamano la Tano la Diaspora Tanzania lililofanyika leo katika ukuimbi wa Uwanja wa Tibirinzi Chake chake Mkoa wa Kusini Pemba.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amewataka Diaspora kutambua kuwa wana jukumu
lililosawa la kuijenga Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mujibu
wa nafasi na uwezo walionao, ikiwa kwa kiuchumi au kielimu.
Dk. Shein aliyasema hayo
leo katika ufunguzi wa Kongamano la tano la Diaspora linalofanyika huko katika
viwanja vya kufurahishia watoto Tibirinzi Chake Chake Pemba.
Katika maelezo yake,
Rais Dk. Shein aliwataka wanadiaspora katu wasiwe miongoni mwa kundi la
wachache wanaodharau nchi zao kwa maendeleo yaliyofikiwa na nchi nyengine.
Alisema kuwa maendeleo ya
kweli hayaji kwa kutupiana lawama na hayaji kwa misingi ya utashi bali
maendeleo ya kweli yanahitaji bidii na maarifa katika utetekelezaji wa majukumu
yao, umoja na mshikamano pamoja na matumizi mazuri ya rasilimali zilizopo.
Aliongeza kuwa Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar imekamilisha Sera ya Diaspora ambayo ilizinduliwa
rasmi tarehe 09 Mei, 2018 kwa lengo la kuhakikisha mipango ya maendeleo.
Pamoja na mambo mengine
Rais Dk. Shein alieleza kuwa Sera inaeleza na kufafanua mipango ya Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar katika kuwashirikisha Wanadiaspora katika fursa za
kijamii na kiuchumi zilizopo kwa Wanadiaspora na namna bora ya kuzitumia fursa
hizo.
Hivyo, Dk. Shein
aliiagiza Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa na Uratibu wa Wazanzibari Wanaoishi
Nchi za Nje iliopo katika Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
kuhakikisha kwamba kopi ya Sera hiyo inawekwa katika Tovuti ya Idara kwa haraka
iwezekanavyo ili Wanadiaspora wengi zaidi wapate kuisoma na kuifahamu.
Pamoja na hayo,
alimuagiza Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyeiti wa Baraza la Mapinduzi
Issa Haji Gavu kuunda Jukwaa rasmi la Diaspora la Zanzibar ambalo kabla ya
Kongamano la Diaspora Jukwaa hilo likae kwa kupanga taratibu za Kongamano.
“Kila kiumbe kina
mapenzi ya nyumbani, na mara nyingi hata wadudu mbali mbali kama nyuki, huwa
tayari kujitoa muhanga kwa ajili ya kutetea nyumbani kwao, nyumbani ni
nyumbani, anayependa kwao ndie mzalendo halisi”,alisema Dk. Shein.
Aidha, Dk. Shein alisema
kuwa hivi sasa suala la kuwashirikisha Wanadiasora katika kuimarisha maendeleo
ya nchi zao za asili limepewa umhimu wa pekee na nchi mbali mbali duniani
pamoja na Mashirikiano ya Kimataifa.
Alisema kuwa tarehe 5
Julai, 2006 akiwa Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alialikwa
kuhudhuria mkutano wa “Inteletuals From
Africa and Diaspora” kwa niaba ya Rais Jakaya Kikwete huko Salvador, Bahia
nchini Brazil ambapo mkutano huo ulieleza umuhimu wa Wanadiaspora kuchangia
maendeleo ya nchi zao.
Alieleza kuwa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania imeamua kuandaa mikakati mbali mbali ya kuwashirikisha
Wanadiaspora katika kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo, ambapo Ilani ya
CCM ya Uchaguzi Mkuu ya mwaka 2010-2015 ilianza kuweka mikakati maalum juu ya
ushiriki wa Wanadisapora katika kuijenga nchi yao.
Dk. Shein aliahidi
kwamba atahakikisha Kongamano hilo linaandaliwa kila mwaka ili kuweza kukutana
na Wanadiaspora hasa katika kipindi hichi cha baina ya mwezi wa Juni na Septemba,
huku akieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuweka bajeti
maalum kila mwaka juu ya Kongamano hilo.
Sambamba na hayo, Rais
Dk. Shein aliwahakikishia Wanadiaspora kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
inawakaribisha kuja kuekeza Zanzibar na kuwahakikishia kuwa suala la ardhi
wasiwe na wasi wasi kwani wahusika wapo akiwemo Waziri anaeshughulikia Ardhi
pamoja na Mkurugenzi wa ZIPA.
Pia, Dk. Shein aliwasihi
Wanadiaspora kuendelea kuwa Mabalozi
wazuri wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika nchi wanazoishi na kuendelea kuwa
mfano wa tabia njema ili kuendeleza sifa ya ukarimu, urafiki na usalama ambayo
raia wa Tanzania wamejijengea na inatambulika katika mataifa yote duniani.
Aliwataka kuendelea
kuishi kwa kuzingatia misingi ya urafiki, udugu na sheria ya nchi hizo
wanazoishi huku wakiwa na mapenzi makubwa baina yao pamoja na nchi yao ya asili
pamoja na kuimarisha Jumuiya zao ili ziendelee kuwa daraja la kuwaunganisha
kati yao na wale waliopo nyumbani pamoja na taasisi zinazogusa maslahi yao.
Pamoja na hayo aliwataka
kuendeleza kwa ari na kasi utamaduni wa kuja kutembelea nyumbani kila baada ya
muda jambo ambalo ni muhimu na linaimarisha mapenzi huku akiwasisitiza
wanapokuja nyumbani wafanye jitihada za kuja na watoto wao.
Nao Wanadiaspora
walimpongeza Rais Dk. Shein kwa kukubali kushirikiana nao katika Kongamano hilo
sambamba na kuwa karibu na Wanadiaspora huku akiwa mshiriki mkubwa wa maendeleo
yao.
Pia, walieleza azma yao
ya kujikusanya ili kuweka nguvu kwa pamoja badala ya kufanya kazi kwa mtu mmoja
mmoja kwa lengo la kuweza kutoa msaada mkubwa zaidi.
Katika hafla hiyo, Dk.
Shein pia, aligawa Sera kwa Wanadiaspora waliofika katika Kongamano hilo huku
akitumia fursa hiyo kueleza mipango ya Serikali ya Kujenga miji mipya ya kisasa
pamoja na kuuongeza mji wa Zanzibar kwa kufukia bahari katika eneo la Gulioni
na kueleza azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuanzisha vyuo vikuu vipya
viwili ambacho kimoja kitajengwa katika eneo la Fumba.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment