Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Azungumza na Mkurugenzi wa Mtendaji wa Zanzibar School of Healthy.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif na Mkurugenzi Mtendaji wa Zanzibar School of Healthy Bibi Aziza Hemed wakibadilishana mawazo juu ya namna ya kuimarisha Chuo cha Afya cha Kwa Mchina Mwanzo kinachoisaidia Serikali kuongeza idadi ya Watoa huduma katika Sekta ya Afya Nchini.
Picha a – OMPR – ZNZ.

Uongozi wa Chuo cha Afya kwa Mchina Mwanzo {Zanzibar School of Healthy –ZSH} umeipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kitendo cha Kihistoria ilichokithibitisha kwa Umma cha Kusaini Mkataba wa Mgawanyo wa Uzalishaji wa Mafuta na Gesi Asilia {PSA} baina ya yake na Kampuni ya Kimataifa ya RAKGAS ya Nchini Ras Al – Khaimah.
Mkurugenzi Mtendaji wa Zanzibar School of Healthy Bibi Aziza Hemed alitoa pongezi hizo kwa niaba ya Uongozi wa Chuo chake wakati wa mazungumzo yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kuelezea malengo la Chuo kicho ya kutaka kutanua wigo wa mafunzo mengine Chuoni hapo.
Bibi Aziza Hemed alisema Wananchi waliowengi Nchini wamejenga matumaini makubwa yakionyesha mwanzo mwema wa Taifa kuendelea kufungua zaidi fursa za Kiuchumi na ustawiwa Jamii.
Alisema wakati dalili za matarajio ya kuongezeka kwa ajira kupitia Sekta hiyo Mpya Nchini inaanza kutoa mwanga, Wananchi hasa Wanafunzi wanapaswa kuendelea kushirikiana na Serikali katika mtazamo wa kujikita zaidi katika Masomo ya Sayansi kwa nia ya kujiweka sambamba na Mradi huo Mpya Nchini.
Bibi Aziza akiwa Mwanataaluma alishauri kuundwa kwa chombo cha Wataalamu kitakacho waunganisha na kuwaendeleza wahitimu Bora wa Masomo ya Sayansi katika ngazi ya Sekondari na Vyuo ambao baadae Taifa litakuwa na uhakika wa Wataalamu watakaoziba mapengo ya wale wanaofikia ukingo wa kustaafu.
Akizungumzia maendeleo ya chuo chake Mkurugenzi huyo wa Zanzibar School of Healthy alisema yapo mafanikio makubwa yaliyopatikana tokea kuanzishwa kwake mnamo mwaka 2013 baada ya kupata baraka na kibali kutoka Nacte mwaka 2012 kufuatia kukamilisha taratibu zote za Chuo.
Alisema ushirikiano mkubwa uliyopata Uongozi wa Chuo hicho kutoka Serikalini umewezesha kuzalisha wahitimu zaidi ya 960 ambapo kwa mwaka hukadiria kuzalisha wahitimu 200 wenye vigezo na sifa zinazowawezesha kutoa huduma katika Hospitali na Vituo vya Afya Zanzibar na baadhi yao Tanzania Bara.
“ Najisikia raha na faraja ninapokwenda kutaka huduma za Afya ama iwe Hospitali kubwa au Vituo vya Afya nimekuwa nikikutana na Wanafunzi wangu wakija kunihudumia jambo ambalo napaswa kujivunia”. Alisema Bibi Aziza.
Mkurugenzi huyo wa Zanzibar School of Healthy alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa kwamba Uongozi wa Taasisi hiyo umejipangia kujenga Majengo yake ya kudumu ili kutanua wigo wake kwa vile  maeneo wanayotumia hivi sasa ya Majengo yanaanza kuonekana finyu kulingana na ongezeko la Wanafunzi wake.
Naye kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliupongeza Uongozi wa Chuo hicho kupitia Mkurugenzi wake huyo Mtendaji kutokana na uamuzi wake wa kuanzisha chuo hicho ikiwa ni jambo la msingi litaloendelea kuungwa mkono ya Serikali Kuu.
Balozi Seif alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar bado inahitaji kuimarisha Sekta ya Afya kwa kuongeza Hospitali na Vituo vya Afya Nchini  vitakavyohitaji Watendaji zaidi ili kutoa huduma bora kwa Wananchi wake.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimueleza Mkurugenzi huyo Mtendaji wa Zanzibar School of Healthy wapo Vijana wanaosahau wajibu na maadili yao ya kazi wakati wa kuwahudumia Wananchi ndani ya kipindi kifupi baada ya ajira jambo ambalo huleta bughdha na kuwaondolea matumaini Wananchi.
Balozi Seif alimshauri Mkurugenzi huyo kupitia Uongozi wa Chuo chake kuandaa utaratibu  maalum wa kuwafuatilia Wanafunzi waliopata taaluma kwenye Chuo hicho ambao kwa sasa wanatoa huduma katika vitengo mbali mbali ili kujiridhisha iwapo wanachokifanya kinakwenda sambamba na mafunzo waliyopata.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.