Habari za Punde

Maktaba Kuu watakiwa kubuni mbinu za kushajiisha kusoma

Na Takdir Ali,

Uongozi wa Maktaba kuu nchini umetakiwa kubuni Mbinu za kuwahamasisha Wananchi kupenda kusoma kupitia Maktaba ikiwa ni pamoja na kuwazawadia wale watakaojitokeza mara kwa mara kujisomea katika Maktaba nchini.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu Zanzibar Suleiman Yahya Ame huko Maktaba kuu Maisara wakati alipokuwa akizindua Tovuti ya Shirika hilo ilioambatana na Kongamano maalum la kujadili njia bora za kuongeza idadi ya watumiaji wa Maktaba hapa nchini.
Amesema Serikali imechukuwa juhudi za kujenga Maktaba lakini  bado kuna changamoto ya Idadi ndogo ya Wananchi wanaojitokeza kujisomea.
Amefafanua kuwa hali hiyo hupelekea kurudisha nyuma juhudi za Serikali za kuhakikisha Wananchi wanapata elimu kupitia Nyanja mbali mbali ikiwemo matumizi ya Makataba.
Amewashauri kuandaa Matamasha maalum ya wazi kama yanayofanywa na baadhi ya Nchi nyengine za Afrika Mashariki ikiwa ni njia ya kuihamasisha jamii kubadilika na kukupenda kujisomea.
Amesema kupitia Maktaba Wananchi wanaweza kuzitumia Maktaba kujifunza masuala mbalimbali yanayoweza kuwasaidia katika harakati zao za kielimu na kijamii.
Kwa Upande wake Mkururugenzi wa Shirika la huduma za Maktaba Zanzibar Sichana Haji Foum amesema ili kuhakikisha Wananchi wengi wanajitokeza kutumia Maktaba wameamua kutoa elimu kwa jamii na Wanafunzi tofauti Unguja na Pemba.
Mbali na hayo amewaomba Wadau wa Maktaba kushirikiana na Serikali Kuhakikisha malengo yaliowekwa na Serikali yafikiwa hasa ikizingatiwa kwamba Serikali imetumia gharama nyingi kufanikisha suala hilo.
Nao baadhi ya Washiriki wa Kongamano hilo wameliomba Shirika la huduma za maktaba Zanzibar kuendelea kutoa elimu kwa jamii ili iweze kupata uelewa juu ya suala hilo na kuweka vitendea kazi vinavyokwenda na wakati uliopo wa Sayansi na Teknolojia.
Hata hivyo wamewaomba Wakutubi kuzingatia Taratibu na Sheria zilizowekwa wanapoingia Maktaba ikiwemo kuwa na utulivu wa hali ya juu ili kuondosha usumbufu wanaoupata Wateja wanaokwenda kupata huduma katika Makataba hizo.
 Imetolewa na Idara ya Habari Maelezo Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.