Habari za Punde

Madaktari Bingwa 20 Kutoka Nchini Saudi Arabia Wawasili Zanzibar.

Na Miza Kona - Maelezo Zanzibar  12/10/2018
WIZARA ya Afya Zanzibar imepokea ujumbe wa Madaktari 20 kutoka nchini Saudi Arabia kwa ajili ya kutoa huduma mbali mbali kisiwani Pemba.
Ujumbe huo kutoka katika Shirika lisilo la Kiserikali litakuwepo nchini kwa ajili kutoa huduma za upasuaji wa aina mbali mbali pamoja na huduma nyengine bure kwa lengo la kuwasaidia wananchi kisiwani humo.
Akizungumza mara baada ya kuwasili ujumbe Mratibu wa Masuala ya Nchi Rafiki kutoka Wizara ya Afya Khadija Khamis Shaaban amesema ujumbe huo utakaa nchini kwa muda wa siku 11 ambao utatoa huduma ya upasuaji pamoja na kutoa misaada mbali mbali kwa wananchi wa kisiwa cha Pemba
Bi Khadija maefahamisha kuwa upasuaji huo utanza tarehe 13 hadi tarehe 24 mwezi huu katika hospitali ya Chake chake na Wete ambapo huduma zinaratajiwa kuanza asubuhi hadi saa tatu usiku kwa siku zote hizo.
Amesema lengo la shirika hilo ni kuwasaidia wananchi wenye matatizo mbali mbali ambayo yanahitaji kuwafanyiwa upasuaji bila malipo ili kuweza kupata matibabu ya matatizo waliyonayo
Amezitaja huduma zitakazotolewa madaktari hao ni pamoja na upasuaji wa goita, mabusha, utengenezaji wa midomo sungura, upasuaji wa mifupa, matatizo ya uvimbe kwa akina mama na watoto waliongua kuwekwa sawa.
Amefahamisha kuwa madaktari hao pia watatoa elimu kwa madaktari wazalendo kwa lengo la kuimarisha utoaji huduma pamoja na kutoa  msaada wa dawa wenye thamani ya zaidi ya sh. milioni 24 ambazo zitasaidia wananchi hao.
Aidha amewataka wananchi kisiwani humo kujitokeza kwa wingi kupata huduma hiyo kwani madaktari hao ni wataalamu wazuri na wenye kutoa huduma iliyobora  nchini.
“Kwa kweli ni madaktari bingwa wenye utaalamu wa kisasa na wanatoa huduma nzuri wananchi wasiwe na wasiwasi wajitokeze kwa ili waweze kupata huduma hizo kwa wataalamu hao”, alifahamisha mratibu huyo.
Nae Daktari bingwa kutoka Shirika hilo Profesa Tarik Habib amesema ujio wao huo ni kuweza kuwasaidia wananchi wenye matatizo mbali mbali ambayo yanahitaji upasuaji pamoja na kutoa huduma nyengine za kijamii.
Shirika hilo la Kiislamu lisilo la kiserikali kutoka nchini Saudi Arabia WAMY limekuwa likilisaidia nchi za Afrika misaada mbali mbali ya kijamii kwa sasa ni mara ya tatu kufunga kambi ya utoaji huduma ya afya nchini.  

 IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO ZANZIBAR  

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.