Habari za Punde

BENKI ZINAZOTOA MIKOPO YA KILIMO TANZANIA BARA NA ZANZIBAR ZATAKIWA KUFUATA VIGEZO VYA UKOPESHAJI

Na. WFM
Serikali imezitaka Benki zote zinazotoa mikopo ya kilimo 
Tanzania Bara na Zanzibar kuhakikisha zinatoa mikopo kwa 
kuzingatia vigezo vya ukopeshaji vikiwemo kuangalia 
historia ya mkopaji ili kuondoa mikopo Chechefu (NPL).

Hayo yameelezwa Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri 
wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, alipokuwa 
akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Bububu Mhe. 
Mwantakaje Haji Juma, aliyetaka kujua utaratibu 
unaotumika kutoa mikopo kwa wakulima wa Zanzibar 
kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB).

Dkt. Kijaji alieleza kuwa kabla ya kutoa mkopo ni lazima 
Benki ijiridhishe na aina ya mradi wa mkopaji ikiwa utaleta 
faida itakayomuwezesha mkopaji kurejesha mkopo huo kwa 
wakati ili kuzuia ukuaji wa Mikopo Chechefu.

Akijibu swali la msingi la Mbunge huyo aliyetaka kujua ni 
wananchi wangapi wanaonufaika na mikopo ya Kilimo kwa 
upande wa Zanzibar, Dkt. Kijaji alisema kuwa jumla ya 
wananchi 3,000 wamenufaika na mikopo ya Benki ya TADB 
hadi kufikia Julai 31, 2018.

“Kati ya wanufaika hao 3000, idadi ya wanaume 
walionufaika ni 1800, wanawake 900 na vijana wa kike na 
kiume ni 300”, alieleza Dkt. Kijaji.

Alisema kuwa jumla ya mikopo ya shillingi bilioni 6.50, 
imetolewa kwa wananchi hao wa Zanzibar hadi kufikia Julai 
31, 2018.

Imetolewa na;
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Wizara ya Fedha na Mipango.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.