Habari za Punde

Maadhimisho ya Siku ya Usafi Duniani yafana Kisiwani Zanzibar.


Na.Abdi Shamnah Zanzibar.
Wadau wanaotumia fukwe za bahari nchini wametakiwa kuweka vifaa maalum kwa ajili ya kuhifadhia taka zinazozalishwa na binadamu, ili kuepuka uharibifu wa mazingira.

Hayo yameelezwa na wananchi mbali mbali walioshiriki katika zoezi la usafi wa mazingira katika fukwe za bahari ya Muyuni Kijini, skuli ya msingi Mbuyu Tende pamoja na Kijini.

Zoezi hilo lililowashirikisha walimu, wanafunzi, wafanyakazi wa Hoteli ya Mnemba Island, mapapasi  pamoja na wananchi , limeratibiwa na Kampuni ya Penny Royal kupitia mradi wa Best of Zanzibar, ikiwa ni maadhimisho ya siku ya Afya Duniani. 

Akizungumza na washiriki wa zoezi hilo, Mkuu wa Wilaya Kaskazini ‘A’ Unguja, Hassan Ali Kombo alisema kuna umuhimu mkubwa kwa wananchi wa ukanda wa Pwani kujenga utamaduni endelevu wa kufanya usafi katika maeneo wanayoishi, ikiwemo fukwe ya bahari.

Alisema ni vyema kwa watumiaji wa fukwe za bahari, ikiwemo watembeza watalii kuweka vifaa maalum  ili kuhifadhia taka, kwa kuzingatia kuwepo ongezeko kubwa la mabaki ya vifaa vitokanavyo na plastik, kama vile chupa za maji, lotion na kadhalika.

Alisema ili kuondokana na magonjwa mbali mbali ya miripuko pamoja na kuvutia wageni, kuna ulazima kwa jamii kujibidisha katika suala la kufanya usafi katika maeneo yao.

‘‘Halmashauri iandae utaratibu wa kuweka vifaa katika maeneo ya fukwe na yale yenye uzalishaji mkubwa wa taka, ili kuangalia uwezekano wa baadhi yake kuzifanyia ‘recyling’ baaade’’, alisema.

Mkuu huyo wa Wilaya aliipongeza Kampuni ya Penny Royal kupitia mradi wa Best of Zanzibar kwa hatua zake za kuunga mkono juhudi za Serikali ya Wilaya hiyo katika kuimarisha usafi wa mazingira katika maeneo mbali mbali.

Mapema, Mkurugenzi wa Mradi wa Best of Zanzibar Aminata Keita, alisema zoezi hilo lililowashirikisha wanafunzi limelenga kuwajengea utamaduni wa kuendeleza usafi katika maisha yao.

Alisema skuli za Kijini na Mbuyutende zinapitiwa na mradi mkubwa wa ujenzi wa Hoteli ya Kitalii, ambapo kw anykati tofauti zimekuwa zikihusishwa katika programu mbali mbali ikiwemo elimu ya Afya.

Alisema zoezi hilo limelengwa kuondokana na mrundikano wa takataka zinazozalishwa na binadamu, ikiwemo mifuko ya plasiti na mabaki mengine ya vifaa vinavyotokana na matumizi ya binadamu katika eneo la ukanda huo.

Nae, Ofisa kutoka Mamlaka ya Mazingira Zanzibar Hashim Salum Hashim, alipongeza juhudi na mwamko wa wananchi wa maeneo hayo kwa kujitokeza kwa wingi kushiriki katika Kampeni hiyo ya jusafi wa mazingira.

‘‘ Tuna kila sababu ya kupongeza, mwamko wa jamii ni mkubwa, kiasi ambacho wageni wanaonekana kufurahia sana, unaona wale kama ingelikuwa fukwe sio safi, katu wasingeweza  kulala pale kwenye mchanga, juhudi iliyofanyika inafaa kupongezwa’’, alisema Salum.

Alitowa wito kwa watembeza watalii na wadau wengine wanaoambatana na wageni kwa ajili ya mapumziko kwenye fukwe hizo, kuandaa utaratibu wa kuweka vifaa, ili kuhifadhi mabaki ya bidhaa wanazotumia.

Alisema wageni ikiwemo watalii ni aina ya watu waliojengeka katika utamaduni wa kutii sheria, hivyo ni dhahiri  pale patakapokuwa na  vifaa hivyo, hawatosita kuvitumia.

Mwanafunzi Mariamu Hassan kutoka Skuli ya Mbuyu tende alisema ni muhimu kwa jamii kuwa na utaratibu endelevu wa kufanya usafi katika maeneo wanayoishi, ili kuondokana na matatizo mbali mbali ikiwemo ugonjwa wa mri[puko.

Alisema zoezi hilo limefanikiwa vyema, hivyo na kusisitiza umuhmu wa kuendeleza utamaduni wa kufanya usafi katika maeneo mbali mbali ikiwemo fukwe za bahari, kwani ni eneo hilo moja la vivutio vya utalii.

Wastani wa wananchi 200 walishiriki katika zoezi la usafi wa mazingira katika maeneo hayo, ambapo kiasi cha tani saba za taka zilikusanywa.   

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.