Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein. Akutana na Mratibu wa UN Hapa Zanzibar.

 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) alipokuwa akisalimiana na Mratibu wa Umoja wa Mataifa (UN) hapa Zanzibar Bibi.Dorothy Temu-Usiri (katikati) alipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo akiwa na ujumbe aliofuatana nao
 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) alipokuwa akizungumza na ujumbe wa Mratibu wa Umoja wa Mataifa (UN) hapa Zanzibar Bibi.Dorothy Temu-Usiri (wa pili kulia) walipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo
 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) alipokuwa akizungumza na ujumbe wa Mratibu wa Umoja wa Mataifa (UN) hapa Zanzibar Bibi.Dorothy Temu-Usiri (wa pili kulia) walipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) alipokuwa akiagana na  Mratibu wa Umoja wa Mataifa (UN) hapa Zanzibar Bibi.Dorothy Temu-Usiri baada ya mazungumzo alipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo akiwa na ujumbe (hawapo pichani),[Picha na Ikulu.] 25/10/2018.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amepongeza juhudi zinazochukuliwa na Umoja wa Mataifa (UN) katika kuendeleza miradi mbali mbali ya maendeleo na kueleza kuwa kuanzishwa kwa “Program ya Pamoja ya Zanzibar” (ZIP) itakuwa ni kichocheo cha mafanikio.

Rais Dk. Shein aliyasema hayo leo Ikulu mjini Zanzibar wakati alipokuwa na mazungumzo na Mratibu mpya wa Umoja wa Mataifa (UN) kwa eneo la Zanzibar Bi Dorothy Temu-Usiri.

Dk. Shein alieleza kuwa kutokana na uzoefu mkubwa wa utendaji kazi wa Mratibu huyo ana matumaini makubwa kuwa program hiyo sio tu itasaidia kuimarisha maendeleo ya Zanzibar bali itasaidia sana katika kufikia malengo ya maendeleo yaliyowekwa na Umoja wa Mataifa (UN) hapa nchini.
Rais Dk. Shein alisema kwamba, malengo ya Mashirika ya Umoja wa Mataifa kwa Zanzibar yako wazi katika kila sekta na yanafahamika kwa wananchi wote wa Zanzibar jinsi yalivyolenga katika kuimarisha sekta za maendeleo.
Alisema kuwa (UN) imekuwa ikifanya kazi na kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta mbali mbali  ikiwemo elimu, afya, upatikanaji wa maji safi na salama, utawala bora, uimarishaji wa haki za binaadamu, uwezeshaji, mapambano ya udhalilishaji wa kijinsia pamoja na uhifadhi wa mazingira.
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa shukurani kwa Mashirika ya Umoja wa Mataifa (UN) kwa mashirikiano inayotoa katika kuimarisha miradi mbali mbali ya maendeleo hapa Zanzibar hasa katika masuala ya wanawake na watoto.
“Programu ya Pamoja ya Zanzibar” (ZIP), inayohusisha Mashirika tisa ya UN, aliizindua Rais Dk. Shein hivi karibuni hapa Zanzibar ambapo katika uzinduzi huo alisisitiza haja kwa wafanyakazi kuleta mabadiliko ya fikra na mawazo na kuacha kufanya kazi kwa mazoea ili kuweza kuifanikisha progamu hiyo kwa ufanisi mkubwa.
Katika maelezo yake, Rais Dk. Shein alimuhakikishia Mratibu huyo kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na viongozi wake itaendelea kutoa mashrikiano makubwa kwa Umoja huo pamoja na viongozi wake wote wakiwemo wale wanaofanya kazi zao katika ofisi za Umoja huo hapa Zanzibar.
Alisisitiza kuwa Programu ya pamoja ni mradi wa kipekee unaolenga kuwawezesha watoto, vijana na wanawake hivyo ni matumaini yake makubwa kuwa malengo yaliokusudiwa yatafikiwa kwa lengo la kutatua changamoto zilizopo.
Mratibu mpya wa Umoja wa Mataifa (UN) kwa eneo la Zanzibar Bi Dorothy Temu-Usiri nae kwa upande wake alimpongeza Rais Dk. Shein kwa juhudi anazozichukua katika kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar na kuahiadi kuwa (UN) itaendelea kumuuunga mkono.

Mratibu huyo wa Umoja wa Mataifa kwa eneo la Zanzibar alieleza uzoefu wake wa kazi kwa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla pamoja na nje ya Tanzania na kusisitiza kuwa atahakikisha anatumia uzoefu wake katika kutekeleza majukumu yake hayo mapya.

Bi Dorothy alimueleza Rais Dk. Shein mipango na mikakati iliyowekwa na Umoja wa Mataifa katika kuhakikisha “Program ya Pamoja ya Zanzibar” (ZIP) inafikia malengo yake na kuleta mafanikio makubwa kwa Zanzibar na watu wake.
Mratibu huyo alimuhakikishia Rais Dk. Shein kuwa mbali na program hiyo pia, juhudi za makusudi atazichukua katika kuhakikisha program nyengine zinafanikiwa na kuleta tija kwa Zanzibar.
Sambamba na hayo, alisisitiza kuwa Umoja wa Mataifa kupitia ofisi zake zilizopo Zanzibar utaendelea kutoa ushirikiano wake kwa Zanzibar kwa kuzingatia mipango na mahitaji yaliyowekwa.
Mratibu huyo alieleza azma za (UN) za kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha sekta za maendeleo.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.