Habari za Punde

Milioni 68 tayari zimeshatumika kituo kipya cha kuegeshea magari Kijangwani

Na Ali Issa, Maelezo Zanzibar   
Zaidi ya shilingi milioni 68.9 zimetumika kwa ajili ya matayarisho ya kituo kipya cha kuegeshea magari kiliopo Kijangwani mjini Unguja.
Hayo yamesemwa leo Baraza la Wawaakilishi na Naibu Waziri Ofisi ya Rais,Tawalaza Mikoa na Idara malumu za SMZ,  Shamata Shaame Khamis wakati akijibu suali la Mwakilishi wa Jimbo la Paje Jaku Hashimu Ayuob alietaka kujua gharama zilizotumika hadi sasa katika mataarisho ya eneo hilo.
 Naibu Waziri alisema gharama zilizotumika ni kwa ajili ya kazi za usafishaji, uwekaji na ushindiliaji wa kifusi katika eneo hilo.
Akizungumzia ujenzi wa vyoo vinavyoendelea kujengwa katika eneo hilo, Naibu Waziri alisema unasimamiwa na Taasisi ya UMAWA kwa gharama zao wenyewe.
Naibu Shamata aliongeza kuwa kituo hicho kipya cha daldala kipo katika hatua ya mwisho kukamilika na hivi sasa Wizara inatafuta   mkandarasi wa kuweka lami ili kianze kutumika.
Katika hatua nyengine alisema katika kituo hicho kutajengwa mabanda kwa ajili ya abiria  na sehemu ya watu wenye mahitaji malumu.
Wakati huo huo Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Mohamed Aboud Mohamed amesema Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania inatoa  gawio kuipa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mambo ya Muungano kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BOT).
Alisema gawio hilo linalopewa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar limekuwa likiongezeka kila mwaka.
Waziri Aboud alikuwa akimjibu Mwakilishi Jaku Khamis Hashimu Ayoub aliyeulizia kuhusu gawio la Zanzibar kutoka Serikali ya Muungano, na idadi ya mashirika na tasisi za muungano ziliopo Zanzibar.  
Alisema Serikali ya Muungano wa Tanzania inaendelea kutoa elimu kwa wananchi  kufahamu masuala ya muungano na umuhimu wake na itaendelea kutoa elimu hiyo kupitia vyombo vya habari, semina, makongamano na  kuzishirikisha taasisi nyengine kwani muungano huo unaumuhimu mkubwa kwa wananchi wa pande zote mbili.
Alisema Taasisi za Muungano na mashirika yake yaliopo Zanzibar ni 26 na baadhi sio ya biashara na hayachangii chochote.
Hata alisema mapato yote yanayokusanywa Zanzibar na TRA yanabakia Zanzibar katika mfuko mkuu wa hazina ya Zanzibar.
Aliyataja baadhi ya Mashirika na Taasisi za Muungano ziliop Zanzibar kuwa ni pamoja na Jeshi la Wananchi wa Tanzania,  Polisi, Uhamiaji, Usalama wa Taifa, Mambo ya nje, Tume ya haki za binaadamu, NIDA, Mamlaka ya haliya hewa, Tume ya pamoja ya elimu ya juu, Bima, Bahari kuu, Shirika la Posta, Shirika la Simu (TTC), Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na TRA.
IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.